PATRICIA KIMELEMETA NA AZIZA MASOUD
WAKATI Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akitoa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 ya Sh trilioni 31.6, ilihali ile ya Sh trilioni 29.5 ya mwaka 2016/17 ikiwa haijatekelezeka, wadau wametoa maoni tofauti, wengi wakisema bajeti iliyopita ilitawaliwa na siasa.
Wamesema pia mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2017/18 yaliyotolewa mbele ya wabunge juzi yanatia wasiwasi kutokana na vipaumbele vyake kujielekeza kwenye miradi ya ujenzi huku ile inayogusa wananchi walio wengi, ikiwamo elimu, maji, kilimo, afya na nishati vikiachwa nyuma.
Baadhi ya vipaumbele vya bajeti hii ni pamoja na mradi wa kuendeleza miradi ya makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma cha Liganga – Njombe, ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge), kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATC), ujenzi wa mitambo ya kusindika gesi kimiminika, Lindi na uendelezaji wa maeneo maaalum ya kiuchumi.
Taarifa ya Dk. Mpango iliyotolewa juzi, inaonyesha katika mwaka 2017/18, Serikali inapanga kutumia Sh trilioni 31.69 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.
Katika bajeti hiyo, Sh trilioni 19.70 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, kati yake Sh trilioni 7.20 ni za mishahara Sh trilioni 9.46 ni za kulipia deni la Taifa.
Matumizi mengineyo (OC) yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 3.03 ambapo Sh trilioni 2.08 ni matumizi yaliyolindwa na Sh bilioni 274.9 ni matumizi yanayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.
Matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh trilioni 11.99 ambapo kiasi cha Sh trilioni 8.96 ni fedha za ndani na Sh trilioni 3.02 ni fedha za nje.
Wakati katika mwaka ujao wa fedha serikikali ikipanga kutumia Sh trilioni 11.99 kwa ajili ya shugguli za maendeleo, katika bajeti iliyokamilisha miezi mitatu kumalizika, kati ya Sh trilioni 11.82 zilizopangwa kutumika kwa shughuli za maendeleo, mpaka Februari mwaka huu, ni Sh trilioni 4.168 sawa na asilimia 35.26 ya lengo ndizo zimetolewa.
Ni kutokana na hali hiyo baadhi ya wadau wanaona bajeti ya mwaka 2017/18 ambayo imeizidi ile ya mwaka 2016/17 kwa Sh trilioni 2.1, kama ya kisiasa na isiyotekelezeka.
Maoni ya wadau
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema hatua ya Serikali kushindwa kutekeleza bajeti ya 2016/2017 imetokana na uwepo wa matumizi mabaya yaliyokuwa yakifanyika kwa amri za kisiasa.
Alisema viongozi wa serikali walikuwa wakijisahau na kufanya uamuzi katika masuala ya fedha kwa vitu ambavyo hata havikuwapo katika mpangilio wa bajeti.
“Bajeti iliyopita haikutekelezeka kwa sababu matumizi hayakuwa mazuri, vitu kama ununuzi wa ndege, kuhamia Dodoma vimegharamu fedha na vyote hivyo havikuwapo kwenye bajeti maamuzi yalifanyika kisiasa, namna hiyo ya utumiaji siyo nzuri”alisema Profesa Mpangala.
Alisema matumizi ya maendeleo yanahitaji mipango ambayo itafuata utaratibu na endapo kunakuwa na jambo jipya nje ya bajeti viongozi wanapaswa kuwa na utaratibu wa kusubiri ili waweze kutekeleza mwaka unaofuata.
Pia alisema kuna umuhimu wa Taifa kuondokana na kutegemea fedha za nje kwani wengi wa wahisani wamekuwa wakiahidi bila kutekeleza ahadi zao.
“Kwa sasa kuna umuhumi wa kuondoa utegemezi, tukiamua tunaweza mfano nchi ya Kenya imeshafikia uko, bajeti nzima inataekelezwa kwa vyanzo vya ndani hakuna fedha za kutoka nje ,”alisema Profesa Mpangala.
Mbali na hilo Profesa Mkandala pia alibainisha wasiwasi wake katika mwelekeo wa bajeti ya 2017/18 ambayo imejikita zaidi katika masuala ya ujenzi wa miundombinu.
Alisema suala hilo ni la msingi hasa katika serikali ya awamu ya tano ambayo inahubiri masuala ya viwanda lakini kulikuwa na haja ya kuweka kipaumbele cha mikakati upatikanaji wa umeme wa uhakika na malighafi za kutenegenezea bidhaa za viwanda.
“Miundombinu ni kitu cha msingi katika serikali ya viwanda,viwanda vinahitaji miundombinu isiyoteteleka ili viweze kusimama,”alisema Profesa Mpangala.
Alisema mbali na viwanda serikali pia ilipaswa iweke kipamumbele katika masuala ya umeme ambao ndiyo msingi wa uzalishaji katika viwanda pamoja na malighafi za kutengenezea bidhaa.
“Nilivyosoma sijaona suala la umeme, viwanda vinahitaji umeme wa uhakika sasa sijui serikali ina mpango gani katika hilo, lakini pia kila mara narudia suala moja kwamba viwanda vyetu pia vinategemea sana malighafi ya nje kunahaja ya kuweka mkazo katika suala la kilimo ambacho hakijatajwa wala kugusiwa kabisa,”alisema Profesa Mpangala.
Alisema katika bajeti zilizopita ni serikali ya awamu ya nne ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete pekee iliyokuwa na sera za kilimo japokuwa haikuwa na mikakati mizuri ya utekelezaji.
Dk. Bana
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) Dk. Benson Bana alisema tangu enzi za mkoloni serikali ya Tanzania haijawahi kuwa na bajeti inayokidhi matakwa ya kifedha kwa asilimia 100.
Alisema miaka wote, wamekuwa wakipanga bajeti kwa makadirio huku wakiangalia vipaumbele vinavyoigusa wananchi moja kwa moja, zikiwamo huduma za jamii.
“Ukiangalia mfano kwenye bajeti ya miundombinu,reli ya kisasa, ununuzi wa ndege na kadhalika, wamepangiwa bajeti kubwa kuliko kwenye huduma za jamii ikiwamo elimu,afya, maji na kilimo,”alisema Dk.Bana.
Aliongeza, katika sekta ya elimu, mpaka sasa bado kuna matatizo, jambo ambalo limechangia kuzorota kwa utoaji wa elimu.
Alisema serikali ingeongeza bajeti ili kuhakikisha kuwa, fedha zinazotolewa zinatumika kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu, vitendea kazi, mishahara, kupanda kwa madaraja na mambo mengineyo, jambo ambalo lingechangia kukua kwa utoajia wa elimu nchini.
Alisema, kwa upande wa afya, mpaka sasa serikali haijaboresha mazingira bora ya utoaji wa huduma hiyo, jambo ambalo limechangia kutokuwepo kwa vitendea kazi, mazingira mabovu,ukosefu wa dawa na mengine katika vituo vya utoaji wa huduma hiyo.
Akizungumzia suala la kilimo Dk.Bana alisema mpaka sasa, idadi kubwa ya wakulima nchini bado wanatumia zana duni za kilimo ikiwamo jembe la mkono pamoja na kusubiri mvua za msimu.
Alisema, kutokana na hali hiyo, serikali ilipaswa kuelekeza bajeti kwenye maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa, wakulima wanaondoka kwenye mazingira duni ya kilimo, wanatumia zana za kisasa, mbegu bora, wanaingia kwenye kilimo cha umwagiliaji ili waweze kupiga hatua za kimaendeleo.
Alisema, kwa upande wa sekta ya maji, serikali imeshindwa kuongeza bajeti kwa ajili ya usambazaji wa huduma bora za maji mijini na vijijini, na kusababishwa wananchi kuhangaika wakitafuta huduma hiyo kwenye maeneo mbalimbali.
“Serikali ilipaswa kuhakikisha kuwa, bajeti inayotengwa kwa ajili ya huduma za jamii inaongezeka ili kuhakikisha kuwa, mawaziri wa wizara hiyo wanatekeleza bajeti hiyo ipasavyo,kwa mfumo huu tunaweza kupunguza malalamiko ya wananchi,”alisema Dk.Bana.
Alisema kitendo cha bajeti ya mwaka huu wa fedha imejikita kwenye miundombinu ya usafirishaji, ikiwamo reli ya kisasa ya ‘standard gauge’ na ununuzi wa ndege ambao pia kinaweza kuchochea maendeleo kwa namna moja au nyingine.
Akizungumzia kuhusiana na fedha za wahisani, Dk Bana amesema kuwa, serikali inapaswa kuongea vizuri na wahisani kwa sababu fedha za ndani haziwezi kukidhi mahitaji.
Alisema, kuna miradi ya kijamii ambayo inahitaji fedha hizo ili iweze kutekelezwa, hivyo basi serikali inapaswa kukaa pamoja na wahisani ili kuangalia namna ya kusaidia kwenye miradi hiyo.
“Wahisani wanatusaidia kwenye miradi mbalimbali ya kijamii, serikali inapaswa kukaa nao meza moja ili kuangalia namna ya kutatua kero zilizopo ili waweze kutoa fedha hizo ambazo zitatusaidia kuboresha miradi mbalimbali ya kimaendeleo,”alisema Dk.Bana.
Alisema, licha ya kukaa nao serikali pia inapaswa kuwapa msimamo wa kutojihusisha na masuala ya ndani ya nchi ikiwamo mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar .
“Wahisani hawawezi kuingilia migogoro ya ndani ya kisiasa hata kama wanatusaidia, hayo ni mambo yetu na kwamba tunaweza kuyatatua wenyewe bila ya kuwashirikisha, kutokana na hali hiyo, serikali inapaswa kuweka msimamo katika hilo,”alisema.
Prof. Semboja
Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Uchumi, Prof. Hajji Semboja alisema , bajeti ya mwaka huu ni nzuri na kwamba imejikita kwenye usafirishaji kuliko shughuli za kijamii zinazowagusa wananchi.
Alisema, kiasi cha fedha zilizotengwa kwenye miradi ya maendeleo ya sekta ya afya, elimu, kilimo na maji ni ndogo kuliko kwenye sekta ya usfairishaji.
“Huduma za jamii zinawagusa wananchi moja kwa moja, hivyo basi serikali ilipaswa kuliangalia suala hilo wakati wa upangaji wa bajeti, jambo ambalo lingeweza kupunguza matatizo yaliyopo,”alisema Semboja.
Bashiru Ally
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Bashiru Ally amesema kuwa, suala la bajeti ni kubwa ambalo linahitaji muda wa kukaa kwa ajili ya kuipitia na kuijadili, jambo ambalo linaweza kusaidia kuiboresha.
“Huwezi kuzungumzia suala la bajeti kwa uwepesi katika mazingira kama haya, linahitaji mjadala mpana ili tuweze kuijadili na kuchambua kipengele kwa kipengele, kutokana na hali hiyo, ngoja tuisome kwanza halafu tutakuwa na maneno ya kuzungumza,”alisema.
Bisimba
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk Hellen Kijo-Bisimba amesema kuwa, serikali ya sasa imejikita kwenye miundombinu huku wakishindwa kuangalia huduma za jamii zinazowagusa wananchi.
Akitolea mfano wa tetemeko la Kagera lililotokea hivi karibuni ambapo, fedha za msaada zilizotolewa na wahisani mbalimbali zimepelekwa kujengwa miundombinu huku wananchi wakishindwa kupata huduma bora za afya, elimu na maji.
Alisema, kutokana na hali hiyo, serikali inapaswa kubadili mtazamo na kuangalia huduma za jamii zinazowagusa wananchi moja kwa moja halafu ndiyo waangalie kuhusu miundombinu.
“Ikiwa wananchi watapata huduma bora za afya, elimu, maji na sekta ya kilimo kuboreshwa, mambo ya miundombinu yakiwamo usafiri wa reli ndege na madini yatakuja yenyewe,”alisema Kijo-Bisimba.
Aliongeza, huwezi kujenga reli, barabara, kununua ndege au kuimarisha madini wakati wananchi wana njaa, hivyo basi walipaswa kuangalia vipaumbele muhimu ambavyo vinawagusa wananchi kwa ujumla wake, kwa sababu watakaopanda ndege au treni ni wachache kuliko watakaokwenda hospitali kupatiwa matibabu.
Kauli za wabunge
Mbunge wa Nzega Mjini, Husein Bashe (CCM) alishangazwa na kutoona suala la kilimo katika mpango huo wa maendeleo wakati kukiwa na sera ya Tanzania ya viwanda.
“Bado sioni kilimo ambacho ndio msingi wa viwanda katika haya makabrasha, malengo ni yaleyale naamini hii ni bajeti kutokana na fedha za ndani vipi kutoka nje,’’ alihoji Bashe.
Bashe aliipongeza Serikali kwa kuweza kukusanya mapato kwa zaidi ya asilimia 90.
Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Act Wzalendo), alishangazwa na miradi inayohusu wananchi kutopewa kipaumbele.
Zitto alisema utekelezaji wa bajeti unaonesha kwamba hautafikiwa kutokana na kushindwa kufikisha malengo ya mwaka 2016-2017.
“Sh trilioni 29 tulishindwa leo unasema Shilingi Trilioni 31 itawezekana wapi ni jambo ambalo haliwezekani bajeti haina uhalisia hata kidogo.
“Mapato ya ndani sawa je ya nje hatukopesheki kwa sasa sababu ya mambo fulani yanayoendelea.
“Ukubwa wa riba ni tatizo masoko ya kimataifa sasa hivi hatukopesheki na ndio maana serikali inashindwa kukopeshwa,sababu ya riba ni bajeti ndio imesomwa ila haina mwelekeo’’alisema.
Naye Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) alisema wamechoka kuona katika machapisho huku wanaohusika wakishindwa kuyatimiza yale yaliyoandikwa.
“Hayo ni maandishi tu hakuna kitu hakuna kilichowahi kutekelezwa hata haya ni mbwembwe tu’’ alisema.
Naye Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba(CCM), alimpongeza Waziri wa Fedha na Mpango, Dk. Philip Mpango, kwa kuwasilisha mapendekezo mazuri.
“Haya ni mapendekezo mazuri lakini ni lazima Serikali iyatekeleze lakini tukiishia katika maneno tu haitakuwa jambo zuri lakini narudia tena ni mapendekezo mazuri’’ alisema.