25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TMDA yakamata dawa za wizi za Sh milioni 4.8 Kaliua

Na Allan Vicent, Tabora

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Magharibi imemkamata Mfanyabiashara, Zakayo Bagomwa mkazi wa Ulyankulu wilayani Kaliua mkoani Tabora anayemiliki duka la dawa baridi la Maliza na Yesu kwa tuhuma za kuuza dawa za wizi na zilizopigwa marufuku na serikali.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Magharibi, Christopher Migoha amesema mtuhumiwa amekamatwa hivi karibuni na Maofisa wa Mamlaka hiyo baada ya kupata taarifa za siri na kwenda kufanya ukaguzi wa kina katika duka lake na kubaini uwepo wa dawa hizo zinazouzwa kinyume na sheria.

Amesema mtuhumiwa amefunguliwa mashtaka katika Kituo Kikuu cha Polisi cha wilaya ya Kaliua na kupewa jalada namba ULY/IR/162/2021 ambapo jumla ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi vilivyokamatwa vilikuwa na jumla ya sh mil 4.869.

Amefafanua kuwa mtuhumiwa alikuwa anafanya biashara hiyo ya duka la dawa baridi katika Kijiji cha Kanindo, Kata ya Kanindo, Tarafa ya Ulyankulu wilayani Kaliua Mkoani Tabora ambapo alikutwa na dawa za wizi, zilizokwisha muda wake na zisizoruhusiwa kuuzwa kisheria.

Aidha, alibainika kuwa alikutwa akiuza dawa za kifua kikuu (TB) na kadi za kliniki za kina mama wajawazito, kutoa huduma za matibabu ndani ya duka, kuuza vifaa tiba ambavyo ni mali ya Serikali ya Tanzania na dawa kutoka Kenya ambazo hazipaswi kuuzwa nchini ikiwemo dawa zinazotolewa bure na serikali kwa wagonjwa.  

Migoha alieleza kuwa walikuta dawa na vitendanishi vya kupimia Virusi vya Ukimwi na malaria ambavyo ni mali ya Serikali ya Tanzania vikiwa vimehifadhiwa na kutunzwa kwa ajili ya kuuzwa kinyume cha Kifungu cha 312(1) cha Kanuni ya Adhabu Sura 16.

Aliongeza kuwa kulikuwa na dawa zisizosajiliwa kutumika nchini zikiwa zimehifadhiwa na kuuzwa kinyume cha Sheria ikiwemo dawa zisizoruhusiwa kuuzwa katika maduka ya watu binafsi kinyume cha kanuni ya 63 ya Makundi ya Dawa ya Mwaka 2015.

Meneja alibainisha katika ukaguzi wao walikuta dawa zilizokwisha muda wa matumizi zikiwa zimetunzwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuuzwa kinyume na Kifungu cha 75(1) cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura 219.

Alisema mmiliki hakuweza kuwasilisha risiti za manunuzi wala mauzo ya dawa zote alizokutwa nazo kinyume cha Kanuni za Uendeshaji wa Biashara ya Dawa za Binadamu.

Aidha aliongeza kuwa walikuta vifaa tiba vya kufanyia tohara vikiwa vimetunzwa katika duka hilo kinyume cha sheria pamoja na dawa za wangojwa wa kifuu kikuu ambazo hazikustahili kuwepo ndani ya duka hilo wala kuuzwa kwenye maduka ya dawa muhimu.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara wote wa bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi kufanyabiashara zao kwa kuzingatia Sheria ya Dawa na Vifaa tiba Sura 219 pamoja na Sheria zingine zilizowekwa, kinyume na hapo TMDA haitawavumilia wale wote watakaokiuka sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles