27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Watoto wenye ulemavu wasaidiwa viti mwendo, bima ya afya

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Shirika lisilo la kiserikali linalohudumia yatima, wajane, wenye ulemavu na wazee (Diana Women Empowerment) limetoa msaada wa viti mwendo na kadi za bima ya afya kwa watoto wenye ulemavu na wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Viti mwendo sita na kadi za bima ya afya 73 zimekabidhiwa kwa watoto wenye ulemavu wanaosoma Shule za Msingi Ukombozi na Majimatitu kitengo cha wenye ulemavu huku tano zikitolewa kwa watoto wanaolelewa majumbani na 20 kwa watoto yatima.

Mwenyekiti wa Shirika la Diana Women Empowerment, Farida Khakoo (Wanne kushoto), akimpongeza Mjumbe wa Bodi ya shirika hilo, Salma Salmin baada ya kukabidhi viti mwendo na kadi za bima ya afya kwa watoto wenye ulemavu. (Watatu Kushoto) ni Mjumbe wa Bodi, Sophia Kinega.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Mjumbe wa Bodi ya shirika hilo, Salma Salmin, amesema watoto wengi wenye ulemavu wanaishi kwenye mazingira magumu na kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia.

“Tunajitahidi kutoa misaada mbalimbali kwa kushirikiana na wafadhili na watu wengine wenye mapenzi mema, lakini uhitaji ni mkubwa hivyo, tunawaomba Watanzana na wadau wengine wajitokeze kuwasaidia watoto wenye ulemavu,” amesema Salma.

Naye Mwenyekiti wa shirika hilo, Farida Khakoo, amewaomba wadau kuwasaidia gari la shule kwa ajili ya kuwachukua na kuwarudisha nyumbani watoto wenye ulemavu wa viungo hasa wanaosoma Shule ya Msingi Ukombozi.

“Tunapata shida kuwahudumia watoto, wengine wanahitaji pampasi tunashindwa kuwanunulia, hatuna uwezo wa kuwafikia wote.

“Wazazi wengine hawana uwezo wa kumudu kununua viti mwendo, wanaumia kwa kuwabeba watoto mgongoni. Asubuhi ampeleke shule halafu mchana amfuate na wengine ni wakubwa…likipatikana gari litasaidia kwa kiasi kikubwa kuwatoa majumbani na kuwarudisha baada ya masomo,” amesema Farida.

Amesema shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1995 linahudumia yatima, wajane, wenye ulemavu na wazee katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Tanga kwa kuwapatia elimu, bima za afya, chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu.

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya shirika hilo, Sophia Kinega, ameitaka jamii kuacha kuwaficha watoto wenye ulemavu kwani wana haki sawa kama wengine.

Mmoja wa wazazi mwenye mtoto aliyepatiwa kiti mwendo, Dalizeni Mapondela, ameshukuru kwa msaada huo na kwamba mwanawe atakuwa na uhakika wa kwenda shule bila kikwazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles