26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Watoto 10 jamii ya Kimasai wanusurika kukeketwa Moshi

UPENDO MOSHA-MOSHI



WATOTO wachanga wa kike zaidi ya 10 wa jamii ya Kimasai, wamenusurika kukeketwa katika Kijiji cha Masaini, Kata ya Arusha Chini, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Watoto hao ambao walikuwa wakeketwe katika kipindi cha Agosti 2017 hadi Februari 2018, walinusurika kufanyiwa ukatili huo wakiwa katika hatua za mwisho na wanaharakati wa shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya uwezeshaji wa kiuchumi kwa makundi maalumu yakiwamo ya wanawake na vijana la Tusonge.

Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini Moshi, Mratibu wa mradi kupinga mila na desturi potofu, zinazopelekea ukatili wa kijinsia na ukeketaji, Joyce Kessy, kutoka katika shirika hilo, alisema watoto hao wachanga waliokolewa kufanyiwa kitendo hicho kwa nyakati tofauti.

“Mradi huu unatekelezwa katika Kata ya Arusha Chini na Shirika la Tusonge kwa kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha vitendo hivyo vinapingwa kwa nguvu zote.

“Katika kipindi cha Desemba, ndicho kipindi ambacho jamii ya wafugaji hufanya sherehe za ukeketaji na kipindi hicho ndicho tulifanikiwa kuwaokoa watoto hao.

“Shirika la Tusonge, lilianza mradi huo wa kupinga mila na desturi potofu katika Kata ya Arusha Chini mwaka 2017 kwa kufadhiliwa na Shirika la The Foundation for Civil Society katika awamu yake ya  kwanza.

“Sasa tumeweka mkakati wa pamoja na maofisa afya walioko katika maeneo hayo ili kukubaliana kila mzazi atakayempeleka mtoto wake hospitali kwa ajili ya matibabu, akaguliwe kama amekeketwa ili kuweza kuangalia ukubwa wa tatizo hilo,” alisema Kessy.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tusonge, Agnatha Rutazaa, aliiomba Serikali kuyaimarisha mabaraza ya usuluhishi yaliyoko ndani ya kata ili kuweza kutenda haki pindi wanapotoa maamuzi bila kuangalia uwezo wa mtu.

Pamoja na hayo, alisema katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia inayoadhimishwa kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10, Shirika la Tusonge limeanza kutoa elimu kwa makundi ya vijana ili kuwa chachu ya mabadiliko ndani ya jamii katika kukemea masuala ya ukeketaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles