JOSEPH HIZA NA MTANDAO
JUNI 12 ya kila mwaka ni siku ya kupinga ajira kwa watoto duniani, ikiangazia maswahibu yanayowakumba kwa namna mbalimbali tangu ilipoanzishwa mwaka 2002 na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Ajira za watoto ni jambo linalopigwa vita dunia nzima kutokana na ukweli kwamba ni kazi zinazohatarisha makuzi ya mtoto na kumweka katika hatari au hali tete na kumsababishia maisha mabovu mbeleni.
Miongoni mwa namna inavyoangaziwa ni jinsi mizozo, vita na majanga inavyoathiri watoto hadi kulazimika kufanyishwa kazi kinyume na sheria za kimataifa.
Mara nyingi watoto ndiyo huathirika zaidi kwa kukosa elimu na hata kupoteza familia zao.
Hali hiyo huwalazimisha wengi kufanya kazi ili mradi mkono uende kinywani, lakini katika hali ya kinyonyaji mno kutokana na ukubwa wa kazi na malipo duni huku mara nyingi wakiathirika kiafya.
Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Watoto (UNICEF), takriban watoto 40,000 wanafanya kazi katika migodi iliyo na madini ya Cobalt katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Aidha, Shirika la kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limesema baadhi ya watoto hao ni wa umri mdogo wengine wakiwa na miaka saba na huwa hawana vitenda kazi vinavyotakiwa kama mavazi ya kuwakinga dhidi ya madhara ya uchimbaji madini.
Wanafanyakazi wakati mwingine hadi saa 24 ndani ya migodi, watoto hao hulipwa chini ya dola mbili kwa siku na wengi wao hupokea ujira mdogo kuliko huo.
Madini hayo adimu ya Cobalt hutumika kutengezea betri za simu za kisasa za mkononi na hivyo, mashirika makubwa ya teknolojia kama vile Apple, Tesla, Microsoft, Samsung na Sony huyategemea madini hayo kutengezea bidhaa zao za kielektroniki.
Madini hayo pia yanatumika katika magari ya kieletroniki yanayotengezewa na kampuni kama vile Daimler na Volkswagen.
Hata hivyo, kampuni hizo hazikutaka kuhusishwa na biashara ya watoto kutumikishwa katika ajira.
Hivi majuzi, Shirika la Habari Marekani CBS kupitia mwandishi wake Debora Patta, liliendesha uchunguzi ikiwa ni miaka miwili tangu ripoti ya kushtusha ya Amnesty ichapishwe.
Katika safari hiyo ya karibuni maeneo ya kusini mwa nchi, CBS News ilishuhudia kile kinachoonekana kama Pori la Magharibi, ambako watoto huonekana wakichimba mitaro na kufanyishwa kazi ziwani – wakisaka hazina katika mazingira ya kutisha.
Ni kazi ngumu kwa mtu mzima, lakini inayofanywa na watoto wadogo. Na bado makumi kwa maelfu ya watoto wa Kongo wanahusika katika kila hatua ya uchumbaji wa cobalt.
Zaidi ya nusu ya usambazaji wa madini hayo duniani hutokea DRC na asilimia 20 huchimbwa kwa mikono, kwa mujibu wa Kampuni ya utafiti ya Darton Commodities Ltd yenye makao makuu London, Uingereza.
Patta na timu yake waliosafiri katika barabara mbovu waliona watoto kila mahala, wakichimba cobalt katika mashimo yaliyotelekezwa.
Inaonekana wazi maofisa wa usalama wanaosimamia hapo, wachache wakiwa wamevalia sare, wana kitu cha kuficha.
Ni kwa sababu hiyo, timu ya CBS News ilizuiwa kila baada ya hatua chache, maofisa wakitaka barua na nyaraka za kuwaruhusu licha ya kwamba walikuwa tayari na kibali cha kufika hapo.
Lakini mawakala wa Kichina wanaonunua cobalt, hawakukumbana na kikwazo chochote kuingia na kutoka eneo hilo hilo la mgodi.
Katika migodi wanawake na watoto wanaowasaidia wanaoitwa wataalamu wa madini.
Lakini watoto wa miaka hadi minne huonekana wakibeba vifusi vizito kutoka mashimoni huku vichanga vilivyopo migongoni mwa mama zao vikikumbana na uchafu au kucheza katika uchafu bila kujua wakivuta hewa ya sumu.
Maofisa eneo hilo hukana ajira ya watoto, lakini wanakana kitu kinachoonekana dhahiri kuwaumbua na ili kukabili hilo, kila kamera au watu wa usalama au polisi wanapoonekana, watoto hufukuzwa haraka kutoka mgodini.
Mmoja wa watoto, Ziki Swaze (11) baada ya kuulizwa na Patta kwanini hayuko shule, anajibu: “Wazazi wangu wamekufa, naishi na bibi. Kipato chetu na mahitaji ya shule yanatokana na madini ya cobalt.
Faustin Adeye anayefanya kazi na shirika la Kikatoliki la Misereor ameliambia Shirika la Habari la Ujerumani (DW) kuwa mazingira ya kazi migodini nchini humo ni ya kusikitisha na kuongeza kuwa watoto wengi huathirika kimwili kutokana na kufanya kazi katika migodi hiyo.
Adeye anasema hali katika migodi kadhaa kusini mwa Congo ni mbaya kiasi kwamba wakati mwingine watoto wao huzikwa wakiwa hai wakati migodi hiyo inapoporomoka.
Desemba mwaka juzi, DW ilizitaka baadhi ya kampuni hizo kuzungumzia suala hilo la watoto kuajiriwa Congo kuchimba madini.
Daimler, moja ya kampuni kubwa za kutengeneza magari Ujerumani ilijibu kwa maandishi kuwa inahitaji watu wanaowauzia bidhaa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo kimataifa.
Daimler ilisema mwongozo wa kampuni hiyo kuhusu mazingira ya kazi, viwango vya kijamii na kimaadili pamoja na uhifadhi wa mazingira unakwenda mbali ya vigezo vya kisheria vya kuzingatia yote hayo.
Iliongeza kuwa inatarajia wanaowauzia bidhaa za kutengeza magari yao kuheshimu na kuzingatia angalau vigezo vyote hivyo.
BMW, kampuni nyingine ya Ujerumani ya kutengeza magari imekubali kuwa imetumia madini ya Cobalt kutoka Congo katika utengenezaji wa baadhi ya betri zao na kutangaza kuwa itaanzisha ukaguzi wa kuhakikisha wanaowauzia bidhaa hiyo hawakiuki sheria za haki za binadamu.
Kampuni ya Marekani ya Apple ilitangaza Machi mwaka jana kuwa inanuia kuacha kununua cobalt inayochimbwa kwa kutumia mikono kutoka Congo.