24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Watafiti dawa za binadamu kuongezeka

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Tafiti kuhusu dawa zinazotumiwa na binadamu zinatarajiwa kuongezeka kutokana na kuwepo kwa mikakati ya kuwajengea uwezo wafamasia na wataalam wengine wa afya katika nchi za Afrika Mashariki.

Profesa Omary Minzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mafunzo ya kuwajengea uwezo wafamasia na wataalam wengine katika kupima ubora wa dawa. Kushoto ni baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo.

Mafunzo ya hivi karibuni kwa wataalam wa nchi sita za Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia na Rwanda ni mkakati mmojawapo wa kuwajengea uwezo katika kupima ubora na ufanisi wa dawa zilizopo na zitakazogunduliwa.

Mafunzo hayo yaliandaliwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Taasisi inayosimamia na kujenga uwezo katika kufanya tafiti za afya Afrika Mashariki (EACCR) na Taasisi ya Utafiti ya Kilimanjaro (KCRI) kwa ufadhili wa EDCTP.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Mratibu Mkuu wa Mafunzo EACCR, Profesa Reginald Kavishe, amesema bado kuna uhaba wa watafiti katika eneo hilo.

“Watafiti wa dawa za binadamu wapo lakini hawatoshelezi ndiyo maana baada ya kubaini kuna upungufu tukaandaa mafunzo haya.

“Zinapofanyika tafiti zinazohusiana na dawa mara nyingi kwenye maabara zetu kwa kuwa wataalam hawapo wa kutosha unakuta sampuli zinapelekwa nje ya nchi kwenda kufanyiwa upimaji, sasa tunataka zisipelekwe tena nje watu wawe na weledi huo wawe wanapima kwenye nchi zao,” amesema Profesa Kavishe.

Amewataka wataalam hao wanaporudi katika maeneo yao ya kazi kuwafundisha wenzao na kuendeleza tafiti kwa kupima dawa zinazotumika kujua ubora wake na kuhakikisha matumizi ya dawa yanakuwa sahihi.

Naye Mratibu wa mafunzo hayo ambaye pia ni Mhadhiri kutoka MUHAS, Profesa Omary Minzi, amesema washiriki hao wamejifunza kubaini namna dawa zinavyonyambulika mwilini ili kuhakikisha zinatibu na kutoka vyema kwa watu ambao wana matatizo mbalimbali kama ya ini na figo.

“Baadhi ya dawa kama ini na figo vina matatizo zinaweza zisitolewe kwa kiasi kinachotakiwa au zikachelewa kutoka, sasa ikichekewa kutoka ukanywa nyingine na ile ya mwanzo ilikuwemo zinarundikana mwishowe zinakuwa sumu.

“Elimu hiyo tumeitoa kuelezana namna ya mgonjwa mwenye figo mbovu au ini bovu apewe dozi gani ili naye apone…mfano mgonjwa anaumwa kifafa lakini figo au ini lake bovu, tukimpa dozi kama ya mtu ambaye hana matatizo hayo itamletea shida,” amesema.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Dk. Kenneth Byashalira kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kifua Kikuu Kibong’oto, amesema wamekuwa wakiwapa wagonjwa wa TB dawa kwa viwango sawa lakini tafiti zimeonyesha wanaokuwa na magonjwa zaidi ya mawili dawa inayofika kwenye eneo la kutibu kifua kikuu ni ndogo ikilinganishwa na anayekuwa na TB peke yake.

“Tukipima damu kwa mtu mwenye magonjwa mawili itatuwezesha kujua kiwango gani cha dawa kimemfikia, kwenye eneo la kutibu itatusaidia vilevile kuweza kuongeza ili aendane sawa na yule mwenye ugonjwa mmoja,” amesema Dk. Byashalira.

Mshiriki mwingine kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Kenya (KIMR), Kennedy Ogweno, amesema; “Tumejifunza vitu vingi kinadharia na kivitendo na kwa kuwa nafanya kazi katika taasisi ya utafiti ambayo pia inachunguza dawa za aina mbalimbali itatusaidia.

EACCR inaratibu mafunzo katika nchi sita za Afrika Mashariki yaani Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia na Rwanda ambapo hutoa mafunzo ya Shahada ya Uzamivu, Shahada ya Uzamili na kozi fupi za kujenga uwezo katika kufanya tafiti za afya.

Kwa kipindi cha 2017 – 2021 zaidi ya washiriki wa kozi fupi 200 wamepatiwa mafunzo, Shahada ya Uzamivu (watano) na Shahada ya Uzamili (26).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles