21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

‘WATOTO NJITI WANAKABILIWA NA MATATIZO MENGI’


Na VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM -

WATOTO wanaozaliwa kabla ya ujauzito kutimiza umri wa miezi tisa (njiti) hasa chini ya kilo moja hukabiliwa na matatizo mengi ikiwamo ya ubongo na hata kufariki dunia.

Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Robert Moshiro alisema hayo alipozungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalum.

Akifafanua alisema mara nyingi mtoto njiti mwenye uzito wa chini ya kilo moja, mishipa yake ya damu huwa laini mno kwa kipindi cha siku tatu tangu anapozaliwa, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuvilia damu na hata mishipa yake kupasuka na ikiwa hali hiyo itatokea kichwani huweza kumsababishia ubongo wake kushindwa kufanya kazi inavyotakiwa,” alisema.

Aliongeza  “Ubongo wa mtoto huwa una-fail kabisa na matokeo yake anaweza kupoteza maisha au ikiwa ataishi basi anakuwa na matatizo ya ubongo katika maisha yake yote.

Alisema watoto waliozaliwa katika kipindi cha wiki 34 cha ujauzito hukabiliwa zaidi na changamoto nyingi.

Dk. Moshiro alifafanua kwamba kibaiolojia mtoto huishi ndani ya tumbo la mama kwa kipindi cha miezi tisa tangu kutungwa mimba hadi kuzaliwa kwake.

“Katika kipindi hicho tunatarajia kwamba mtoto huyo atakapozaliwa anakuwa amekamilika na viungo vyake vinakuwa vimekomaa vema,” alisema.

Aidha katika ufafanuzi huo Dk. Moshiro alisema hata hivyo inapotokea mtoto amezaliwa kabla ya wakati huo, viungo vyake vingi ukiwamo moyo, ini, figo na vinginevyo vinakuwa bado havijakomaa inavyotakiwa.

“Na ndipo hapo changamoto inapotokea, kwa kawaida mtoto huwa anakamilika kuumbwa viungo vyake ndani ya wiki 24  tangu mimba ilipotunga lakini zile ogani za ndani zinakuwa bado hazijakomaa.

“Viungo hivyo hukomaa katika zile wiki 12 za mwisho za ujauzito, hapo mtoto huendelea kupokea virutubisho vyote muhimu kutoka kwa mama yake ili kuwezesha kukamilika kwa viungo vyake,” alibainisha.

Aliongeza “Hivyo, anapozaliwa kabla viungo vyake vinakuwa bado havijakomaa tayari kwa kuja kukabiliana na mazingira ya huku nje,

Dk Moshiro alitaja matatizo mengine yanayowakabili watoto hao wanaozaliwa kabla ya wakati kuwa ni pamoja na usikivu (uziwi), ulemavu wa kudumu wa kuona na mengineyo.

“Lakini wakati mwingine matatizo hayo huweza kutibika ikiwa yatagundulika mapema na ndiyo maana tunashauri wanawake kuwahi kliniki pindi wanapojihisi ni wajawazito ili kufanyiwa uchunguzi kujua umri wa mimba, tatizo lililopo ni kwamba wengi hukadiria,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles