23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

UTAFITI VIASHIRIA VYA UKIMWI WAANZA PWANI

 

 

NA GUSTAPHU HAULE

UTAFITI wa viashiria vya maambukizi ya virusi vya Ukimwi umeanza mkoani Pwani huku kaya zilizoainishwa kufanyiwa utafiti huo zikitakiwa kutoa ushirikiano ili ukamilike kwa wakati.

Meneja Takwimu wa Mkoa wa Pwani, Kalisto Lugome, alikuwa akiwaeleza waandishi wa habari jinsi utafiti huo utakavyotekelezwa.

  Lugome alisema  Mkoa wa Pwani umepata kipaumbele  cha kufanyiwa utafiti huo kutokana na kuwapo idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi yaliyofikia asilimia 7.2 wakati wastani kwa taifa ni asilimia tano.

Alisema utafiti huo utafanyika katika halmashauri zote za mkoa  katika kaya 37 zilizoanishwa.

Lugome alisema hivi  sasa timu ya wahamasishaji  imeanza kupita katika maeneo hayo   kufanya maandalizi.

“Utafiti wa viashiria vya maambukizi ya virusi vya Ukimwi sasa umeingia mkoani kwetu.

“Tunawaomba wananchi katika kaya zilizoanishwa kutoa ushirikiano  kuweza kukamilisha hatua hiyo kwa wakati,” alisema.  

Awali akizindua hatua hiyo,  Mkuu wa Mkoa wa Pwani,   Evarist Ndikilo, alisema   utafiti huo utaisaidia Serikali hususan watunga sera, kuandaa mikakati mipya ya kudhibiti Ukimwi na kuimarisha mipango ya ufuatiliaji.

 Ndikilo alisema takwimu hizo zitasaidia pia kuboresha juhudi zinazofanywa na Serikali kusogeza huduma za VVU katika vituo vya afya ikiwamo huduma ya mama kwenda kwa mtoto.

Hata hivyo,  aliwataka waganga wakuu wa halmashauri hizo   na watendaji wote waweke  mazingira mazuri ya kuhakikisha watafiti hao wanafanya kazi yao kulingana na matakwa ya Serikali.
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles