23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Watakiona

Print*Dk. Magufuli: Siku zao zinahesabika

*Lowassa asema akiingia Ikulu hataki mchezo

 

Bakari Kimwanga, Kigoma na Maregesi Paul, Bariadi

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema iwapo atachaguliwa kuwa rais, atahakikisha anakomesha vitendo mbalimbali vya kihalifu nchini ukiwamo ujambazi.

Mgombea huyo pia ametoa onyo kwa watu wasioitakia mema Tanzania wanaoingiza nchini silaha haramu na kusema kuwa siku zao zinahesabika.

Wakati Dk. Magufuli akitoa onyo hilo, naye mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa ametoa kauli inayofanana na hiyo akisema iwapo ataingia Ikulu atajenga Tanzania mpya, kwani hataki mchezo.

Dk. Magufuli, alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana, alipokuwa akihutubia mikutano ya kampeni iliyofanyika wilaya za Buhigwe, Kasulu na Kibondo.

 

Katika mikutano hiyo, Magufuli alisema watu hao waovu hutoka nchi za jirani baadhi yao wamekuwa wakishirikiana na Watanzania waliokosa uzalendo kwa taifa lao.

Alisema watu hao huteka magari pamoja na kuua raia wasiokuwa na hatia, jambo ambalo alisema kamwe hatolivumilia katika serikali yake.

Alisema moja ya kazi atakayoifanya endapo akichaguliwa kuwa rais, ni kuhakikisha anakomesha vitendo vya uhalifu vinavyoharibu sifa ya taifa.

Alisema anashangazwa na matukio ya uhalifu katika mikoa ya Kigoma, Kagera na Katavi, hali inayolazimu askari polisi kuwa na kazi ya kusindikiza mabasi kila siku.

“Kigoma ipo jirani na Burundi, kuna watu ambao si wema huingia nchini wakiwa na silaha na mabomu…cha kusikitisha wanashirikiana na Watanzania wenzetu na hufanya matukio mabaya ya uhalifu.

“Kutokana na hofu ya usalama sasa polisi wamekuwa na kazi ya kusindikiza mabasi…wakati wana kazi nyingine za kufanya. Nasema siku zao zinahesabika, Serikali ya Magufuli itakomesha mambo haya.

“…ndio maana CCM  katika ilani yetu ya uchaguzi, imesema italinda amani amani amani… hata akija rais mwingine kupitia CCM naye atalinda amani,” alisema Dk. Magufuli.

“Tunahitaji amani, ole wenu mnaoingia Tanzania na mabomu yenu , nawaambia yaacheni hukohuko,” alifoka Dk. Magufuli

Aliwaonya watu wanaoingia nchini kutoka nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na Rwanda kuacha kuingiza silaha nchini.

“Nawaomba  ndugu zangu, Serikali ya awamu ya tano itaimarisha uhusiano na nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla,”alisema.

 

Atambia lugha

Dk. Magufuli  ambaye kabla ya kuanza kuomba kura huanza kwa kuwasalimia wananchi kwa lugha mbalimbali, jana alifanya hivyo na kuamsha shangwe.

Alisema suala la yeye kuanza na salamu, halina uhusiano na masuala ya ukabila.

“Lugha ninazoongea si kwamba naendeleza ukabila… jamani Watanzania wote watakuwa wangu katika Serikali yangu,” alisema.

Akizungumzia mikakati ya Serikali yake, alisema elimu ya msingi hadi kidato cha nne itakuwa bure sambamba na kuondoa michango ya kero kwa wazazi.

“Kodi zote za kero tutaziondoa pamoja na kumaliza mgogoro wa Msitu wa Kagera Nkhanda, ambao wananchi wanahitaji eneo kwa ajili ya kilimo,” alisema.

 

Edwad Lowassa

Naye mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, amesema atakapoingia madarakani atajenga Tanzania mpya kwa sababu hataki mchezo.

Amesema kwamba, pamoja na umasikini unaowakabili Watanzania, Serikali yake itaondoa hali hiyo kwa kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi za kukabiliana na umasikini huo.

Lowassa aliyasema hayo mjini Bariadi jana alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Halmashauri Jimbo la Bariadi Magharibi, ambalo mbunge wake aliyemaliza muda ni Andrew Chenge (CCM).

“Rais wa Marekani Barack Obama alipokuwa akiomba kura kwa Wamarekani, aliwauliza can we (tunaweza?), nao wakamjibu, yes we can (ndiyo tunaweza).

“Kwa hiyo na mimi nawaambia tunaweza, nikiingia madarakani nitaijenga Tanzania mpya ili aliyekuwa na  gari moja awe na magari mawili, aliyekuwa na baiskeli moja awe nazo kumi na aliyekuwa na boda boda moja, awe nazo ishirini.

“Katika nchi yetu, tuna rasilimali nyingi na kama tukizitumia vizuri, kila mmoja ataishi maisha mazuri kwani chini ya Serikali yangu, elimu itatolewa bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.

“Nawahakikishieni michango yote mashuleni itaondolewa, yaani mtoto wako atakayefaulu darasa la saba mwaka huu, atakapoingia fomu one mwakani hatalipa chochote.

“Hata baada ya kuapishwa, ushuru wote wa mazao utakoma, wakulima watakuwa huru kwenda kuuza mazao yao popote, atakayetaka kuuza mazao yake, Rwanda, aende, atakayetaka kuuza Kenya, Uganda au kwingineko ni shauri yake, apeleke tu.

“Nawaahidi kwamba, nitaunda Serikali ya maendeleo sitaki mchezo, nipeni kura kwa sababu kazi hiyo naiweza na ninatosha,” alisema Lowassa.

Pamoja na hayo, mgombea urais huyo aliwasisitizia Watanzania watunze shahada zao za kupigia kura ili waweze kuzitumia Oktoba 25 mwaka huu, kumpigia kura yeye pamoja na wagombea wote wa Ukawa.

Akizungumzia sekta ya maji, Lowassa alisema Serikali yake itafanya kila liwezekanalo kufikisha maji ya ziwa victoria katika mji wa Bariadi kama alivyofanya kwa kusafirisha maji ya ziwa victoria kutoka Mwanza hadi Shinyanga.

SUMAYE

Naye waziri mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, alipokuwa akiwahutubia wananchi hao, alisema kama Watanzania wanataka maisha bora, lazima waiondoe CCM madarakani kwa kuwa ndiyo iliyowasababishia maisha magumu.

Pamoja na hayo, alisema CCM ni kama mtumbwi uliotoboka na kuingia maji na kwamba ili waliomo waweze kuokoa maisha yao, njia pekee ni kushuka katika mtumbwi huo kabla haujazama.

“Tusipoiondoa CCM marakani kamwe hatutapata maisha bora Tanzania. Hebu angalieni, mnalima pamba kila mwaka lakini haiwanufaishi.

“Wakati wao wameshindwa kuwasaidia kupitia pamba, Serikali ya Ukawa itaimarisha kilimo, Serikali ya ukawa itaimarisha huduma za afya hospitalini tofauti na sasa ambapo huduma za afya ni mbovu.

“Nyie mliobaki huko CCM, kumbukeni Mwalimu Nyerere aliwahi kusema CCM siyo mama yake, sasa wewe unayeng’ang’ania huko unataka kuniambia unaijua vizuri CCM kuliko Mwalimu Nyerere?

“Serikali ya CCM imejaa mafisadi ambao kila siku wanamtukana Mzee Lowassa na pia ufisadi umejaa katika Wizara ya Ujenzi anayoiongoza Magufuli (Dk. John Magufuli, mgombea urais wa CCM).

“CCM maji hayako tena shingoni bali sasa maji yamewafika puani, hawana jipya tena na ndiyo maana hata Magufuli kwenye mabango yake ameandika Chagua Magufuli badala ya Chagua CCM,” alisema Sumaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles