KABUL, AFGHANISTAN
WATU 63 wameuawa na wengine zaidi ya 180 kujeruhiwa baada ya bomu kulipuka katika ukumbi wa harusi katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.
Walioshuhudia waliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kwamba mlipuaji wa kujitolea muhanga alijilipua wakati wa sherehe hiyo ya harusi.
Mlipuko huo ulitokea saa nne na dakika 40 kwa saa za Afghanistan katika eneo lililopo magharibi mwa mji ulio na raia wengi Waislamu wa dhehebu la Shia.
Kundi la Taliban limekana kuhusika na shambulio hilo na hakuna kundi jingine lililokiri kutekeleza shambulio hilo.
Wapiganaji wa Kiislamu kutoka Dhehebu la Sunni, ikiwemo Taliban na kundi la wapiganaji wanaojiita Dola la Kiislamu (IS) mara kwa mara wamekuwa wakiwalenga Waislamu wa Hazara wa dhehebu la Shia walio wachache nchini Afghanistan na Pakistan.
Waziri wa maswala ya ndani nchini Afghanistan, amethibitisha vifo hivyo saa chache baada ya bomu hilo kulipuka.
Picha zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii zilionyesha miili ikiwa imetapakaa huku viti na meza vikiwa vimependukia.
Harusi za Afghanistan huruhusu mamia ya wageni katika kumbi kubwa ambapo wanaume hutengwa na wanawake na watoto.
Mgeni mmoja kwa jina Mohammad Farhag, alisema kuwa alikuwa katika eneo la wanawake wakati aliposikia mlipuko mkubwa eneo la wanaume.
“Kila mtu alikimbia nje akipiga kelele na kulia. Kwa takriban dakika 20 ukumbi huo ulikuwa umejaa moshi.
“Karibu kila mtu katika eneo la wanaume ni aidha amekufa au kujeruhiwa. Sasa saa mbili baada ya mlipuko, wanaendelea kutoa miili ndani ya ukumbi huo,” Farhag aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP).
Muhudumu mmoja wa chakula, Sayed Agha Shah, alisema kila mtu alikuwa akikimbia baada ya mlipuko huo.
“Wahudumu wetu kadhaa walifariki ama kujeruhiwa,” alisema.
Msemaji wa Taliban, Zabiullah Mujaheed alisema kuwa wanalaani shambulio hilo.
“Hakuna haki ya shambulio la kusudi kama hilo na mauaji ya kiholela yaliyowalenga wanawake na watoto,” alisema Mujaheed katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Mlipuko huo unajiri siku 10 baada ya bomu kubwa kulipuka nje ya kituo cha polisi cha Kabul na kuwaua watu 14 huku 150 wakijeruhiwa.
Kundi la Taliban lilisema kuwa lilitekeleza shambulio hilo.
Ijumaa iliyopita, ndugu mmoja wa kiongozi wa Taliban, Hibatullah Akhundzada, aliuawa kutokana na bomu lililotegwa ndani ya msikiti karibu na mji wa Quetta nchini Pakistan.
Hakuna kundi lolote kufikia sasa lililokiri kutekeleza shambulio hilo.