27.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

‘Watoto wa kifisadi’ wanapojaribu kuiteka Afrika

JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM

‘INASHANGAZA lakini ni kweli, ukweli mara nyingi hushangaza; unashangaza kuliko hata simulizi ya kubuni’, aliandika mwanazuoni na mshairi wa karne ya 18 wa Kiingereza, Lord Byron katika shairi lake, Don Juan.

Don Juan, katika muktadha huo ni mwanaume anayemrithi mwanamke mrembo ikiwamo kulala naye bila kujali mwonekano mbaya wa sura na umbo wa mwanaume huyo.

Na ndiyo maana si ajabu au haishangazi lakini ni kweli kuwa kuna watoto wa marais wa zamani Afrika walio madarakani au  walioyakamilisha.

Lakini pia kuna watoto wa marais walio madarakani wanaopasha misuli ili kuwarithi baba zao; bila kujali iwapo wana sifa au ni kinyume na matakwa ya raia wao.

Vitendo hivi vya marais wengi wa Afrika kutawala kana kwamba ni wa ukoo wa kifalme, iwe urais wa maisha na kurithisha watoto au ndugu zao madaraka ni vya kawaida kabisa.

Katika hali ya kawaida, marais hawa walipaswa kukabidhi madaraka kwa chaguzi zinazokubalika kidemokrasia, lakini kilichopo miongoni mwao ni demokrasia ya kiini macho.

Watawala hawa hufanya kila linalowezekana kufia madarakani au kukabidhi madaraka kwa ndugu zao kutokana na sababu kuu mbili;

Kwanza kunogewa madaraka na kujiona ni wao tu wanaostahili hadhi hiyo na au hofu ya uwezekano wa kushtakiwa watakapoondoka na madaraka kuangukiwa mikononi mwa wasio damu yao.

Mbali ya sababu hizo mbili, hutokana na shinikizo kutoka kwa watu wao wa karibu, ambao wananufaika na tawala hizo na hivyo kuhofia ondoko lao hilo litakuwa mwisho wa ‘kula kula’ yao hiyo ya kifisadi.

Kutokana na sababu hizo kuna wimbi la kurithisha watoto hata wake madaraka katika bara hili na wakati huo huo kuwajengea utajiri mkubwa hata kama bado wangali wadogo ama shuleni.

Wengine hupewa nyadhifa kubwa serikalini au mashirika ya umma bila kujali uwezo wao. Hakika matanuzi yao yanatisha ilhali wananchi wao wengi wametopea katika umaskini.

Hata hivyo, si watoto wote wa marais au wake zao walioingia madarakani kwa malengo hayo ya kifisadi, wapo waliotokana na juhudi zao au kuangukiwa ngekewa kutokana na historia ya baba zao huko nyuma.

Katika kundi hili lina watoto wa kiume kwa kike hadi waume na wake, ambao wanaweza kushuhudiwa katika karibu mabara yote ya sayari hii kuanzia Asia, Ulaya, Amerika ya Kusini na Kaskazini ikiwamo Marekani.

Katika mabara hayo unaweza kuziona familia za Bhutto, Bush, Indira na nyinginezo, ambazo baada ya baba, mwana, binti au mke walikuja kuongoza kutokana na ngekewa au huruma iliyotokana na kifo au kuuawa kwa wapendwa wao (rais), ama juhudi binafsi tu.

Kwa muktadha huo, hata Afrika wapo waliopitia njia kama hizo, ambazo huwezi kuzikosoa sana kwa vile kila mtu ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa kuongoza taifa lake.

Afrika watawala wa kundi hili ni pamoja na Luteni Jenerali Ian Khama, ambaye ameondoka madarakani hivi karibuni tu.

Mtoto huyo mkubwa wa baba na mwasisi wa taifa hilo tajiri kwa almasi Marehemu, Sir Seretse Khama, aliingia madarakani  April 1, 2008.

Sir Seretse Khama alikuwa Rais wa kwanza wa nchi, ambaye aliongoza harakati za kudai uhuru kutoka utawala wa Kiingereza na kuupata Septemba 30, 1966.

Ikijivunia demokrasia na utulivu wa kisiasa na kiuchumi, tangu uhuru Botswana imeongozwa na marais watano tu, Sir Seretse Khama, Sir Ketumile Masire, Festus Mogae na Luteni Jenerali Ian Khama.

Khama akagoma mtego wa muhula wa tatu akajiuzulu rasmi mapema mwaka huu na nafasi yake kujazwa na Mokgweetsi Masisi.

Nchini Kenya, Rais Uhuru Mugai Kenyatta, aliingia Ikulu kwa kushawishiwa na Rais wa pili wa Kenya huru, Daniel Arap Moi katika kinachoonekana kulipa fadhila kwa baba wa Uhuru, Mwasisi wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta.

Kwa watawala wa aina hiyo si ajabu duniani, kinachogomba tu ni zile taratibu mbaya za umimi au kurithisha madaraka kwa mwanafamilia mithili ya ukoo wa kifalme.

Katika kundi hili la pili la kurithisha madaraka, kuna ambao walijaribu kufanya hivyo, wasifanikiwe baada ya kung’olewa au kuuawa kabla ya kutimiza ndoto zao hizo.

Miongoni mwao ni Kanali Muammar Gddafi mwaka 1969 akiwa na miaka 27 alimwangusha Mfalme Idris 1, akaenda kuidhibiti nchi kwa zaidi ya miaka 40.

Mtoto wake, Sayf al-Islam Gaddafi alikuwa mwenye nguvu na ushawishi baada ya baba yake akiandaliwa kumrithi.

Hata hivyo, hilo halikufanikiwa licha ya maendeleo na ustawi wa kiuchumi na kijamii, aling’olewa na waasi mwanzoni mwa mwongo huu kwa msaada wa majeshi ya Magharibi.

Libya ikiwa ukanda wa Kaskazini mwa Afrika, taifa lingine la eneo hilo lililopanga kukabidhi madaraka kutoka baba kwenda mwana ni Misri.

Wamisri kamwe hawakuwahi kuhamisha madaraka ya urais kidemokrasia. Wakati wa Rais mkongwe, Hosni Mubarak akiwa amelitawala miaka 30, Wamisri wengi walikuwa wameikabidhi nchi kwa familia yake, chama tawala, maofisa wa kijeshi na wa usalama jukumu la kuamua mrithi wake, ambaye hakuwa mwingine zaidi ya mwanae, Gamal Mubarak.

Nchini Misri hawakumchagua Anwar Sadat kuwa rais wala Mubarak na hawakutarajia kumchagua mrithi wake. Aliyemrithi Mubarak baada ya waandamanaji kumng’oa, Mohammed Morsi 2011 aliweza kuwa chaguo la wananchi kidemokrasia.

Hata hivyo, Morsi hakuwa chaguo la jeshi bali wananchi, hivyo basi haikuwa ajabu kutodumu kwani aling’olewa na Mkuu wa Majeshi, Abdel Fattah el-Sisi ambaye ndiye rais hadi sasa.

Kwa maana hiyo, Jeshi la Misri limewachagulia Wamisri viongozi tangu Gamal Abdel Nasser, Sadat Anwar, Hosni Mubarak na sasa el-Sisi, wote wakitokea jeshini.

Mwingine aliyeshindwa njama kama hizo ni Rais mkongwe Robert Mugabe, ambaye alipanga kumrithisha taifa lake hilo, mkewe Grace, kitendo kilichomgharimu kwani aling’olewa kwa aibu Novemba mwaka jana.

Waliofanikiwa katika mikakati hiyo haramu ni pamoja na Meja Jenerali wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila. Ilikuwa Januari 16, 2001 wakati baba yake, Laurent Desire Kabila, alipouawa na mlinzi wake.

Uongozi wa kijeshi katika kulinda maslahi yake, ukadai kuwa ni busara kumweka mwanae huyo katika kiti cha urais kilichoachwa na baba yake katika taifa, ambalo hadi sasa limeathirika kwa vita, umaskini licha ya uwapo wa rasilimali kedekede.

Akiwa na umri wa miaka 29 tu, Jenerali Joseph Kabila aliapishwa kuwa Rais na kamanda wa majeshi Januari 26, 2001 akiwa Rais mdogo  zaidi kiumri duniani.

Hata hivyo, anatarajia kuondoka madarakani shingo upande mwishoni mwa mwaka huu baada ya jaribio lake la kung’ang’ania madaraka kushindikana.

Kwa vile Kabila hana mtoto mkubwa wa kutosha kumrithisha madaraka huku akichukiwa na wanandugu wake wengine hasa waliotokana na wake wengine wa marehemu baba yake, Kabila akaona dawa ya kujilinda na uwezekano wa kushtakiwa au kunyang’anywa utajiri wake na familia yake uliopatikana kifisadi ni kung’ang’ania madaraka.

Lakini baada ya kuweza kubaki kwa miaka miwili tangu kumalizika muda wake wa urais mwaka 2016, maji yakamfikia shingoni. Waandamanaji wakiongozwa na Kanisa la Katoliki walimtikisa vibaya na hivyo kumteua msiri na rafiki wake mtiifu asiyejulikana sana kisiasa Emmanuel Ramazani Shadary kumrithi.

Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Ndani amewahi kuwekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya kwa tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu na ufisadi.

Ripoti zinasema Shadary yupo maalumu kulinda madaraka ya Kabila kwa mlango wa nyuma, wakati akijipanga kurudi madarakani katika uchaguzi ujao kwa vile Katiba inaruhusu.

Ili kufanikisha ushindi wa Shadary wake, wagombea urais wa upinzani wenye nguvu wameondoshwa na kubakia wale dhaifu au wanaoiunga mkono Serikali.

Mlolongo wa magari ya kifahari, chupa za shampeni za bei mbaya, jumba la kirais lenye thamani ya dola milioni 500, viatu maarufu vya kumfanya rais aonekane mrefu na makumi ya majumba mjini Paris pekee vinamzungumzia Omar Bongo Ondimba.

Rais huyo wa zamani wa Gabon  hakutawala tu taifa hili tajiri kwa mafuta la kati mwa Afrika kwa mkono wa chuma tu kwa zaidi ya miongo minne. Bali aliifanya kazi hiyo kwa staili.

Wakati alipofariki ghafla kwa shambulio la moyo mwaka 2009 akiwa na umri wa miaka 73, aliacha mjane, watalaka wawili akiwamo aliyeondokea kuja kuwa mwanamuziki maarufu wa pop baada ya talaka, watoto zaidi ya 50 na raia milioni 1.5 katika taifa ambalo wafuasi wake wanadai alilitoa shimoni.

Omar Bongo alichukua urais wa Gabon mwaka 1967, miaka saba baada ya taifa hilo kujikomboa kutoka ukoloni wa Ufaransa. Haikushangaza sana mmoja wa wanae 50, Ali, Bongo akachukua kiti hicho miezi mitatu baada ya kifo cha babaye huyo.

Laini bado Ali Bongo Ondimba anakana kuwa kivuli cha baba yake kilimsaidia kuingia madarakani.

Anadai baba yake aliapa kuwa atarithisha nyumba yake lakini si kiti cha urais na kwamba kivuli cha baba yake kilikuwa mzigo kuliko faida wakati wa kampeni yake ya urais mwaka 2009.

Kwa kweli inashangaza lakini ni kweli, Faure Gnassingbe ni Rais wa Jamhuri ya Togo. Faure amekuwa mrithi wa baba yake aliyefariki madarakani Februari 5, 2005, akiwa amelitawala taifa hilo kwa msaada kamilifu wa jeshi tangu mwaka 1967.

Faure alianza kuunda Serikali ya Mpito. Huku wafuasi wengi wa upinzani wakiona utawala wake ni wa kurefusha ule wa baba yake – Gnassingbe Eyadema – karibu miongo minne ya kulitawala.

Faure alishinda uchaguzi kitatanishi April 24, 2005 huku waangalizi wa kimataifa wakiuponda kuwa haukuwa uchaguzi na ulishuhudia mandamano ya kuupinga wakisema wizi wa kura ulifanyika waziwazi.

Matokeo ya mwisho yalimpa Faure zaidi ya asilimia 60 ya kura dhidi ya asilimia 38 ya mpinzani wake Emmanuel Akitani-Bob.

Faure Essozimna Gnassingbé Eyadéma aliyezaliwa Juni 6, 1966 kabla ya urais aliteuliwa na baba yake kuwa Waziri wa Mazingira, Madini, Posta na Mawasiliano mwaka 2003 hadi 2005.

Kufuatia kifo cha Eyadéma mwaka 2005, Gnassingbé mara moja akawekwa na jeshi madarakani. Utata wa uhalali huo kikatiba wa urithi ukasababisha shinikizo kubwa lililomfanya Gnassingbé ajiuzulu Februari 25. Ilikuaje?

Faure aliandaliwa mapema kumrithi baba yake ndiyo maana mabadiliko ya Katiba yaliyofanyika Desemba yalipunguza umri wa kuwa rais kutoka miaka 45 hadi 35 yakimlenga kijana Gnassingbé.

Uteuzi wake kuingia serikalini kama waziri Julai 2003 ulionekana wazi na tayari kabla alikuwa akionekana sambamba na baba yake katika shughuli rasmi za kiserikali na kuibua minong’ono. Kweli wenye shaka hawakukosea!.

Kwa mujibu wa Katiba ya Togo, baada ya kifo cha Rais Februari 5, 2005, Rais wa Bunge la Taifa alipaswa kuwa Kaimu Rais. Wakati wa kifo cha Eyadéma, Rais wa Bunge la Taifa Fambaré Ouattara Natchaba alikuwa nje ya nchi na hivyo Gnassingbé akaapishwa kuwa Kaimu Rais kwa kilichodaiwa ‘kuhakikisha kuna utulivu.’

Wengi wanaamini Natchaba hakutaka kurudi Togo kwa hofu ya kuuawa na ukoo wa Gnassingbé maana Jeshi lilikuwa likimlazimisha ajiuzulu wadhifa wake bungeni ili kutoa fursa ya Gnassingbé kuwa Rais bila kikwazo cha sheria.

Kufuatia maandamano akajiuzulu na kwenda kushinda uchaguzi wenye utata wa Aprili 24, 2005 na kuapishwa lakini pia akashinda tena uchaguzi wa 2010 na 2015, ambao ulishuhudia maandamano makubwa kumtaka ang’oke.

Ni kiasi kuwa Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo amemtaka ajiuzulu maana haoneshi kuwa na kipya cha kuifanyia nchi yake hiyo mambo makubwa kimaendeleo.

Ukanda wa Afrika Mashariki, Rais wa Uganda, Jenerali  Yoweri Museveni Julai 2005 aliibaka Katiba, kufuta na kuondoa kipengele cha Katiba kinachoweka ukomo wa mihula miwili ya Rais kilichomfanya awe madarakani hadi leo hii.

Marekebisho ya Katiba yalimshuhudia akiwania urais Februari 2006, Februari 2011 na majuzi Februari 2016.

Lakini kilichokuja shtuka ni kupanda ngazi haraka kwa mwanae mkubwa mzaliwa wa Dar es Salaam, Meja Jenerali Muhoozi Kainerugaba (44). Meja Muhoozi alikuwa kamanda wa kikosi cha ulinzi wa Rais. Alijitosa jeshini mwaka 2001 baada ya kupitia kozi katika Chuo cha Kijeshi cha Sandhurst, Uingereza na kupanda ngazi ya umeja aliyotunukiwa na Kiongozi wa Libya. Marehemu Kanali  Muammar Gaddafi. Katika tukio hilo la Januari 2001, Gaddafi aliungana na rafiki yake Jenerali Museveni kuadhimisha miaka 15 ya Museveni kuitwaa Uganda kijeshi Januari 26, 1986.

Katika tukio hilo, Kanali Gaddafi alimshauri Museveni kuwa wanamapinduzi akiwamo yeye na Museveni hawakabidhi madaraka kwa hiyari.”

Kufuatia  kuhitimu kwake na kupanda ngazi haraka haraka,  Muhoozi akateuliwa kusimamia majeshi maalumu yanayohusika na ulinzi wa maeneo yenye utajiri wa mafuta na kisha akaja kuwa mshauri wa kijeshi wa rais.

Museveni (74) pia amempa Mkewe Jeneth wizara tangu Mei 2011 na sasa anaongoza Wizara ya Elimu na Michezo,

Nchini Guinea ya Ikweta, Teodoro Nguema Obing Mangue (49) ni Makamu wa Pili wa Rais wa Guinea ya Ikweta, akiwa mtoto wa Rais Teodoro Obiang Nguema Mbaogo aliye madarakani tangu mwaka 1979 baada ya kumpindua mjomba wake.

Utajiri unaelezwa kufikia zaidi ya dola milioni 105 ambazo ni sawa na zaidi Sh. bilioni 220.

Licha ya kuandaliwa kumrithi baba yake, amekuwa akifuatiliwa na Serikali za Ufaransa, Marekani na Uswisi sambamba na familia za marais wa Gabon na Togo kwa ufisadi.

Nchini Ufaransa anashutumiwa kununua makumi ya magari ya kifahari yenye thamani ya Sh. bilioni 300 za Kitanzania huku akitetekeza Sh. bilioni 50 kwenye anasa mbalimbani na vimwana wakiwamo wasanii na wanamuziki nyota.

Licha ya uchafu wake wote huo, huyo ndiye rais ajaye wa Guinea ya Ikweta

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles