24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

WASOMI, WAFANYABISHARA WAMPONGEZA KENYATTA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta, kuruhusu wananchi wa bara la Afrika kuingia na kufanya biashara Kenya kwa kutumia kitambulisho imepokelewa kwa mitizamo tofauti.

Juzi baada ya kuapishwa, Rais Kenyatta alitangaza kuwa kuanzia sasa mtu yeyote anaweza kwenda Kenya kuishi, kufanya kazi, kumiliki mali, kulima, kuoa au kuolewa.

Watu mbalimbali wakiwamo wasomi na wafanyabiashara wamejadili uamuzi huo kwa kuupinga na kuupongeza.

Baadhi ya wachambuzi wanautazama uamuzi huo kama hatua ya kutaka kuharakisha makubaliano ya Shirikisho la Afrika Mashariki (EAC).

PROFESA MPANGALA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alichokifanya Rais Kenyatta ni kutaka kuharakisha makubaliano ya EAC.

“Naiangalia hatua hii kwa mitizamo miwili, kwanza anataka kuharakisha makubaliano ya EAC kwa kuzipa presha nchi zingine zifanye hivyo,” alisema Profesa Mpangala.

PROFESA WANGWE

Mtaalamu wa masuala ya uchumi nchini, Profesa Samuel Wangwe, alisema uamuzi wa Kenyatta ni mzuri lakini akatahadharisha kabla ya nchi zingine kufungua milango ni lazima zijipange kwanza.

“Ni wazo zuri lakini utekelezaji wake lazima uangaliwe kama kweli uko wazi. Kama wenyewe kwa wenyewe wanafungiana milango halafu wanafungua kwa wengine hapo lazima kuwe na alama ya kuuliza.

“Ukienda Kenya huwezi kukuta ardhi haina mtu na hata ukitaka kwenda kununua kwa mtu huwezi hivyo unaona wao tayari wamejipanga,” alisema Profesa Wangwe.

 

BANA

Mhadhiri wa Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema uamuzi huo ni mzuri na utaendeleza utengamano kwa wananchi wa Afrika Mashariki.

“Alichokifanya Kenyatta ni kizuri na kitaimarisha uhusiano baina ya Kenya na nchi wanachama wa shirikisho hilo. Na sisi wengine tuige tuache kufungia wananchi wetu kwenye maboksi,” alisema Dk. Bana.

JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA

Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini (JWT), Johnson Minja, alisema watakaa na kuangalia namna watakavyoweza kuitumia fursa hiyo.

“Hatua hii itafungua fursa ya watu kuweza kufanya biashara, sisi pia tutakutana ili kuona jinsi tutakavyoitumia fursa hii,” alisema Minja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles