Na JUDITH NYANGE,
JESHI la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu watano kwa kupatikana na nyavu za makokoro wilayani Sengerema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika Kijiji na Kata ya Nyarwambo wilayani ya Sengerema.
Alisema watu hao walikamatwa na askari waliokuwa katika doria ambao walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kwamba katika maeneo Kijiji cha Nyarwambo kuna watu wanaojihusisha na uvuvi haramu.
Kamanda Msangi alisema askari waliweza kuwakamata watuhumiwa watano wakiwa na makokoro mawili yakiwa kwenye mtumbwi.
“Watuhumiwa waliokamatwa katika msako huo ni Poneja Mkashi (51) mkazi wa Kijiji cha Ngoma B, Simeo John (23), Mashaka Hitila (17) naDaniel Lucas (25), wote wa Kijiji cha Rubanda, na Turuzira Hitila (35) mkazi wa Kijiji cha Kahumuro,” alisema Kamanda Msangi.
Alisema watuhumiwa wote wanahojiwa na polisi na uchunguzi ukikamalika watafikishwa mahakamani.
Kamanda alisema upelelezi na msako kuwatafuta watu wengine wanaojihusisha na uvuvi haramu katika maeneo yote unaendelea.
Msangi amewataka watu wote wanaojihusisha na shughuli za uvuvi kufanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na serikali.
Ppia amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu mapema waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.