Na Clara Matimo, Mwanza
Watanzania 940,507, wamepata chanjo ya Uviko 19 sawa na asilimia 88.9 ya chanjo zote 1,058,400 aina ya JJ zilizoingia nchini awali huku lengo la serikali likiwa ni kutoa chanjo kwa asilimia 60 ya wananchi wote.
Hayo yamebainishwa jijini Mwanza Oktoba 17, 2021 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati akitoa taarifa ya serikali ya wiki kwa waandishi wa habari mkoani humo.
Amesema shehena ya chanjo 1,065,000 aina ya Sinopharm zilizoingia nchini wiki iliyopita kutoka nchini China zimeanza kusambazwa katika halmashauri na mikoa yote ambapo zoezi la kuchanja wananchi linaendelea.
“Pamoja na chanjo hizo pia tunatarajia kupokea chanjo zingine aina ya Pfizer dozi 500,000 mwishoni mwa mwezi huu wa kumi kutoka Covax Facility ambazo ni sehemu ya dozi milioni 3.7 za chanjo aina ya pfizer ambazo nchi yetu itazipata kwa awamu,”amesema na kuongeza:
“Hivi ninavyoongea majokofu ya baridi kali 14 yenye uwezo wa kuhifadhi chanjo milioni 3.7 yameishafungwa pale jijini Dar es Salaam lakini kupitia Covax Facility tunatarajia kupata dozi milioni 11.8,”amesema Msigwa.
Aidha Msemaji huyo wa serikali amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya korona kama wanavyoelekezwa na madaktari ikiwemo kuchanjwa, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, kuvaa barakoa, kuepuka misongamano, kufanya mazoezi na kula vyakula vyenye lishe bora.