24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mpinzani wa Lipumba afukuzwa uanachama

lipumbaNa Aziza Masoud, Dar es Salaam
BARAZA Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), limemvua uanachama mjumbe wake kutoka Mkoa wa Shinyanga, Chifu Lutayosa Yemba.
Chifu Yemba ambaye pia alikuwa ni mpinzani wa Profesa Ibrahim Lipumba katika kuwania uenyekiti wa CUF kwenye uchaguzi uliofanyika mwaka jana, alivuliwa uanachama kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za chama pamoja na kutumia vibaya jina la mwenyekiti wa chama hicho.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho cha Baraza Kuu kilichoanza vikao vyake jana jijini Dar es Salaam, kililiambia MTANZANIA kuwa tuhuma za mjumbe huyo zilifikishwa mbele ya kikao hicho na kufikiwa uamuzi huo.
“Kikao cha Baraza Kuu bado kinaendelea hapa na ajenda kubwa ilikuwa ni tuhuma dhidi ya Chifu Yemba ambaye anadaiwa kutumia jina la Mwenyekiti wa chama kuanzisha Saccos na hata kusababisha chama kudaiwa shilingi milioni 12.
“Lakini pia amekuwa akitumia jina la Mwenyekiti wa chama, Profesa Lipumba katika mradi wake huo binafsi ambao anauendesha na hata kusababisha chama kuingia katika mgogoro hasa katika Mkoa wa Shinyanga,” kilisema chanzo hicho.
Chifu Yemba alipambana na Profesa Lipumba katika uchaguzi wa kuwania nafasi ya uenyekiti ambapo alipata kura 30 huku Lipumba akishinda kwa kura 659 na kufanikiwa kukiongoza tena chama hicho.
Chanzo hicho kilisema baada ya kufikiwa kwa uamuzi wa kuvuliwa uanachama kwa Mjumbe huyo wa Baraza Kuu, alitolewa nje ya ukumbi kwa ulinzi maalumu hadi nje ya geti na kuondoka.
Yemba kwa muda amekuwa haelewani na hata kushambuliana katika mitandao ya kijamii na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya ambaye hivi karibuni alishindwa kura za maoni za kuwania ubunge wa Jimbo la Kinondoni.
Kutokana na kushindwa huko kwa Kambaya, kuliibua hisia mbalimbali miongoni mwa wana CUF hali iliyosababisha baadhi ya kikundi cha watu kuandamana na kwenda Makao Makuu ya CUF kufikisha malalamiko yao kuhusu mwenendo wa uchaguzi Kinondoni.
Alipotafutwa Naibu Mkurugenzi wa Habari wa Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya, alithibitisha kuvuliwa uanachama kwa Chifu Yemba na kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la CUF.
“Ni kweli tumemfukuza uanachama mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Shinyanga kwa tuhuma mbalimbali, tutatoa taarifa rasmi kesho kutwa (kesho) kwa sababu kesho (leo) tunaenda mahakamani,” alisema Kambaya.
Pamoja na kufikiwa kwa uamuzi huo, MTANZANIA lilimtafuta Chifu Yemba ambaye alithibitisha kufukuzwa kwake uanachama ndani ya CUF.
“Tatizo wana shaka na mimi sana, tuhuma zao zote hazina mashiko, katika mashtaka nilikubali moja tu la kutumia nembo ya chama, ni kweli na nikabadilisha sijaelewa jina la Profesa Lipumba nimelitumia vipi, wamepanga kuathiri taasisi na wataniathiri kwa kweli.
“Mimi sina tatizo na CUF, naipenda katika moyo wangu lakini wao hawanipendi na wamefanya maamuzi kikatiba, ila hizi ni hujuma za Kambaya (Abdul) na Sakaya (Magdalena) ambao ndio walipanga kuhakikisha natoka CUF na wamefanikiwa.
“… unajua mimi ni mwanasiasa, natafakari kwa kina hatua za kuchukua baada ya kutokea hili. Na kwa sasa najipanga kuendelea na maisha mengine ya kisiasa nje ya CUF,” alisema Chief Yemba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles