24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

BWANA VITA AJIUA KWA SUMU MAHAKAMANI

THE HAGUE, UHOLANZI


KIKAO cha kusikiliza rufaa iliyowasilishwa na washtakiwa wa uhalifu wa kivita mjini The Hague, Uholanzi kilisitishwa ghafla jana baada ya mmoja wa washtakiwa, Slobodan Praljak, kudaiwa kunywa sumu baada ya kusikiliza hukumu.

Praljak (72), alikuwa mmoja wa viongozi sita wa zamani wa kisiasa na wa kijeshi wa Bosnia wenye asili ya Croatia, ambao walikuwa wanasikiliza uamuzi wa mwisho wa rufaa uliokuwa ukitolewa na Mahakama Maalumu ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia uhalifu uliofanyika Yugoslavia (ICTY) nchini hapa.

Vyombo vya habari vya Croatia, vinasema mshtakiwa huyo alifariki dunia, lakini mahakama hiyo ya UN ilisema haiwezi kuthibitisha mara moja taarifa hizo.

Alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 20 mwaka 2013 kwa makosa ya uhalifu wa kivita yaliyotekelezwa katika mji wa Mostar.

Baada ya kusikiliza hukumu kuwa majaji wamepitisha kifungo hicho, alimwambia jaji, ‘nakunywa sumu, mimi si mhalifu wa kivita’ huku washtakiwa wenzake wakimwangalia bila kuamini kinachotokea.

Uhalifu huo wa kivita unatokana na vita ya mwaka 1992-95 baina ya Wacroatia wa Bosnia na Waislamu.

Praljak alisimama na akainua mkono wake hadi kwenye kinywa chake, kisha akainamisha kichwa chake nyuma na kuonekana kunywa kitu kutoka katika kichupa kidogo.

Jaji Mwandamizi Carmel Agius, mara moja alisitisha shughuli na gari la kuwabeba wagonjwa likaitwa.

“Sawa,” alisema Jaji Agius na kuendelea: “Tunaahirisha, pazia tafadhali, usiondoe kichupa ambacho amekitumia alipokunywa kitu.”

Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kutoka The Hague, Anna Holligan, alisema kuwa kabla ya pazia kurejeshwa, ukumbi wa mahakama ulionekana kujawa na mkanganyiko.

Gari la kuwabeba wagonjwa lilifika baadaye nje ya ukumbi, huku helikopta ikiruka juu angani na wafanyakazi kadhaa wa uokoaji kuingia ukumbini na vifaa vyao.

Zaidi ya saa moja baada ya tukio hilo, mlinzi mmoja aliliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa Praljak alikuwa bado anatibiwa, lakini baadaye taarifa za vyombo vya habari zilisema amefariki dunia.

Praljak, anadaiwa kutochukua hatua zozote akiwa kamanda wa wahudumu wakuu wa Jeshi la Walinzi wa Wacroatia wa Bosnia (HVO) wakati walipokuwa wakiwakamata Waislamu majira ya joto mwaka 1993.

Aidha hakuchukua hatua hata baada ya kupewa taarifa kuwa mauaji yalikuwa yamepangwa, na mashambulio dhidi ya wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa na kuharibiwa kwa daraja la kale la mji wa Mostar na misikiti.

Mahakama hiyo, ambayo iliundwa 1993, itamaliza kazi  yake mwisho wa mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles