Na Editha Karlo, Bukoba
BAADHI ya wazazi wilayani Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera wametelekeza familia zao baada ya wilaya hizo kukumbwa na njaa.
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Charles Tizeba alikuwa akizungumza na wadau mbalimbali mjini hapa jana katika maadhimisho ya siku ya chakula duniani ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Kagera.
Alisema amefanya ziara katika baadhi ya kata za wilaya za Karagwe na Kyerwa na kujionea jinsi mazao katika baadhi vijiji yalivyoungua shambani na kaya zilivyokumbwa na baa la njaa.
“Jana nimekwenda Kata ya Biyanga, kwa kweli hali ni mbaya na inatisha. Kijiji ni kikavu mazao yote yameungua shambani, kuna familia nimewakuta watoto wapo peke yao nilipowauliza wazazi wao walipo wakasema wamewakimbia sababu ya njaa na wao wanashindia uji tu, kwa kweli hii ni hatari.
“Mashamba ya ndizi, mibuni na mazao mengine waliyokuwa wanategemea wananchi wa maeneo hayo kwa chakula yote yameungua kwa sababu ya jua kali na mvua haijanyesha tangu Juni hadi sasa,” alisema Dk. Tizeba.
Alisema ameamua kuchukua hatua za awali kwa kuwataka Wakala wa Taifa wa Chakula (NFRA) kutoka ghala ya kanda ya Shinyanga kuleta chakula haraka ndani siku tatu.
“Ni bora kuchukua hatua za tahadhari kabla hali haijawa mbaya zaidi na watu kuanza kufa, zitaletwa tani 20 za mahindi ndani ya siku tatu zitakuwa hapa. Mkoa ufanye utaratibu wa chakula hicho kiwafikie waathirika kwa haraka,” alisema
Alisema kutokana na baa hilo la njaa hata mifugo nayo imeathirika hivyo amewataka wananchi walime mazao yanayovumilia ukame.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Salumu Kijuu alisema ni kweli wilaya hizo zimekumbwa na baa la njaa na tayari amewasiliana na wakuu wa wilaya hizo na kutoa taarifa kitengo cha maafa ofisi ya Waziri Mkuu.
Kijuu alisema tatizo ni kwamba wakazi wa Kagera huwa hawapendi kulima mazao kama mahindi, wamezoea kulima ndizi kama chakula chao kikuu.