24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Maige awashangaa wagombea urais CCM

maigeNa Khamis Mkotya, Dodoma
MBUNGE wa Msalala, Ezekiel Maige (CCM), amesema amesikitishwa na mwenendo wa wagombea urais kupitia chama chake kwa jinsi wanavyojinadi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari ya Bunge mjini hapa jana, Maige alisema inasikitisha wagombea hao badala ya kujadili hoja wamebaki kushambuliana na kurushiana vijembe.
Alisema kitendo cha wagombea hao kujadili watu badala ya hoja kinaonyesha udhaifu walionao huku akiwataka kuacha siasa za kushambuliana na badala yake waeleze nini watawafanyia Watanzania endapo watapewa hiyo nafasi.
“Ninakerwa na mwenendo wa wagombea urais wa CCM, kwa kweli mtu mzima ukikaa kuwasikiliza jinsi wanavyojinadi unashindwa kuelewa hawa watu wanahubiri sera au mipasho.
“Mfano kuna mgombea mmoja kasema wazi kuwa anataka kukitoa chama mikononi mwa vibaka akirejeshe kwa wazalendo, hiyo maana yake ni nini?
“Maana yake ni kwamba as for now (sasa hivi) chama hiki kipo mikononi mwa vibaka, hii ni kejeli kwa mwenyekiti wetu taifa… ina maana kina Kinana (Katibu Mkuu) ni vibaka?
“Mimi nawashangaa sana, kwanini hawaelezi sera zao wanataka kwenda Ikulu kufanya nini. Wayaseme hayo ili Watanzania wajue dhamira na malengo yao badala yake wamebaki kukanyagana,” alisema.
Maige ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema ni aibu kwa wagombea wanaotoka chama kikubwa kama CCM wanashindwa kutumia busara.
“Kujadili watu badala ya masuala ya msingi ni udhaifu, wewe kama kiongozi eleza nini unataka kuwafanyia Watanzania badala yake unajikita katika kuwasema watu.
“Badala ya kuonyesha uhodari kwamba wanayajuaje matatizo ya Watanzania na vipi watayaondoa, wanaonyeshana umwamba wa kushambuliana, ni aibu.
“Juzi nilimsikiliza Profesa Lipumba (Mwenyekiti wa CUF), alizungumza dhamira na sera zake. Hakuna mahala nilimsikia akiwasema vibaya viongozi wenzake wa Ukawa.
“Kuna watu kule upinzani wanatafuna ruzuku za vyama vyao sikusikia akiwasema; kuna watu kule wanatafuna hadi wake za watu sijamsikia akisema katika Ukawa kuna watu wanatabia mbaya wanakula wake za watu wapuuzeni,” alisema.
Maige aliwataka viongozi wa juu wa CCM kuwakemea wagombea warudi katika mstari kulinda heshima ya chama hicho.
Wagombea waliotangaza nia hadi sasa ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere na Mwanadiplomasia, Balozi Ali Karume.
Wengine waliotangaza juzi ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus Kamani na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles