Na Clara Matimo, Mwanza
Watafiti wa mazao ya uvuvi wametakiwa kutoa matokeo yenye tija yatakayowawezesha wananchi kunufaika na masoko ya nje ya nchi.
Wito huo umetolewa jijini hapa Aprili 19,2023 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Adam Malima alipomwakilisha kwenye ufunguzi wa warsha ya wadau wa mazao ya uvuvi iliyolenga kupokea na kupitisha taarifa ya utafiti kuhusu upotevu wa mazao ya uvuvi nchini.
Amesema ingawa kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2020 umeonesha kiwango cha uvuvi wa dagaa kiko juu kwa asilimia 45 ukilinganishwa na sangara ambao una asilimia 33 lakini haujawa na tija ya kuinua kipato cha wananchi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa soko la uhakika.
“Lazima tujiulize kwa nini uvuvi wa dagaa hauna tija kubwa hivyo tunahitaji watafiti wa mazao ya uvuvi mfanye utafiti mje na suluhisho ili dagaa zinazovuliwa ziandaliwe kisasa katika hatua zote kuanzia zonapovuliwa hadi zinapoingizwa sokoni twende na wakati ili dagaa zetu ziwe bora zikidhi vigezo vya soko la kimataifa ili ziinue uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Hata hivyo naipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kwa kufanya utafiti huo wa mwaka 2020 hasa katika mazao ya dagaa hivyo ni matumaini yangu kwamba utapunguza changamoto zilizopo au kuzimaliza kabisa,” amesema Elikana
Kaimu Mkurugenzi wa TAFIRI, Hilary Mroso amebainisha kwamba kwa ya kuimarisha mnyororo wa thamani kwa kusimamia njia zote bora na za kisasa kwa mazao ya uvuvi ili kulinda usalama wa mazao hayo baharini na kwenye maziwa.
“Tutaendelea kufanya utafiti kama huo ili kuhakikisha taifa linakuwa salama kwa chakula na wananchi kwa ujumla, tunashukuru nchi yetu kupata nafasi ya kuteuliwa na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO)kufanya utafiti.
“FAO limeziteua nchi tatu ikiwemo Tanzania, Sri Lanka na Colombia kutoka mabara matatu ya Afrika, Asia na Latin Amerika kuhusika na utafiti wa upotevu wa mazao ya uvuvi kwa lengo la kupata ufumbuzi, nini kifanyike na kuwepo mikakati endelevu ya usalama wa mazao hayo kwa udhamini wa Serikali ya Norway,” amesema Mroso.
Kwa mujibu wa Mroso utafiti huo umefanyika Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria na Nyasa.