24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge wamuaga Mwaiposa

NA ARODIA PETER, DODOMA
VILIO na simanzi jana vilitawala katika viwanja vya Bunge mjini hapa wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, Eugen Mwaiposa (CCM).
Mwaiposa (55) alifariki dunia juzi mjini hapa akiwa usingizini nyumbani kwake eneo la Chadulu na chanzo cha kifo hicho kimeelezwa kuwa ni shinikizo la damu.
Shughuli za kuaga mwili huo ziliongozwa na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri Mkuu za zamani, Edward Lowassa, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue na wabunge.
Baadhi ya wabunge walionekana wakishindwa kujizuia wakati wa kuaga mwili huo, na kuangua vilio huku wengine wakionyesha nyuso za huzuni.
Msafara uliokuwa na mwili wa marehemu uliingia katika viwanja vya Bunge saa 6:13 mchana na baadaye Ndugai alitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye yuko njiani kurejea nchini akitokea Geneva, Uswisi kwa shughuli za kikazi.
“Spika ametoa salamu za rambirambi kwa familia na Bunge kwa msiba huu na hivi ninavyoongea yupo njiani anarudi, atafika leo usiku (jana) na kuungana nasi katika msiba,” alisema.
Ndugai alisema baada ya shughuli za kuaga mwili huo, utasafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maziko yatakayofanyika Jumamosi baada ya watoto wawili wa marehemu walioko Canada na Uingereza kuwasili.
“Hatuna neno la kuongeza kwa huzuni tuliyonayo, Eugen alikuwa mbunge wa vitendo, ni mwanamke aliyethubutu,” alisema Ndugai.
Akiongoza sala katika shughuli hiyo, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma, Mshana Samwel, aliwataka wabunge wamtumainie Mungu kwa sababu ndiye kila kitu.
Alisema kwa sasa wabunge wasipoteze matumaini na kuanza kuingia katika njia zisizompendeza Mungu, hasa wakati huu ambapo nchi inaelekea katika Uchgzui Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.
“Wabunge nawaombeni tushushe presha, sisi watumishi wa Mungu tupo nanyi tunawabeba katika maombi, tusipoteze matumaini, tuwe wajasiri na tumwangalie Mungu ingawa michakato katika kipindi hiki ni mingi, shusheni presha, hata wanaotangaza nia tusiache imani zetu.
“Mwalimu Nyerere aliwahi kusema heshima ya mtu inapatikana kutokana na huduma yake katika jamii, na sisi ni muda wetu sasa kuwachapa na kama hukutoa huduma yako sawasawa ndiyo mwanzo wa kukimbilia kwa sangoma,” alisema Mchungaji Mshana na kusababisha kicheko.
Mwili wa marehemu Mwaiposa ulisafirishwa jana kwa ndege kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya mazishi.

RAMBIRAMBI
Akitoa salamu za Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama, alisema msiba huo ni pigo kubwa, kwani hawajasahau machugu ya kuondokewa na aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Mashariki, John Komba.
“Tutamkumbuka Eugen kwa kuwa alikuwa mstari wa mbele kupigania wapigakura wake. Tunaweza kusema alikuwa jembe imara Ukonga na alikuwa akitekeleza ilani ya chama vizuri.
“Juzi tulikuwa naye na alikuja kuomba kuchangia, hii inaonyesha jinsi alivyokuwa akiwapigania wapigakura wake…alikuwa rafiki wa wabunge wote na kila mtu alimwita Dear,” alisema Mhagama.

LISSU
Akisoma salamu kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mnadhimu Mkuu wa kambi hiyo, Tundu Lissu alimwelezea marehemu Mwaiposa kuwa alikuwa ni aina ya wabunge wanawake jasiri na wa kipekee waliogombea katika majimbo na kushinda.
“Kifo kimetutenganisha na aina ya wabunge wa kipekee kabisa, alikuwa jasiri aliyeweza kuongoza Jimbo la Ukonga lenye wapigakura wengi katika Jiji la Dar es Salaam la kiuchumi na kisiasa. Ni mfano wa Mtume Paul, alipigana vita vizuri na kumaliza kazi yake,” alisema Lissu.

ANNA ABDALLAH
Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG), Anna Abdallah, alisema Mwaiposa ni mbunge wa pili mwanamke kufariki dunia katika Bunge hilo. Wa kwanza ni aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Regia Mtema (Chadema) aliyefariki kwa ajali ya gari Januari 4, 2012.
Anna alimwelezea marehemu kuwa alikuwa mpambanaji, jasiri, na aliyelijua vyema jimbo lake na wapigakura wake.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Hamis Kigwangala, alisema kamati yake imepoteza mmoja wa wajumbe wake tegemeo ambaye alifanya kazi yake bila kuchoka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles