28.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Majimbo yawavuruga Ukawa

NA JONAS MUSHI NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

HALI si shwari ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) baada ya Chama cha NCCR-Mageuzi kuibuka na madai kuwa kuna vyama washirika vinavuruga umoja huo, na kwamba chama chao kinaweza kufa baada ya uchaguzi mkuu.

Ukawa ni umoja unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD ambavyo vimekubaliana kuungana katika uchaguzi mkuu na kusimamisha mgombea mmoja kwenye urais, ubunge na udiwani.

Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Landmark Hotel jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti Bara wa chama hicho, Leticia Mosore na Katibu Mkuu wake, Mosena Nyabambe walisema hali hiyo inatokana na kukiukwa makubaliano mbal imbali yaliyofanywa na viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa.

“NCCR Mageuzi tulijitoa muhanga kweli kwa kukubali kuwaacha watu wetu ili tu tujenge Ukawa iliyotakiwa, lakini sasa tumegundua Chadema wanafanya mambo yao kivyao,” alisema Nyabambe na kuongeza kuwa hali hiyo imewapa shaka kuwa huenda chama chao kitakufa baada ya uchaguzi.

Alisema tangu chama hicho kijiunge Ukawa, kimeendelea kudhoofika tofauti na lengo la umoja huo ambalo lilikuwa ni kuimarisha vyama vyote.

“Uchaguzi wa 2010 tulisimamisha wagombea katika majimbo 67, lakini sasa hivi tumepewa majimbo 12 tu…yaani tumerudishwa nyuma sana,” alisema.

Nyambabe alisema Chadema wamekuwa wakiwafanyia fujo kuliko wanavyofanyiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo hata majimbo hayo waliyopewa bado wamewaingilia kwa kusimamisha wagombea wao katika majimbo sita kinyume cha makubaliano.

Aliyataja majimbo hayo kuwa ni Korogwe Mjini, Manyovu, Kasulu Mjini, Kasulu Vijijini, Kigoma Mjini na Kigoma Vijijini.

Hata hivyo, Nyambabe alisema msimamo wa chama chao ni kuendelea kubaki Ukawa ili kuiondoa madarakani CCM na kuwataka viongozi wa umoja huo kukutana na kurekebisha kasoro hizo.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti, Mosore, alisema Ukawa ilianza kukiuka makubaliano ya ushirikiano wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, na sasa wanakiuka makubaliano ya Jangwani, waraka wa uteuzi wa madiwani na waraka wa makubaliano juu ya wagombea ubunge ambayo yote yalisainiwa na viongozi wa Ukawa.

Alimtupia lawama Mwenyekiti wao James Mbatia kuwa amekuwa msemaji wa Chadema, huku akikisahau chama chake na kukiacha kikidhoofika.

Kutokana na hali hiyo, Mosore alitoa ushauri kwa mwenyekiti huyo kuacha kuisemea Chadema na kuwa wanamtaka ahitishe vikao vya kikatiba kujadili masuala hayo.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu kuwapo kwa baraka za Mwenyekiti Mbatia, katika kutoa malalamiko hayo pamoja na kujadili suala hilo ndani ya chama, Katibu Mkuu, Nyambabe, alionekana kujiumauma na kushindwa kutoa jibu la moja kwa moja kwa kudai kuwa suala hilo linahusu Ukawa na si la chama.

“Kuhusu baraka za mwenyekiti, naomba mwelewe suala hili tunailalamikia Ukawa na wala si chama chetu, na ndani ya chama tumejadili mara nyingi na mwenyekiti,” alisema Nyambabe japo alishindwa kuelezea msimamo wa mwenyekiti wake katika majadiliano hayo.

 

WAHUNI

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu kauli za viongozi hao, Msemaji wa NCCR-Mageuzi, Florian Rutayuga, alisema hazina baraka ya mwenyekiti wao, Mbatia aliyesaini makubaliano ya Ukawa kwa niaba ya chama, hivyo waliojitokeza mbele ya waandishi wa habari, wachukuliwe kama wahuni.

“Hao wahesabiwe kama wahuni, msemaji mkuu wa chama ni mwenyekiti, na yeye ndiye aliyesaini makubaliano baina ya viongozi wa Ukawa, anajua nani anapaswa kupata jimbo gani, kungekuwa na matatizo angesema,” alisema Rutayuga.

Alisema kwa utaratibu wa chama chao, baada ya mashauriano na Halmashauri Kuu ya chama, mwenyekiti ndiye mwenye mamlaka ya kuzungumza.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema NCCR Mageuzi inapaswa kufuata taratibu za kuwakilisha malalamiko kwa kuanzia katika vikao vya ndani ya chama chao.

“Mambo ya NCCR yanapaswa yatatuliwe ndani ya chama, wana fursa ya kuyazungumza katika vikao vyao na baadaye wakakutana katika vikao vya Ukawa yatajadiliwa, hakuna jambo ndani ya Ukawa linashindikana, likija tutalitatua,” alisema Makene.

Mwingiliano wa wagombea ubunge wa umoja huo umekuwa ukijitokeza katika maeneo mbalimbali nchini ambapo katika Jimbo la Mtwara mjini mgombea mwenza wa urais chadema alimtangaza mgombea ubunge wa Cuf badala ya yule wa NCCR aliyepitishwa na Ukawa na kuzua vurugu.

Juzi akiwa Nzega, Duni alilazimika kuwaomba wananchi wa Jimbo la Nzega Vijijini kumchagua Dk. Khamis Kigwangala wa CCM baada ya kumkataa mgombea wa CUF aliyepitishwa na Ukawa na kumtaka wa Chadema.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles