Na Gurian Adolf -Kalambo
BAADHI ya wakazi waliopo vijiji vya mwambao wa Ziwa Tanganyika mkoani Rukwa, wamekuwa wakitumia vyandarua vinavyotolewa bure na Serikali kwa wajawazito na watoto kujikinga na malaria kuvulia samaki.
Wakizungumza na gazeti hili jana, baadhi ya wakazi hao walidai wamekuwa wakitumia vyandarua katika shughuli za uvuvi, kilimo na ufugaji kwa kuwa nyavu maalumu za shughuli hizo hazipatikani wilayani humo.
Mmoja wa wakazi hao, Rosemary Mtepa alisema baadhi wamekuwa wakitumia vyandarua kutega samaki Ziwa Tanganyika, wengine wakivitumia kuzungushia bustani ili kuzuia kuku kuingia na kuharibu mazao yao.
Alisema pamoja na kutambua nia ya Serikali kuwapa wajawazito vyandarua hivyo, wamekuwa wakipuuza matumizi hayo na badala yake kutumia katika matumizi wanayoyajua wenyewe.
Diwani wa Kata ya Kasanga, Jacob Chisenga alikiri kuwapo matumizi mabaya ya vyandarua.
Alisema limekuwa tatizo kubwa ambalo linawasumbua wakazi wa eneo hilo la mwambao mwa ziwa.
Chisenga alisema elimu ya matumizi ya vyandarua bado inahitajika eneo hilo kama njia ya kuwasaidia wananchi kukabiliana na malaria.
Ofisa Afya Wilaya ya Kalambo, Richard Manuma alisema kipindi hiki ambacho wameanza kuandikisha majina kwenye kaya, kila moja itapewa vyandarua viwili.