Ferdnanda Mbamila, Dar es Salaam
Watu zaidi ya 400 wanatarajia kuhudhuria katika sikukuu ya Makumbusho duniani(IMD),yatakayofanyika katika Kijiji cha Makumbusho , jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho ya sikukuu hiyo hufanyika Mei 18 kila mwaka, huadhimishwa kwa kaulimbiu tofauti ambapo kwa mwaka huu kaulimbiu inasema “makumbusho kitovu cha utamaduni”.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Mei 16, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabula amesema lengo la kuwa makumbusho duniani ni kuleta uelewa kwa umma kwamba makumbusho ni taasisi ambayo urithi wa utamaduni unahifadhiwa na utamaduni ni uhai wa nchi.
Amesema utamaduni ulio hai unabadilishana , unahuishwa na kurutubishwa na hivyo kuwa maelewano,ushirikiano na amani miongoni mwa wananchi.
“Kama taasisi za makumbusho zina nguvu na uwezo wa kuleta utengamano wa kiutamaduni na kisiasa na kujenga umoja wa kitaifa,uzalendo na kuwafanya watu wathamini na kuhifadhi urithi wa utamaduni na asili kwa kizazi hiki na kijacho,”amesema.
Amesema makumbusho zinaendelea kufanya kazi zake za misingi za utafiti, uhifadhi, kukusanya mikusanyiko na kuelimisha umma kwa njia ya maonesho, semina, machapisho na program za kielimu juu ya mambo yote yanayohusu urithi wa asili na kiutamaduni kwa lengo la kutoa elimu, kujifunza na kuburudisha.
Amesema kwa sasa makumbusho duniani kote zina jukumu kubwa la kuihudumia jamii kuifanya kuufikia urithi wao wa utamaduni na asili.
Profesa Mabula amesema pia katika kuadhimisha siku hiyo makumbusho ya taifa imeandaa tamasha la mama na mwana ambalo litahusisha wazazi na watoto wao kutembelea makumbusho na kujifunza juu ya urithi wao.
“Tamasha la Mama na Mwana litajumuisha mambo yafuatayo, maandamano yatakayoanzia eneo la bamaga au kwenda kijiji cha makumbusho na maeneo mengine.
“Watoto na wazazi wao kucheza michezo mbali mbali ya asili, kujifunza kupika vyakula vya asili, kuruka kamba ,mdako, kombolela, kidalipo, , kuchora na michezo mingine mingi,”amesema Profesa Mabula.