24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yatoa wito kwa wafanyabiashara kujiepusha na biashara za magendo

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imewataka wafanyabiashara nchini kujiepusha
na biashara za magendo wakati wanapofanya shughuli zao za kibiashara katika
maeneo yao ili wao wenyewe pamoja jamii inayowazunguka wasiathirike na athari
zitokanazo na biashara hiyo.

Afisa Forodha Mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Muhidini Mwalugoya (aliyesimama) akitoa elimu kuhusu athari za magendo kwa wavuvi wa pwani ya Kilwa Kivinje hivi karibuni wakati wa kampeni ya utoaji elimu kuhusu athari za magendo katika Mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Afisa Forodha Mwandamizi wa TRA, Muhidini
Mwalugoya wakati wa kampeni maalumu ya utoaji elimu kuhusu athari za magendo
iliyofanyika katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Amesema kuwa kufanya biashara za magendo kunaweza kuleta athari nyingi katika
jamii kiafya, kiuchumi na usalama wa nchi na kwamba inapotokea wafanyabiashara
wanaingiza bidhaa zao kupitia njia zisizo rasmi maarufu kama njia za panya, jamii ya
eneo husika huathirika.

“Kwa mfano uingizaji wa vyakula au bidhaa zisizo na viwango ama zilizopita muda wake wa matumizi kunaweza kupelekea mlipuko wa magonjwa na kuathiri wananchi,”
amesema Mwalugoya.

Ameongeza kuwa, athari nyingine zitokanazo na biashara ya magendo ni pamoja
usalama wa nchi kwani baadhi ya watu wasio na lengo zuri ama waharifu wanaweza
kuingiza nchini bidhaa ambazo ni hatari kwa usalama wa nchi kama kuingiza silaha au risasi ambazo baadaye huweza kusambaa katika jamii na kuleta machafuko.

“Watanzania wenzangu, athari za kufanya biashara za magendo ni nyingi hivyo lazima
tuhakikishe kuwa tunaelimishana ili wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla
waachane na kufanya biashara za namna hii, kwa mfano tukiendekeza kupitisha bidhaa kutoka nje ya kwa njia zisizo rasmi tunaweza kuathiri uchumi wa nchi yetu pia, kwasababu zitakua hazilipi kodi na matokeo yake tunakosa mapato stahiki ya kutuletea maendeleo nchini, hivyo niwaombe sasa tuachane na hizi biashara”, amesema Mwalugoya.

Afisa Forodha Mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ernest Mngube (aliyesimama) akitoa elimu na kujibu maswali kuhusu athari za magendo kwa wavuvi wa pwani ya Kilwa Kivinje hivi karibuni wakati wa kampeni ya utoaji elimu kuhusu athari za magendo katika mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara.

Aidha, amewataka wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kuwa
wanatumia njia zilizo rasmi katika kupitisha bidhaa zao ili TRA iweze kukusanya mapato na pindi wapatapo changamoto yoyote wasisite kuwasiliana na maofisa wa TRA katika maeneo husika ikiwemo kutoa taarifa kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama mara waonapo baadhi ya watu au kikundi cha watu wanafanya biashara za magendo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kilwa Kivinje Wilayani Kilwa,
Mohammed Msumeno amesema kuwa, anaishukuru TRA kwa kutoa elimu hiyo kwa
jamii ya eneo lake na kuahidi kuiepeleka elimu hiyo kwa wengine na ametoa wito kwa
wakazi na wafanyabiashara wa Kilwa Kivinje kuachana na biashara za magendo na

kukemea vikali wale wanaofanya biashara hizo na kuahidi kutoa taarifa za wale
watakaobainika kwa vyombo husika ili wachukuliwe hatua.

Mmoja wa wafanyabiashara ambaye pia ni mvuvi wa eneo la Kilwa Kivinje, Nurdin
Likwata ametoa maoni yake kuhusu elimu iliyotolewa na TRA kuhusu biashara za
magendo ambapo amesema kuwa, elimu hiyo wameipokea na wataizingatia
kwasababu ina manufaa kwao na kwa vizazi vyao na kuahidi kuwa mstari wa mbele
kukemea wale wote watakaobainika kuendesha biashara za magendo.

“Kiukweli hii elimu tuliyopewa na hawa watu wa TRA tulikua wala hatuifahamu,
tumeipokea kwa mikono miwili na mimi binafsi naahidi kuwa mstari wa mbele
kuhakikisha kwamba nakemea vikali biashara ya magendo, kwanza ina madhara
makubwa sana kwetu sisi na hata kwa watoto wetu lakini pia tunaiomba TRA iendelee
kutupatia elimu hii mara kwa mara”, amesema Likwata.

Elimu kuhusu biashara za magendo nchini ni endelevu na ni moja ya vipaumbele vya
TRA iliyojiwekea katika Idara ya Forodha katika kuhakikisha kuwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wanaelimishwa ipasavyo kuhusu madhara yatokanayo na
biashara za magendo na hatua mbalimbali za kuchukua pindi waonapo watu
wanajihusisha na biashara hizo ikiwemo kutoa taarifa TRA pamoja na kwenye vyombo
vya Ulinzi na Usalama ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles