25.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

WATANZANIA TUMIENI FURSA UJENZI WA BOMBA LA MAFUTA

Rais, Dk. John Magufuli na mwezake Yoweri Museveni wa Uganda wanatarajia kufanya tukio la kihistoria kati ya nchi hizo mbili.

Tukio hilo linahusu uzinduzi rasmi wa ujenzi mkubwa wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda kwenda Tanga.

Katika toleo la jana la gazeti la MTANZANIA, ilielezwa kwa kina namna ambavyo fursa nane zinavyoweza kupatikana katika mradi mkubwa na wa kihistoria Afrika Mashariki.

Tunaamini wadau wengi na wapenda maendeleo, wataanza kutumia nafasi hii itakayosaidia Watanzania kubaki na ujuzi kwa kushiriki katika ujenzi huo.

Tunategemea wazi kabisa kwamba, hata baada ya kukamilika kwa mradi huu utaalamu wa ujenzi wa mabomba ya gesi utabaki nchini.

Tunasema hivyo kwa sababu Tanzania hatuna uwezo wa kujenga mabomba hayo, licha ya kuwapo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Tunatambua shirika letu lina uwezo wa ndani kusaidia kupata wataalamu ambao wataweza kujenga mabomba  ya gesi na mafuta katika miradi mbalimbali.

Fursa mbalimbali zilizopo katika mnyororo wa ongezeko la thamani zinazohitajika katika mradi huu, zitaweza kupatikana, zikiwamo za ujenzi, huduma za chakula, ulinzi, uuzaji wa vifaa vya ujenzi, huduma za afya, sheria, fedha na bima.

Mradi huo unatajwa kuwa utaweza kutoa ajira zaidi ya 10,000 kwa Watanzania na kufungua fursa za biashara katika mikoa minane itakayopitiwa na bomba hilo, ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Pamoja na ajira hizo, mradi huu unategemea kugharimu Dola za Marekani bilioni 3.5 sawa na Sh trilioni 8 za kitanzania.

Hili ni jambo, ambalo tunategemea bomba hili ambao litakuwa na urefu wa kilomita 1,145 na asilimia 80 ya ujenzi huu unafanyika Tanzania. Ni wazi kabisa kwamba tuna kila sababu ya kujipanga ipasavyo kutumia fursa hizi.

Pamoja na fursa hizi kwa wananchi, mradi huu utaisaidia Serikali kuongeza mapato kupitia vyanzo vyake mbalimbali.

Ni matarajio yetu, makampuni ya watoa huduma za mafuta na gesi yanapaswa kujiunga katika jumuiya hiyo ili  kuchangamkia  jambo hili.

Tunatoa rai kwa makampuni ya ujenzi  ya wazawa kujitokeza kwa wingi kwenye eneo la mradi huu wapate nafasi ya kuonesha uwezo wao.

Hadi kumalizika mradi huo, uchumi wa Tanzania utapanda ikiwa ni pamoja na kuwapo ongezeko kubwa la matumizi ya mafuta na gesi kuliko hivi sasa.

Ni wazi kwamba Tanzania na Uganda ambazo zimekuwa na ushirikiano wa miaka mingi, zitafaidika mno na upatikanaji wa mapato ya kodi ambayo kwa namna moja au nyingine yatasaidia wananchi wa pande zote mbili.

Kwa msingi huo, tunasema kusema huu ndiyo ushirikiano wa dhati ambao siku zote tumekuwa tukiulilia hasa kwa nchi za Afrika ambazo zimekuwa ngumu kuungana katika baadhi ya mambo ya msingi.

Sisi MTANZANIA, tunaamini baada ya uzinduzi wa ujenzi wa mradi huu wa kihistoria, kila mkazi ambaye mikoa yote imetajwa bomba kupita, wajipange vizuri kutumia fursa hizi.

Tunasema hivyo, kwa sababu kama kila mmoja atajipanga vizuri, ni wazi sasa wananchi wataondokana na umasikini mdogo mdogo.

Tunamalizia kwa kuipongeza Serikali kufikia hatua hii ambayo itaitangaza vya kutosha Tanzania  ngazi za kimataifa.

Pia tunapongeza kufanikisha uwekezaji  huu mkubwa ambao sasa unaieleta Tanzania ya viwanda machoni mwa Watanzania kwa vitendo kuliko maneno zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles