24.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

USHAHIDI WA ‘FLASH’ YA NASSARI, LEMA WATUPWA

Na Ratifa Baranyikwa-DAR ES SALAAM


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imesema imeutupa ushahidi wa video uliowasilishwa kwa ‘flash’ na wabunge wawili wa Chadema, Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki na Godbless Lema wa Arusha Mjini, ukiwaonyesha madiwani waliohama chama hicho na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakihongwa rushwa.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili mwishoni mwa wiki, Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba, aliitaja sababu ya kufikia uamuzi huo kuwa ni wabunge hao kuharibu uchunguzi baada ya kuingiza siasa katika jambo hilo.

“Ni kweli ‘flash’ tulikabidhiwa, lakini Nassari na mwenzake kwa sababu walivuruga uchunguzi, hatuwezi kuendelea nalo, unajua pale kilichofanyika ni kuendeleza kufanya siasa kwa sababu uchunguzi lazima uwe huru,” alisema Misalaba.

Alipoulizwa wabunge hao walifanyaje siasa, Misalaba alisema kila walipokuwa wanakwenda Takukuru, walikuwa wanatoa maagizo na walionekana kutokuwa tayari kuukabidhi ushahidi mzima.

“Ilionekana kama sanaa, hawakuwa na utayari wa kutuletea taarifa, walikuwa wanaleta kipande kidogo halafu kesho wanafanya kama mchezo wa Isidingo, kwa hiyo uchunguzi hauendi namna hiyo,” alisema.

Alipoulizwa kwanini wao wasiangalie kile kilichomo ndani ya video walizokabidhiwa hata kama ni kidogo na kukifanyia kazi, alisema mmoja kati ya wabunge hao ambaye hakumtaja jina, alipotakiwa kufika kuwaongezea taarifa hakutokea.

“Ule haukuwa ushahidi, kuna mmojawapo siwezi nikakwambia ni nani, tulimwambia aje kutoa ushahidi, hakuonekana, matokeo yake wakawa wako pembeni  wanaendelea kutoa siri na mikakati nje kwenye vyombo vya habari, kwahiyo tuliwaambia hatuwezi kufanya kazi kwa namna hiyo,” alisisitiza Misalaba.

Gazeti hili lilipomtaka kuweka sawa jambo hilo kwa kuwa kauli yake hiyo inaweza isieleweke vyema kwa jamii, na kuhoji iwapo wameiangalia video hiyo ambayo ndiyo msingi wa kile ambacho Lema na Nassari wanadhani kuwa ndio msingi wa ushahidi wao, alisisitiza juu ya matumizi ya kanuni zinazotumika katika ushahidi na kueleza kuwa video peke yake hazitoshelezi katika ushahidi.

“Sasa unajua kuna kanuni zinatumika katika utoaji wa ushahidi sawa! Video kama zilivyo huwezi kusema ni tayari ushahidi, ile ni taarifa na ushahidi ni tofauti umenielewa?

“Walisema kwamba walisema hiki hapa, lakini sasa walitakiwa waende mbali, huyu mtu anasema kuna hiki kitu asionekane, wewe unasemaje?” alihoji Misalaba.

Akifafanua kwanini hawatumii video peke yake kama ushahidi, Misalaba alisema katika zama hizi za teknolojia, mtu anaweza kuzichezea, hivyo huwezi kusema huo ndio ushahidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles