Chaguzi za Ukonga na Monduli, uhalali finyu wa uwakilishi

0
1159
Mtu akipiga kura

Na ANDREW MSECHU

Agosti 15, mwaka huu gazeti hili lilieleza kwa kina namna chaguzi za marudio zinavyoshusha morali ya wapiga kura.

Makala hiyo ilionesha namna ambavyo hatua ya kujiuzulu kwa wabunge na madiwani kisha chaguzi kurudiwa na kuwarudisha wale wale waliojiuzulu kuwa wagombea kutoka chama A kwenda chama B.

Matokeo ya uchaguzi wa marudio uliofanyika Septemba 16, mwaka huu katika majimbo ya Ukonga jijini Dar es Salaam na Monduli jijini Arusha yanaonesha kushuka kwa mwitikio wa wapiga kura kwa kiasi kikubwa, ikilinganishwa na ule Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Hili linadhihirishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji (mstaafu ) Aristocles Kaijage ambaye akiwa katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Juhudi alisema ameshuhudia mwenyewe kuwa mwitikio wa wapiga kura umekuwa mdogo.

Jaji Kaijage alisema hata katika maeneo mengine yaliyokuwa yakishiriki uchaguzi huo wa Jumapili, kwa mujibu wa taarifa alizokuwa akiendelea kupata, mwitikio wa wapiga kura haukuwa mzuri na walijitokeza wapiga kura wachache tofauti na matarajio.

“Kwa ujumla katika uchaguzi wa majimbo hayo mawili na kata tisa uchaguzi umefanyika japokuwa inaonekana mwitikio wa wapiga kura si mzuri katika baadhi ya vituo tulivyotembelea,” alisema.

Uwiano wa matokeo ya Monduli

Katika Jimbo la Monduli mkoani Arusha, Julius Kalanga ambaye alikuwa akiwania nafasi hiyo kupitia CCM baada ya kujiuzulu kutoka Chadema, alitangazwa mshindi kwa kupata kura 65,714 sawa na asilimia 95 ya kura zote, ikiwa ni idadi kubwa zaidi hata kushinda kura alizopata mwaka 2015 alipogombea kwa tiketi ya Chadema.

Katika uchaguzi wa 2015, Kalanga alishinda kwa kura 35,024 akifuatiwa na mgombea wa CCM aliyepata kura 25,925 na mgombea wa ACT-Wazalendo aliyepata kura 367, hivyo kufanya majumuisho ya kura zote kufikia 61,316 hivyo kuwa na ongezeko la zaidi ya kura 4,398 kati ya kura zote zilizopigwa mwaka 2015.

Hii inamaanisha kuwa Kalanga alipata kura zaidi ya zote zilizokuwa zimepigwa na wapiga kura wote walioshiriki katika uchaguzi wa mwaka 2015 ambao kimsingi ulikuwa na mwamko mkubwa kuliko huu wa marudio.

Katika uchaguzi wa juzi, mgombea wa Chadema, Yonas Laizer, alitangazwa kupata kura 3,187 akifuatiwa na Wilfred Mlay wa ACT-Wazalendo aliyepata kura 144, Feruz Juma wa NRA alipata 45 na Simon Ngilisho wa Demokrasia Makini aliyepata kura 35.

Wengine ni Omary Juma wa DP aliyepata kura 34, mgombea wa ADA-Tadea, Francis Ringo kura 21 na Elizabeth Salewa wa chama cha Wakulima aliyepata kura 16.

Hii inafanya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi huo wa marudio ambao hata Tume ya Uchaguzi ilieleza kuwapo kwa idadi kubwa ya wapiga kura ambao hawakujitokeza kufikia 69,196 ikiwa ni kura 7,880 zaidi ya kura zote zilizopigwa mwaka 2015, ambazo zilifikia 61,316.

Katika uchaguzi wa mwaka 2015, Kalanga alipata kura 35,024 na kumwangusha aliyekuwa mpinzani wake, Namelock Sokoine aliyegombea kupitia CCM na kupata kura 25,925.

Uchaguzi Ukonga

Katika matokeo ya uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita, Septemba 16, mwaka huu Tume ya Taifa ya Uchaguzi pia ilimtangaza mgombea wa CCM, Mwita Waitara kuibuka mshindi na kuendelea kulitumikia jimbo hilo.

Waitara pia, kama ilivyokuwa kwa Kalanga alitangaza kujiuzulu ubunge alioupata kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 hivyo kulazimika kufanyika uchaguzi wa marudio, ambapo CCM ilimchagua kuwania tena nafasi hiyo kupitia chama hicho.

Msimamizi wa uchaguzi katika Jimbo la Ukonga Jumanne Shauri alimtangaza Waitara kuwa mshindi kwa kura 77,795  sawa na asilimia 89.19 na Asia Msangi wa Chadema alipata kura 8,676 sawa na asilimia 9.95.

Katika jimbo hilo, wapiga kura walioandikishwa walifikia 300,609 ila waliojitokeza ni 88,270 sawa na asilimia 29.4 na katika jimbo hili, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Kaijage anakiri pia kuwa wapiga kura waliojitokeza walikuwa wachache.

Kwa mwaka 2015, ambapo kama ilivyoainishwa kwenye gazette la Serikali la Oktoba 28, 2015 idadi ya kura iliyopigwa ilikuwa 177,736 hivyo kufanya kura zilizopigwa msimu huu wa marudio kuwa pungufu kwa kura 89,466 hivyo wapiga kura wanaonekana kupungua kwa karibu nusu ya wale waliojitokeza mwaka 2015.

Katika matokeo hayo ya mwaka 2015, Waitara alionekana kupata kura nyingi lakini kutokana na mwamko wa wapiga kura ambao walijitokeza kwa wingi, kura zake zilifikia asilimia 50.9 kati ya kura za wagombewa wote wa vyama 10 vilivyoshiriki katika uchaguzi huo.

Katika jimbo hili, hesabu imejaribu kuwekwa sawa, kwa kuwa Waitara anaonekana kupata kura 77,795 tofauti na kura 90,478 alizopata katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 alipogombea akiwa Chadema, safari hii ikionesha amepoteza kura 12,683 ikilinganishwa na kura alizopata mwaka 2015.

Malalamiko ya Chadema 

Matokeo hayo ya uchaguzi mdogo yanatangazwa wakati Chadema ikiwa na malalamiko yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu, John Mnyika akidai kuwa mwenendo mzima wa uchaguzi haukuwa sawa.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akilalamikia mwenendo wa uchaguzi huo akidai kuwa kumekuwa na viashairia vingi vya udanganyifu.

Mnyika anaelekeza lawama zake kwa Jaji Kaijage aliyesema kuwa uchaguzi unaendelea vizuri wakati kukiwa na taarifa za kuzuiwa mawakala wa upinzani tangu saa 12 asubuhi hadi saa mbili ndipo walipoanza kuruhusiwa kuingia vituoni.

Alisema hatua hiyo ya Jaji Kaijage ni kudhihirisha kuwa madhaifu yote yanayoonekana katika uchaguzi huo, ambayo ni pamoja na tuhuma za kutumiwa kwa wasimamizi wa uchaguzi vituoni kuwazuia mawakala kisha kuweka karatasi za kura kwenye maboksi na baadaye kuwaruhusu kuingia vituoni wakati kura zikiwa zimeshapigwa yamepata baraka za tume hiyo.

Katika malalamiko yake, Mnyika anaeleza kuwa kwenye eneo hilo la Shule ya Msingi Juhudi alipozungumzia Mwenyekiti huyo wa NEC lililokuwa na vituo 10, ni mawakala watatu tu wa Chadema walioruhusiwa huku chama hicho kikiwa kimepeleka mawakala wote 10.

“Kwa taarifa tulizokuwa tumezipata, ilipofika saa 12 asubuhi, muda ambao mawakala wanatakiwa kuwapo vituoni mawakala wetu walikwenda katika vituo vyote 673, wakiwa na barua za chama lakini walianza kuzuiwa kwamba wawe na nakala za viapo,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa maelekezo ya NEC, vyama vilitakiwa kupeleka orodha na picha mbili za mawakala siku saba kabla ya uchaguzi kisha tume ndiyo itakayopeleka majina vituoni na kwamba mawakala hawatatakiwa kwenda na kitambulisho chochote siku ya uchaguzi.

Alisema walibaini kuwa tume ilitoa maagizo hayo ya kutaka zipelekwe barua za utambulisho na picha za mawakala na kwamba mawakala hawatahitaji utambulisho mwingine vituoni ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhujumu uchaguzi huo.

Alisema kwa kuwa maelekezo hayo hayakutekelezwa kama ilivyoagizwa na kusababisha mawakala wao kuzuiwa muda wa asubuhi, wanaamini hiyo ilifanywa makusudi ili kutekeleza wizi wa kura katika vituo, unaodaiwa kufanywa kwa kutumia wasimamizi wa vituo vya kupigia kura.

“Baada ya kufuatilia, tulibaini kuwa wasimamizi wote walipewa jukumu la kutekeleza wizi wa kura, kwa hiyo waliamua kuzuia mawakala wetu kuanzia saa 12 hadi saa 2 asubuhi na kutekeleza wizi wa kura kwa kujaza karatasi za kura kwenye maboksi, kisha kuwaruhusu waingie.

“Walifanya hivyo wakijua kwamba watakuwa wamepoteza ushindi kwa kuwa mawakala wetu hawakupata muda wa kukagua maboksi kabla hayajaanza kuwekwa kura na waliruhusiwa kuingia wakati yalikuwa tayari wapiga kura wameshaingia na wao walishatumbukiza kura zao kwenye maboksi,” alisema.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Kibamba, alisema hadi kufikia Jumapili mchana, mawakala 20 wa Chadema katika kata za Msongola, Gongolamboto, Mzinga, Majohe walikamatwa na kuwekwa rumande katika kituo cha Polisi cha Stakishari, Ukonga.

Alisema pamoja na hujuma hizo, mawakala wachache walioruhusiwa kuingia katika vituo walitekeleza wajibu wao hadi mwisho na chama hicho kitatoa taarifa yake kuhusu uchaguzi huo.

Msimamizi wa kituo namba tano cha Pugu Mnadani, Josephat Musiba ambaye alizungumza na MTANZANIA alisema taarifa za kuzuiwa mawakala katika eneo hilo si sahihi, japokuwa kulitokea kutoelewana katika hatua za awali.

Alisema baadhi ya mawakala walifika na barua kutoka vyama vyao bila hati ya kiapo kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi lakini baada ya muda walielewana na kuwaruhusu kuendelea kuwapo katika vituo vyao.

Uchaguzi ulivyokuwa Kinondoni na Siha

Marudio ya chaguzi hizi, ukiacha hesabu iliyotia for a ya marudio ya uchaguzi katika Jimbo la Monduli wiki iliyopita, ambapo inaonekana idadi ya wapiga kura ilikuwa kubwa zaidi ya mara mbili ya wale waliojitokeza mwaka 2015, pamoja na maelezo ya NEC kuwa idadi ya waliojitokeza vituoni ni ndogo, hali imekuwa tofauti katika chaguzi zilizopita.

Katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Siha uliofanyika Februari 27, mwaka huu pia haukunusurika ambapo ni wapiga kura 32,277 (asilimia 58.35) tu kati ya watu 55,313 waliojiandikisha kupiga kura ndiyo waliojitokeza.

Hasira za wapiga kura zilikuwa dhahiri pia katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni ambapo ni wapiga kura 45,454 (asilimia 17.2) pekee ya watu wote waliojiandikisha kupiga kura ndiyo waliyojitokeza kupiga kura.

Singida Mjini, Longido na Songea mjini

Katika uchaguzi wa marudio Jimbo la Songea Mjini, Singida Kaskazini na Longido uliofanyika Januari 13, mwaka huu idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura pia ililalamikiwa kuwa ndogo tofauti na idadi ya watu waliojiandikisha.

Katika uchaguzi huo, kati ya watu 278,167 waliojiandikisha kupiga kura katika majimbo hayo matatu ni watu 110,883 pekee ndio waliojitokeza kupiga kura, huku kukiwa na watu 167,284 ambao hawakushiriki katika upigaji kura, ambao ni sawa na asilimia 60.14 ya wapiga kura wote waliojiandikisha.

ends

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here