21.4 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara Ruvuma waipongeza TRA kuendesha kampeni ya Elimu ya Kodi kwa Mlipakodi

Na Mwandishi Wetu, Ruvuma

Wafanyabiashara wa mjini Songea mkoani Ruvuma wameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kufanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani humo ambapo wamesema kuwa kwa sasa kuna mabadiliko makubwa ndani ya mamlaka hiyo ikilinganishwa na hapo awali.

Akizungumza wakati wa kampeni hiyo mkoani humo, Chasiko Mhagama ambaye ni mfanyabiashara Mjini Songea, amesema kuwa licha ya TRA kuwafikia na kuwapa elimu ya kodi, kuna maboresho makubwa yamefanyika kwenye mifumo ya ulipaji kodi suala ambalo limeondoa usumbufu kwa walipakodi.

“Mwanzoni mfanyabiashara alikuwa akichelewa kulipa kodi, TRA walikuwa wanakuja na kufunga maduka lakini sasa hivi wameboresha mifumo yao kiasi kwamba tunakumbushwa kwa meseji kwenye simu zetu za mkononi na bado wanatufuata kutupatia elimu na kutukumbusha kulipa kodi kwa wakati, kwakweli TRA wanastahili pongezi, amesema Mhagama.

Naye Advera Katabaruki ambaye ni mfanyabishara wa kufua nguo kwa kutumia mashine mkoani Ruvuma amesema kuwa, kampeni ya elimu kwa mlipakodi imesadia kuwajulisha mambo mengi waliyokuwa hawayajui kama vile utunzaji wa kumbukumbu za biashara, matumizi sahihi ya mashine za EFD pamoja na umuhimu wa kulipa kodi.

“Kampeni hii ya elimu kwa mlipakodi imetufunza mambo mengi sana ambayo tulikuwa hatuyajui kama vile jinsi ya kutunza kumbukumbu zetu za biashara, kutoa risiti sahihi za EFD kwa wateja wetu na sisi kudai risiti tunapokwenda kununua bidhaa kwa wafanyabiashara wakubwa ikiwa ni pamoja na kutukumbusha kulipa kodi kwa wakati, amesema Katabaruki.

Kwa upande wake Klasa Chengula ambaye nae ni mfanyabiashara wa vitambaa mkoani humo, amesema kuwa amefurahia elimu aliyoipata na kuipongeza TRA kwa kubadilika tofauti na zamani kwani wafanyabiashara walikuwa wakiwaogopa hasa kutokana na maofisa hao kutokuwa na ukaribu na walipakodi wao.

“Kiukweli maofisa wa TRA wamejirekebisha sana tofauti na mara ya kwanza ambapo ilikuwa ukipigiwa simu unaitwa TRA mtu ulikuwa unapata mawazo sana lakini hivi sasa TRA haigopeki na wamekuwa marafiki kiasi kwamba wamepita kutupa elimu nzuri ya kodi wala hatujajificha wala kufunga maduka,” amesema Chengula.

Kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkaoni Ruvuma inaendelea kufanyika katika maeneo mbalimba ya mkoa huo ambapo walipakodi wanaelimishwa juu ya haki na wajibu wao, utunzaji wa kumbukumbu za biashara, umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati pamoja na kutoa risiti stahiki za EFD kila wanapouza bidhaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles