23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

WATOTO WENYE ULEMAVU MTWARA WANASOMA MZUNGU WA NNE

Ofisa Elimu Maalumu Manispaa ya Mtwara Mikindani, Ally Ndale (kulia) akisaidiana na Ofisa Tarafa Wilaya ya Mtwara, Octavian Lipimbile (kushoto) kufunga kifaa cha kumwezesha kusikia mwanafunzi wa Shule ya Msingi Rahaleo baada ya kuletewa kifaa hicho na shirika la Woman for Vision.
Ofisa Elimu Maalumu Manispaa ya Mtwara Mikindani, Ally Ndale (kulia) akisaidiana na Ofisa Tarafa Wilaya ya Mtwara, Octavian Lipimbile (kushoto) kufunga kifaa cha kumwezesha
kusikia mwanafunzi wa Shule ya Msingi Rahaleo baada ya kuletewa kifaa hicho na shirika la Woman for Vision.

Na FLORENCE SANAWA-MTWARA

KUKOSEKANA kwa huduma stahiki ya elimu kwa watoto wenye ulemavu mkoani Mtwara kumeathiri upatikanaji wa elimu bora kwao baada ya kukumbana na miundombinu isiyo rafiki.

Hali hiyo inasababisha kuwepo kwa watoto wachache shuleni na kuchangia uduni wa maisha ya wakazi wa mkoa huo huku wazazi wa watoto hao wakishindwa kuwapeleka shuleni kutokana na kipato kidogo wanachopata.

Hivyo kufanya idadi ya watoto wenye ulemavu shuleni kuwa ndogo huku wasiosoma kuwa kubwa zaidi.

Upatikanaji wa elimu bora kwa watu wenye ulemavu imekuwa changamoto kubwa kwa Mkoa wa Mtwara hasa katika shule mbili za msingi zinazotoa elimu maalumu kwa watoto wenye ulemavu.

Shule ya Msingi Rahaleo ikiwa na watoto wenye ulemavu wa kusikia huku Shule ya Msigi Shangani ikiwa na watoto wenye ulemavu wa akili, zote zikiwa na kilio kimoja cha kupata madarasa na mabweni ili watoto hao waishi shuleni.

Hali ya upungufu wa madarasa umepunguza darasa moja na walimu wao huku wakati wa vipindi wakishindwa kusikilizana vizuri kutokana na madarasa matatu kuendeshwa kwa wakati mmoja ndani ya darasa moja.

Manispaa ya Mtwara Mikindani inakadiriwa kuwa na jumla ya wanafunzi 114 wenye mahitaji maalumu huku ikiwa na shule mbili tu za msingi ambazo hazikidhi mahitaji ya watoto hao.

Kitengo hicho cha watoto wenye ulemavu wa masikio kilichoanzishwa mwaka 2004 kimekuwa kikipata wakati mgumu hasa wakati wa masomo kutokana na walimu watatu kufundisha kwa wakati mmoja wakiwa wamepeana migongo.

Mkuu wa Kitengo hicho, Mwalimu Caroline Chitumbi, anazungumizia changamoto ya usikivu kwa wanafunzi hao.

Anasema kuwa wanafunzi wengi wanatoka katika familia zisizo na uwezo hivyo kuwalazimu walimu kuwahangaikia ili waweze kupata vifaa stahiki sambamba na madarasa ya watoto hao.

“Hawa watoto wanatoka katika mazingira magumu sana wanapokuwa hapa shuleni tunajaribu kuwaweka karibu na sisi ili waweze kujisikia wako huru, ndio maana tunahakikisha wanapata chai na chakula cha mchana japo tunayo changamoto kubwa ya vifaa vya ufundishaji.

“Unajua ulemavu wa kusikia una changamoto kubwa sana ambayo ikipatiwa ufumbuzi kwa kupewa kipaumbele tunaweza kufika mbali, wapo wanafunzi waliomaliza kitengo hiki leo hii wako shule za sekondari na wengine wanasomea ufundi. Serikali ilichukulie hili kwa uzito wa aina yake,” anasema Chitumbi.

Anasema wana upungufu wa madarasa tisa huku wakiwa na darasa moja wakilitumia pamoja na walimu wao.

Chitumbi anasema kuwa changamoto hizo zimekuwa kikwazo kwao huku wakiwa na mahitaji makubwa ya madarasa, chumba maalumu kwa ajili ya kupima usikivu wa wanafunzi hao, bwalo la chakula, ofisi ya walimu na stoo kwa ajili ya kuhifadhia vifaa vyao.

Mwalimu mwingine katika kitengo hicho, Deodata Mnunduma, anasema kuwa ufundishwaji watoto hao ni mgumu kutokana na kukosa vifaa, mitaala na madarasa.

“Hali hii inasababisha kushindwa kuelewana darasani hasa wakati wa kuanza vipindi ambapo walimu watatu hufundisha kwa wakati mmoja,” anasema Mwalimu Mnunduma.

Anaishauri wizara ya elimu iangalie uwezekano wa kusaidia vitengo maalumu na kuviboresha ili kuweza kupata wanafunzi wengi ikiwemo kuwajengea shule na mabweni na kuwawekea vifaa stahiki.

“Hawa watoto wanatakiwa kukaa katika mazingira mazuri ili waweze kupenda shule ikiwemo kupata chakula, vitabu na mambo mengine ya msingi,” anasema.

OFISA ELIMU

Ofisa Elimu Maalumu Viziwi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Ally Ndale, anasema Manispaa hiyo ina wanafunzi 114 wenye mahitaji maalumu hivyo kuwa na hitaji kubwa la shule kutokana uhaba mkubwa wa majengo uliopo.

Ndale anakiri kuwepo kwa changamoto hiyo ya upungufu wa madarasa na kwamba bado hayakidhi mahitaji kulingana na idadi ya wanafunzi iliyopo kwa sasa.

“Licha ya kukabiliana na changamoto nyingi katika elimu maalumu ila kwa sasa tunaishukuru serikali imeweza kutoa bajeti ya chakula kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, wanapata chakula cha asubuhi na mchana lakini bajeti hii iliyopo bado haikidhi mahitaji kwa wanafunzi,” anasema Ndale.

Anasema kuwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu wana uhitaji mkubwa na kwamba jitihada zinaendelea kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa ili kuwaruhusu wengi zaidi kufika shuleni na kuweza kujifunza.

Anaishauri jamii iachane na mila potofu zinazochangia kuwafungia ndani watoto wenye ulemavu au kuwaacha majumbani.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Mtwara Mikindani, Florah Kafiriti, anasema halmashauri inatambua shida hiyo ndio maana wanashirikiana na wadau mbalimbali ili kuweza kuzipunguza changamoto zilizopo.

“Tumeona wapo wengine ambao ni walemavu wamesoma na wana elimu nzuri, hivyo ongezeni bidii kuwafundisha ili waweze kutimiza ndoto zao,” anasema Kafiriti.

MSAADA

Kwa kutambua hitaji la watoto wenye ulemavu wa usikivu (Viziwi), Taasisi ya Women of Vision ilitoa vifaa vya kuwasaidia kusikia watoto 17 vyenye thamani ya Sh milioni 4.4 ili kuwawezesha watoto hao kuweza kupata usikivu mzuri hasa wakati wa masomo.

Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Adelina Karumuna, anasema msaada wa vifaa hivyo kwa kitengo hicho umekuja baada ya kuona uhitaji wake ni mkubwa na wa haraka ili kuweza kuwasaidia wanafunzi hao.

“Sisi ni wanawake tunambua umuhimu wa elimu kwa watoto wetu hasa wenye ulemavu, ndio maana tunajitahidi kupitia michango yetu ya kikundi ili kuweza kushikiriana  na jamii zenye mahitaji maalumu.

“Tunatambua kuwa kuna watoto wengi wenye uhitaji wa haraka lakini kutokana na uwezo mdogo na changamoto ni nyingi sisi tukaona tuanze na hawa wachache na tutaendelea kusaidia kadiri tuwezavyo,” anasema Karumuna.

Mwalimu Chitumbi anasema msaada huo utaongeza umakini kwa wanafunzi hao ambao awali walikuwa wakifundishwa kwa nadharia zaidi.

Anasema licha ya kupokea vifaa hivyo bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utelekezaji wa majukumu yao ya ufundishaji watoto hao.

HALI ILIVYO

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Hakielimu mwaka 2008 kuhusu hali ya upatikanaji wa elimu kwa watoto wenye ulemavu Tanzania, imechambua changamoto na fursa za kielimu zilizopo kwa watoto wenye ulemavu.

Utafiti huo ulitathmini kwa kina vikwazo vya kielimu ambavyo watoto wenye ulemavu katika shule za Tanzania wanakumbana navyo.

Kuna vikwazo vitano ambavyo vimeainishwa ikiwemo mpango mbovu katika ujenzi wa majengo ya shule, ambayo hayawapi fursa watoto wenye ulemavu kuweza kuyatumia hasa wale wenye ulemavu wa macho na viungo.

Uelewa mdogo na kutothamini mambo yanayowahusu watu wenye ulemavu miongoni mwa walimu, viongozi wa shule na jamii kwa ujumla. Mambo yote haya yana madhara pindi linapokuja suala la kutambua na kuthamini mahitaji ya kielimu kwa watoto wenye ulemavu.

Wazazi wengi hawako tayari kuwaandikisha watoto wenye ulemavu katika shule. Hii ni kutokana na mila na desturi ambazo zinawabagua watoto wenye ulemavu. Matokeo yake kiwango cha uandikishaji katika shule kwa watoto wenye ulemavu kimebakia kuwa cha chini.

Kutokana na ukosefu wa mafunzo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu na elimu jumuishi, walimu wengi hawako tayari kufundisha darasa lenye watoto wenye ulemavu na wasio na ulemavu. Hali hii imechangiwa na kutotekelezwa kwa vitendo sera ya serikali inayohusu elimu jumuishi, ambayo ingetoa fursa zaidi za kielimu kwa watoto wenye ulemavu.

Shule nyingi hazina sifa za kufundisha watoto wenye ulemavu kutokana na ukosefu wa vifaa muhimu na matini yanayofaa kufanikisha tendo la ujifunzaji kwa watoto wenye ulemavu.

Pengine kikwazo zaidi cha kielimu kwa watoto wenye ulemavu ambacho kinaweza kujumuisha vikwazo vyote ni kwamba hakuna juhudi za makusudi zilizochukuliwa kuondoa vikwazo hivi.

Kwa hiyo, kuna haja kwa wadau wote wa elimu pamoja na wapenda elimu na maendeleo hapa nchini kuzindua kampeni zitakazolenga kuwainua katika elimu watu waliotengwa, hasa watoto wenye ulemavu. Kushindwa kutoa fursa za kielimu kwa watoto wenye ulemavu ni kudidimiza, malengo, mafanikio na matarajio ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu (MMEM) ambao unasisitiza elimu kwa wote.

Kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni mwanachama wa jumuiya nyingi za kimataifa ambazo zinatambua na kuhimiza falsafa ya elimu kwa wote, likiwemo Tamko la Salamanka na namna ya kulitekeleza (UNESCO, 1994), kuna haja ya kuondoa vikwazo vinavyozuia upatikanaji wa elimu kwa watoto wenye ulemavu.

Ripoti imependekeza hatua nyingi za kisera ili kuondoa vikwazo vya elimu kwa watoto wenye ulemavu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles