WASHINGTON: MAREKANI
MGOMBEA wa urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican, Donald Trump, amemshutumu mpinzani wake wa Chama cha Democrat, Hillary Clinton kuwa huenda alitumia aina fulani ya dawa, wakati wa mjadala wao uliopita.
Alisema alikuwa na haiba mwanzoni mwa mjadala huo.
Trump alipendekeza wote wafanyiwe uchunguzi wa matumizi ya dawa kabla ya kufanyika mjadala wao wa mwisho Jumatano wiki hii.
Katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika New Hampshire, Trump kwa mara nyingine, alidai kuna njama za kumwibia kura.
Timu ya kampeni ya Hillary, ilisema wapiga kura sasa wameona bayana kile anachokiita juhudi za aibu za Trump za kutaka kuhujumu shughuli za upigaji kura.
Umaarufu wa Trump umezidi kudidimia katika majimbo mengi, huku akikabiliwa na madai ya kudhalilisha wanawake.