24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WATANO WAFARIKI KWA AJALI, 13 WAJERUHIWA

Na CLARA MATIMO-MWANZA


WATU watano wamefariki dunia na wengine 13 wamejeruhiwa baada ya gari lenye namba za usajili T 107 BBK Toyota Coaster mali ya Kampuni ya Auki ya jijini Mwanza, kugongana uso kwa uso na gari aina ya Scania lenye namba T 504 BZB likiwa na tela lenye namba T 880 ASA.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema tukio hilo lilitokea Desemba 16 saa 1:30 usiku katika Barabara ya Mwanza-Shinyanga, Kata ya Buhongwa jijini hapa.

Alisema Coaster iliyokuwa ikitokea Katoro mkoani Geita kuja jijini Mwanza, ilikuwa ikiendeshwa na Badru Habibu (33), mkazi wa Nyegezi na Scania hilo lililokuwa likitoka jijini Mwanza kwenda Dar es Salaam, lilikuwa likiendeshwa na Salim Omary (28), mkazi wa Dar es Salaam.

Kamanda Msangi alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa Coaster iliyokuwa imebeba abiria.

Alisema kuwa dereva wa basi hilo dogo, alikuwa akiyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, ndipo aligongana na Scania hilo.

“Hadi sasa kati ya waliofariki ni mwili wa mtu mmoja tu ambao umetambuliwa, marehemu huyo alikuwa anaitwa Abdul Mustafa, anakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 42 na 45. Miili mingine bado haijatambuliwa na ndugu zao.

“Nawaomba wananchi wafike katika Hospitali ya Kanda ya Bugando ili kuitambua miili ya marehemu, maana tumeihifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo. Pia majeruhi wote wapo hapo hapo hospitalini, wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri,” alisema.

Kamanda Msangi alitoa wito kwa waendeshaji wa vyombo vya moto, hususani magari ya  abiria, kuwa makini wawapo barabarani na kuendesha huku wakifuata kanuni, taratibu na sheria za barabarani.

Kutokana na hali hiyo, alisema Jeshi la Polisi linawashikilia madereva wote wawili kwa mahojiano na uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.

“Kama tutabaini mwenye kosa ni mmoja, tutamfikisha mahakamani, lakini endapo wote wawili watakutwa na hatia, basi wote watakwenda mahakamani. Hatuwezi kuendelea kupoteza nguvu kazi ya taifa kutokana na uzembe wa madereva wasiozingatia sheria ya usalama barabarani,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles