30.4 C
Dar es Salaam
Friday, September 24, 2021

Aeleza mawe kwenye figo yalivyomtesa miaka saba

Na AVELINE KITOMARY

Afya njema humfanya mwanadamu kufurahia maisha yake ya kila siku, huku akiendelea na kazi ya kujenga uchumi.

Lakini mambo huwa tofauti pale mwili unapokuwa na maumivu, hapa mtu hushindwa kabisa kufanya chochote kutokana na kuathirika kiafya.

Ugonjwa unaweza kufanya mtu asiwe na furaha na mafanikio katika maisha yake.

Hili limedhihirika kwa Mwajuma Mohamed (44) , mkazi wa Gongolamboto jijini Dar es Salaam, ambapo ugonjwa wa figo ulimtesa kwa muda wa miaka saba.

Mwajuma anasema licha ya kuwa na maisha ya furaha kwa muda mrefu, huzuni iliingia mwaka 2014 wakati alipoanza kuumwa.

Anasema kwa kipindi cha miaka mitano alihangaika hospitali kadhaa bila kupata suluhisho la tatizo lake kutokana na ugumu wa kujua maradhi yanayomsubua.

“Niliweza kwenda hospitali mbalimbali kutafuta tiba baada ya kuanza kupata maumivu makali sehemu ya tumbo huku awali nikifikiri ni kibofu cha mkojo.

“Katika hospitali kadhaa za kawaida nilizopita waliniambia ninaumwa U.T.I lakini hata nilivyopewa dawa maumivu yalitulia kwa muda mfupi na baadae kurudi.

“Baada ya kuona hali inaendelea kuwa vilevile nikaamua kwenda hospitali ya Jeshi (hakutaja jina lake) huko nilipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili hata hivyo, kwa kipindi cha kwanza nilipewa dawa,” anasimulia Mwajuma.

Anabainisha kuwa kwa kipindi cha miaka mitano alilazimika kutumia dawa hizo huku maumivu yakiwa yanajirudia mara kwa mara asijue la kufanya.

“Dawa hizo zilikuwa zinatuliza maumivu kwa muda tu na zikiisha naanza kupata maumivu tena lakini ilivyofika mwaka 2019 nilipangiwa kufanyiwa operation wakati huo madaktari wakaniambia nina jiwe kubwa katika figo na lilikuwa limekaa vibaya hapo ndipo nilijua tatizo linalonisumbua.

“Baada ya kufanyiwa upasuaji nikawa nahudhuria kliniki na maumivu yakatulia kabisa, lakini baada ya kukaa maumivu yakaanza kurudi tena nikalazimika kurudi hospitali kwa mara nyingine,” anaeleza.

Mwajuma anasema hakuwahi kuthubutu kutumia dawa za asili za tiba mbadala kutokana na kuogopa madhara ya dawa hizo hasa kwa figo.

“Sikutaka kwa sababu wanasema tiba mbadala inaharibu figo nikawa naogopa kuua figo kwa kutumia dawa za kienyeji.

Anasema kuwa baada ya kurudi hospitali alipewa dawa za kutuliza maumivu huku daktari akimuahidi kufanyiwa vipimo zaidi.

“Nilifanyiwa kipimo cha CT Scan nikaambiwa jiwe bado linaonekana lipo na nikaambiwa nitumie tu dawa za kutuliza maumivu.

“Baada ya kukaa mwaka huu mwanzoni nikarudi tena, daktari akaniambia kuwa wanataraijia kufunga mashine mpya ambayo itakuwa njia rahisi ya matibabu hivyo niendelee kusubiri wataniita,” anabainisha.

CORONA YAMZUIA

Anasema kuwa baada ya kuitwa tena na daktari alimpa rufaa ya kwenda Mloganzila ambapo ndipo atakapoenda kupata matibabu.

“Lakini wakati ule kulikuwa na tishio la ugonjwa wa corona hivyo nilivyofika huko wakaniambia wamesitisha kupokea wageni nikalazimika kurudi nyumbani.

“Nilivyorudi sikuwa na bahati kwa sababu waliniambia mashine bado inasumbua kidogo, nikarudi tena nyumbani baada ya mwezi mmoja daktari akanipigia simu akaniambia niende mashine tayari imeshaanza kazi,” anaeleza.

APATA MATIBABU YA KISASA

Mwajuma anasema baada ya kurudi hospitali alipewa huduma ya kuvunja mawe kwenye figo kwa njia ya mawimbi mshtuko.

“Ilichukua muda mfupi na nilipata maumivi kidogo tu lakini pia nilipewa dawa za
maumivu huku dakatari akinisisitiza kunywa maji mengi.

“Kwa sababu niliwekewa mrija ikabidi nilale niweke miguu juu huku nikinywa maji mengi nilivyofanya hivyo nikawa najisaidia haja ndogo kwenye chombo ili kuangalia kama mawe yanatoka.

“Wakati nikienda haja ndogo nilihisi kuchomwachomwa lakini kumbe mawe ndio yalikuwa yakitoka nikawa nahifadhi nilivyoona kuwa yametoka nikafurahi, nikwa naendelea vizuri sipati tena maumivu hadi leo.

“Nawashauri watu wengine waende hospitali kwani huduma zipo hapa Mloganzila, naendelea kunywa maji mengi madaktari wameaniambia yanasaidi tatizo lisijirudie, mwanzoni nilikuwa sipendi kunywa maji lakini sasa kwa siku natumia lita tatu,” anamaliza kusimulia Mwajuma.

HUDUMA MPYA KUOKOA WENGI

Juni mosi, Hospitali ya Mloganzila ilianza rasmi kutoa huduma ya matibabu ya kisasa ya kuvunja mawe kwenye figo na mfumo wa mkojo kwa njia ya mawimbi mshtuko ambapo hadi sasa wagonjwa 10 wamefanikiwa kupata huduma hiyo.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru, anasema waliamua kuagiza mashine ambayo itarahisisha kazi ya matibabu ya mawe ya figo ili kurahisha huduma hiyo kwa wagonjwa.

Profesa Museru anasema huduma hiyo itafanywa kwa kutumia mashine ambayo inatoa mawimbi sauti yanayosafiri kupitia ngozi hadi kwenye figo sehemu yenye jiwe.

“Mawimbi hayo hugeuka kuwa nishati yenye uwezo wa kuvunja mawe kuwa madogo mithili ya mchanga ambapo yakishasagwa yatatoka kwa njia ya haja ndogo.

“Tumeanza kutoa huduma ambayo ndani ya muda mfupi matibabu yanakuwa tayari wala haina maumivu tofauti na njia ya upasuaji mtu anaweza kuchukua miezi miwili mpaka mitatu ndo anapona hapa ni wiki moja tu tunamsubiri tumpime tena,” anabainisha

Profesa Museru. Anasema gharama za matibabu kwa mgonjwa mmoja ni Sh 500,000 hadi milioni 1.2 kulingana na kundi alilopo mgonjwa.

“Kwa raia wa kigeni gharama itakuwa Sh milioni 4.8 lakini kwa matibabu ya nje ya nchi serikali ikimpeleka mgonjwa mmoja anatumia Sh milioni 10 hivyo kufuatia matibabu ya watu 10 tuliowahudumia serikali imeokoa kiasi cha Sh milioni 95,” anaeleza.

Profesa Museru anasema faida ya matibabu hiyo ni kubwa kwani mgonjwa hutumia muda mfupi wa matibabu na gharama ni ndogo.

“Matibabu haya hayahitaji mgonjwa kulazwa hospitalini kwani anaweza kutibiwa na kuruhusiwa siku hiyo hiyo ili kuendelea na kazi zake na uwapo wa huduma hii unaondoa upasuaji mkubwa kwa wagonjwa,” anabainisha.

HALI ILIVYO MUHIMBILI

Takwimu za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika kipindi cha mwaka 2019 zinaonesha kuwa jumla ya wagonjwa wenye mawe ya figo 1,035 walionwa katika kliniki za wagonjwa wa nje (OPD).

Kati ya wagonjwa hao, wapya walikuwa ni 425 wakati wagonjwa waliolazwa kutokana na tatizo hilo walikuwa 144 na wastani wa wagonjwa wanne walifanyiwa upasuaji wa kuondoa mawe hayo kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2017 jumla wa wagonjwa 23 wenye matatizo ya mawe kwenye figo walipatiwa rufaa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi.

SABABU ZA MAWE KWENYE FIGO

Athari za mawe ya figo na njia ya mkojo hutokana na kuwapo kwa baadhi ya madini kwa wingi katika mkojo mfano madini aina ya calcium oxalate na citric acid.

Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa mfumo wa njia ya Mkojo, Dk. Jacob Jica, wakati mwingine mawe ya figo hutokana na kutengenezwa kwa kiwango kidogo cha mkojo katika figo hasa kwa wale ambao unywaji wao wa maji sio wa kutosha.

Anasema maambukizi ya bakteria katika mfumo wa mkojo yanaweza kusababisha kupata ugonjwa kwenye mfumo wa mkojo.

“Kwa kiasi kikubwa waathirika zaidi wa ugonjwa huo ni wanaume wenye umri wa miaka 20 na kwa wingi wenye umri wa kati ya miaka 40 hadi 70.

“Sababu zingine zinazobainishwa ni ulaji wa nyama nyekundu ambao huweza kusababisha mawe ya figo kutokana na wingi wa calcium oxalate huku watu wanaoishi katika mazingira ya joto wakiwa hatarini zaidi,” anafafanua Dk Jica.

DALILI ZA MAWE KWENYE FIGO

Daktari Bingwa wa Mfumo wa Njia ya Mkojo kutoka Hospitali ya Tifa ya Muhimbili, Dk. Hamisi Isaka, anasema dalili za mawe kwenye figo hutegemea sehemu jiwe lilipo na ukubwa wake.

“Dalili huwa ni tofauti, utakuta kuna mwingine atapata maumivu sehemu ambapo jiwe lipo, mwingine atakojoa damu hii inatokea kama jiwe ni kubwa.

“Dalili zingine mtu mwenye mawe ya figo anaweza kupata maumivu makali wakati wa kukojoa na mwingine anaweza kutokwa na usaha katika sehemu zake za siri kwahiyo hizo ndio dalili kubwa,” anabainisha Dk. Hamisi.

UNAVYOWEZA KUEPUKA

Dk. Hamisi anasema watu wanaokaa katika mazingira ya joto wako hatarini kupata tatizo la mawe kwenye figo hivyo, anawashauri kunywa maji mara kwa mara ili kuweza kuepuka tatizo hilo.

Pia anashauri ni vyema jamii kuepuka ulaji wa nyama nyekundu kwa wingi kwani zinaweza kusababisha tatizo hilo.

“Ukiwa unakunywa maji mara kwa mara utapata mkojo ambao utasaidia kusafisha figo na kuzuia uwezekano wa kupata tatizo hilo kwa asilimia kubwa,” anabainisha

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
157,873FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles