26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

DAKTARI: HOMA YA INI HATARI ZAIDI YA UKIMWI  

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


WATU wanane kati ya 100 nchini wana maambukizi ya virusi vya homa ya ini (Hepatit B), ambavyo vinatajwa kuwa hatari zaidi ya virusi vya Ukimwi (VVU).

Uwezekano wa mtu kupata maambukizi ya virusi vya homa ya ini ikiwa atajamiiana na mtu mwenye virusi hivyo, ni mara 10 zaidi ikilinganishwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), John Rwegasha, alisema hayo jana alipozungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu.

“Homa ya ini ni hatari, na njia za maambukizi ni kama zile za maambukizi ya VVU na ikiwa mtu hatapata matibabu mapema, huweza kuvisambaza virusi hivi kwa kasi kubwa mno kwa wengine,” alisema.

Daktari huyo ambaye ni miongoni mwa wataalamu saba wa hospitali hiyo wanaoondoka kwenda nchini India kujifunza jinsi ya kufanya upasuaji na upandikizaji wa ini, alisema wanaume ndio kundi ambalo lipo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo kuliko wanawake.

“Ni kundi ambalo lipo kwenye ‘risk’ kubwa, kulingana na takwimu zetu hapa hospitalini, kati ya wagonjwa wanaolazwa wodini tunaowatibu magonjwa ya ini, asilimia 60 ni wanaume na 40 ni wanawake,” alibainisha.

Alisema hiyo inatokana na baadhi ya wanaume kuwa na tabia hatarishi zinazowasababisha kupata magonjwa hayo, ikiwa ni pamoja na unywaji pombe, hasa zile zisizothibitishwa ubora wake.

“Baadhi ya wanaume wana tabia ya kuwa na mahusiano na wanawake zaidi ya mmoja, ni hatari, ikiwa anakutana na ambaye ana maambukizi ya virusi hivi, basi hupata maambukizi hayo,” alibainisha.

Alisema katika kitengo hicho, asilimia 60 ya wagonjwa wamepata matatizo ya ini kutokana na kupata maambukizi ya virusi vya homa ya ini.

Akizungumzia hali ya ugonjwa huo nchini, Dk. Rwegasha ambaye pia ni mkuu wa kitengo hicho, alisema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania imepewa kiwango cha asilimia tano cha maambukizi.

“Tunacho kiwango cha kitaifa pia, ambacho ni asilimia tano hadi 17 na kuna makundi ambayo yapo kwenye hatari ya kupata maambukizi, wakiwamo wenye VVU ambao kiwango chao ni asilimia 17, wajawazito asilimia tano,” alisema.

Aliongeza: “Makundi mengine ambayo tunapendekeza wapewe chanjo ili kudhibiti kiwango cha maambukizi ni wanaojidunga dawa za kulevya, wanaofanya biashara ya ngono na mengineyo.

“Duniani takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kati ya watu bilioni mbili waliogundulika na kutibiwa virusi vya homa ya ini, 450 bado wanaishi navyo duniani.”

Alisema kwa mujibu wa WHO kila mwaka watu milioni 1.5 hufariki dunia kwa maambukizi ya virusi vya homa ya ini na kila mwaka kunagundulika kesi mpya milioni nne za watu wenye virusi hivi.

Alisema tafiti zinaonyesha asilimia 60 hadi 80 ya saratani ya ini zinazogundulika duniani huwa zimetokana na maambukizi ya virusi hivyo.

“Changamoto tunayoiona ni wakati unatibu wagonjwa, bado kunajitokeza maambukizi mapya, vifo na kuna makundi ya watu ambayo huwa ni ‘carrier’ (wabebaji) wa virusi hivi ambao huvisambaza kwa kasi kwa wengine,” alisema.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa MNH, Aminiel Aligaesha, jopo la wataalamu linalokwenda India, lina madaktari bingwa wanne wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, wauguzi wawili wanaosimamia mifumo ya hadubini na mhandisi wa vifaa tiba anayesimamia mitambo ya hadubini.

Alisema mafunzo hayo yatachukua miezi mitatu na wataalamu hao watarejea nchini wiki ya kwanza ya mwezi Machi, mwakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles