NAIROBI, KENYA
WASIWASI wa makabiliano baina ya NASA na polisi jijini Nairobi Jumanne ijayo umetanda baada ya muungano huo kuapa kuendelea na mipango ya kumwapisha Raila Odinga katika Uwanja wa Uhuru, licha ya Serikali kutangaza hautumiki.
Kundi linalojiita Jamii ya Wafanyabiashara Nairobi, pia limetangaza litatumia uwanja huo siku hiyo kwa shughuli ya tohara kwa vijana wa mitaani bila malipo.
Ofisa Mkuu Mtendaji wa NASA, Norman Magaya, alisisitiza jana kuwa shughuli ya kiapo itaendelea katika uwanja huo kama ilivyopangwa.
Akihojiwa na televisheni za hapa, Magaya alisisitiza kuwa NASA ilituma maombi kwa Serikali ya Kaunti ya Nairobi kutaka kutumia uwanja huo na walipaswa kulipa ada jana.
“Tunajua Gavana Mike Sonko ameshauriwa na chama chake cha Jubilee kuufunga uwanja huu ilhali tulifuata sheria kutuma ombi rasmi. Hatutabadili mipango yetu,” alisisitiza Magaya.
Kwenye ilani iliyochapishwa magazetini juzi, Serikali ya Kaunti ya Nairobi ilitangaza kuufunga kwa muda uwanja huo kutoa nafasi ya kukarabati sehemu kadhaa zinazotumiwa na wananchi kustarehe.
Ilani iliyotiwa saini na Kaimu Katibu wa kaunti hiyo, Leboo ole Morintat, ilisema wananchi hawataruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara katika uwanja huo kuanzia Januari 23, 2018.
Lakini Magaya aliwashauri wafuasi wa NASA wakaidi marufuku hiyo na kujitokeza kwa wingi kuhudhuria hafla hiyo aliyosema itaanza saa mbili asubuhi.
Aidha Kamanda Mkuu wa Vuguvugu la National Resistance Movement (NRM), Miguna Miguna, pia alishikilia uzi huo huo akiwataka wafuasi wa NASA kujitokeza bila woga.
“Uwanja wa Uhuru Park ni mali ya umma. Haumikiliwi na Jubilee wala NASA. Kwa hivyo, hakuna mtu mwenye mamlaka ya kutuzuia kukutana hapo kwa sherehe rasmi ya kumwapisha kiongozi wetu Raila Odinga na naibu wake Kalonzo Musyoka,” Miguna aliwaambia wanahabari katika ofisi za Okoa Kenya, Nairobi jana.