23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Watangaza nia wachukua fomu za urais

MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliotangaza nia ya kugombea urais, jana wameanza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na chama chao mjini Dodoma.
Kila aliyechukua fomu alikutana na waandishi wa habari nje ya jengo la makao makuu ya CCM na kueleza nini ambacho atawafanyia Watanzania endapo akiteuliwa kupeperusha bendara ya chama chake.

PROFESA MWANDOSYA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, alisema makundi yaliyoibuka ndani ya chama hicho yanaashiria baadhi ya wanachama kupunguza upendo wa chama na kumtukuza mtu.
Profesa Mwandosya ambaye ni Mbunge wa Rungwe Mashariki, aliingia katika viwanja vya Makao Makuu ya CCM mjini hapa saa 4:01 asubuhi, akisindikizwa na mkewe, Lucy Mwandosya, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Hilda Ngoye (CCM) na Mbunge wa Rungwe Magharibi, Profesa David Mwakyusa. Alikabidhiwa fomu hiyo na Mjumbe wa Halmashauri Kuu, Idara ya Oganaizesheni, Dk. Mohammed Seif Khatib.
Alisema makundi yaliyoibuka si ya kisiasa kama yanavyofahamika, isipokuwa yapo kwa ajili ya kumtukuza mtu fulani.
“Haya makundi si ya kisiasa, kuna kundi linalotaka mambo yao yaende haraka, yapo yanayotaka mambo yao yaende kwa kiasi na yapo makundi yanayotaka mambo yaende polepole.
“Lakini mengine ni yale yanayosema ‘nampenda Mwandosya na nitakufa naye’, hii inadhihirisha upendo kwa chama umepungua na kuanza kumtukuza mtu kuliko chama, hakuna mtu mkubwa zaidi ya chama,” alisema Profesa Mwandosya.
Alipoulizwa swali iwapo anao maadui katika siasa, alisema urafiki na uadui hiyo si siasa.
Alisema katika siasa hakuna uadui wala urafiki, lakini yanakuwapo masilahi makubwa ya nchi na chama pamoja na uhusiano wa masilahi yanayofanana.
Aliwaambia wanachama wa CCM waliohudhuria hafla hiyo kuwa mwaka 2005 alipojitokeza kuwania kuteuliwa na chama, walimvisha nishani ya shaba na kusisitiza hiyo kwake ilikuwa si haba.
“Zaidi hapa ni chama, mkumbuke sisi wana CCM tunamchagua atakayekuwa mwenyekiti wetu wa CCM na Mwalimu Julius Nyerere alisema rais anaweza kutoka chama chochote, lakini rais bora atatoka CCM,” alisema.

WASIRA
Naye Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, aliingia katika ukumbi wa Makao Mkuu ya CCM saa 5:15 asubuhi.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Wasira anayefahamika kwa jina la utani la ‘Tyson’, alisema anafikiria kutumia jina hilo katika kampeni zake za urais iwapo litaonekana linafaa.
Mike Tyson ni raia wa Marekani, alikuwa mmoja wa mabondia bora waliowahi kutokea duniani na kupendwa na watu wengi kutokana na kuwashushia kipigo wapinzani wake.
Wasira ambaye ni Mbunge wa Bunda, alisema hayo baada ya kuulizwa swali na MTANZANIA jina hilo lilitokana na nini.
Akijibu, alisema msingi wa jina hilo ni ushindi wa kishindo alioupata katika Jimbo la Bunda miaka yote ambayo amekuwa akigombea.

“Wakati huo ndiyo yule mpiganaji Tyson anawika duniani, niliposhinda wakafananisha na ushindi wa mpiganaji huyo kwani nilimtoa mwenzangu kwa ‘knock out’,” alisema Wasira.
Aliwaambia wana CCM waliohudhuria hafla hiyo kuwa iwapo atateuliwa kuwania nafasi ya urais na kushinda, atahakikisha anaifanya jamii kuchukia ufisadi pamoja na kuwachukia mafisadi.
Alisema iwapo akiulizwa swali atafanya nini kuondoa ufisadi, itakuwa ni sawa na kumwonea kwani hakuwahi kuuonja ufisadi, haupendi ufisadi na haujui.
Hata hivyo, alisema ufisadi na rushwa vinadhoofisha maendeleo na kusisitiza atahakikisha sheria inatumika kupambana navyo.
Alisema iwapo atateuliwa kupeperusha bendera ya CCM na hatimaye kuchaguliwa kuwa rais, ataendeleza pale ambapo Serikali ya awamu ya nne imeishia pamoja na kuendeleza vipaumbele alivyoahidi.

AMINA SALUM ALI
Naye Balozi Amina Salum Ali, amesema endapo akifanikiwa kuwa rais, Serikali yake itaweka kipaumbele cha kukuza uchumi bila kutegemea wafadhili.
Alisema nchi inayotegemea wafadhili haiwezi kuendelea kama ambavyo inatokea sasa.
Balozi Amina, alisema hayo baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama chake mjini hapa jana.
“Endapo chama changu kitaniteua kugombea, naamini nitashinda nafasi hii… nikishinda Serikali yangu itawaalika wafadhili waje wawekeze, si kutupa fedha kwa sababu nchi zote zenye kutegemea wafadhili hazikuendelea.
“Hakuna nchi inayoongozwa bila dira, dira yetu ni kutoka katika uchumi wa tatu kufikia uchumi wa kwanza, huu ndiyo msingi wa maendeleo.
“Kitu kingine ni matumizi, Serikali lazima ibane matumizi, kuanzia sasa tujenge msingi wa kuwa na uchumi imara, tusitegemee wafanyabiashara wanaoenda China watukuzie uchumi, ukitegemea kukuza uchumi kwa njia hiyo Serikali hiyo itaanguka,” alisema.

MAKONGORO NYERERE
Naye Charles Makongoro Nyerere, mtoto wa tano wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, alichukua fomu huku akisema mdhamini wake namba moja ni Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour.
Makongoro, alitoa kauli hiyo jana mjini hapa baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais.
Makongoro alisema amepanga kutembelea nchi nzima kutafuta saini za wadhamini.
Alisema makundi ndani ya chama yamekuwa si ya kiitikadi tena, bali yanachochea uhasama miongoni mwa makada.
“Ndani ya chama kumekuwa na makundi yatokanayo na walarushwa sugu, ukiangalia kwanini wanachukiana utakuta wamezidiana kuiba fedha katika hazina yetu…hawa watu ni sugu kweli kweli, mwenyekiti akiwaonya hawamsikii, wanaendelea kufanya yao,” alisema.
Makongoro alifika katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM saa nane mchana akiwa ameongozana na wapambe wake 10
wakiwamo wazee tisa kutoka Unguja na Pemba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles