26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

WASIORUDISHA FOMU ZA MAADILI KUFUKUZWA KAZI


Na FERDINANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM -

SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewataka viongozi wa umma kurudisha  fomu za tamko la maadili ya mali walizojaza wakati wanaapishwa kuwa viongozi.

Baadhi ya hatua za kinidhamu ambazo zinaweza kuchukuliwa dhidi ya kiongozi wa umma atakayekiuka agizo la kujaza fomu ni kuonywa au kupewa tahadhari, kushushwa cheo, kusimamishwa kazi au kufukuzwa kazi.

Viongozi hao wanapaswa kuwasilisha fomu hizo katika ofisi za sekretarieti hiyo ndani ya siku tatu kuanzia jana.

Agizo hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Kamishna wa Maadili wa Sekretarieti hiyo, Jaji Mstaafu Harold Nsekela alipozungumza na waandishi wa habari.

Alisema agizo hilo limetolewa kwa  kuzingatia Sheria ya Maadili  ya Viongozi wa Umma kifungu cha 9 (1) (b) ambacho kinaeleza kiongozi wa umma ana wajibu wa kurudisha fomu ya tamko la maadili.

Jaji Nsekela alisema sheria hiyo inamtaka kiongozi kuwasilisha fomu kila mwisho wa mwaka ili kujua mali na rasilimali anazozimiliki ikiwamo mke au mume na watoto wake walio chini ya miaka 18 na ambao hawajaolewa wala kuoa.

“Kwa kuzingatia kifungu cha 9 (1) (a) na (c) cha sheria hii, viongozi wapya wanaochaguliwa au kuteuliwa wanatakiwa kujaza fomu hizo na kuzirejesha kwa kamishna ndani ya siku 30 baada ya kupewa wadhifa.

“Kiongozi anapofika mwisho wa kutumikia wadhifa wake anatakiwa tena kujaza fomu za tamko la rasilimali na  madeni na kuziwasilisha kwa kamishna,” alisema Jaji Nsekela.

Alitoa wito kwa viongozi wote ambao bado hadi sasa hawajajaza fomu wajaze na kuziwasilisha katika ofisi za Sekretarieti jijini Dar es Salaam, Ofisi za Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Ziwa (Mwanza) na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani Mbeya.

Naye Ofisa Sheria Mkuu wa Sekretarieti hiyo, Filotheus Mawila, alisema Sheria ya Maadili haimzuii mtumishi wa umma kumiliki mali nyingi au kutomiliki kabisa.

“Isipokuwa sekretarieti itachunguza mali alizokuwa nazo awali na alizonazo sasa kujiridhisha iwapo zinaendana na kipato chake,” alisema Mawila.

Alisema  endapo mtumishi husika atatiliwa shaka kwamba huenda aliidanganya sekretarieti katika maandishi yake aliyojaza kwenye fomu, aliiba au alidhulumu juu ya upatikanaji wa mali zake atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.

“Lengo la serkretarieti hii ni kujenga na si kubomoa ili kulinda miongozo na sheria za utumishi wa umma zilizowekwa,  ni furaha pia kuona viongozi wanaenda sawa na sheria na si kukiuka  maadili ya uongozi,” alisema.

HATUA ZA NIDHAMU

Hatua zingine zinazoweza kuchukuliwa ni kiongozi husika kushauriwa kujiuzulu wadhifa wake sanjari na kupewa adhabu zingine zinazoruhusiwa kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo kabla ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu kiongozi husika huruhusiwa kujitetea kwanini alichelewa kutoa tamko na iwapo sababu zake zitaonekana hazina msingi wowote sheria hufuata mkondo wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles