23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wasira: Sina hakika na utafiti wa Makonda

stephen wasiraNa Elizabeth Hombo, Dar es Salaam
MWANASIASA mkongwe aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, Stephen Wasira, amesema hana uhakika kama mpango wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, wa usafiri bure kwa walimu unaweza kufanikiwa.
Wasira alikuwa akizungumzia mpango huo wa Makonda wa usafiri bure katika daladala kwa walimu wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam.
Aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na Mtanzania nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es Salaam, hivi karibuni.
Hata hivyo, baadaye viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwamo wanasiasa na wenye vyombo vya usafiri wakiwamo wamiliki wa daladala; walikutana na kuamua utaratibu huo uwahusishe walimu wote wa mkoa huo.
Kwa mujibu wa mpango huo unaotarajiwa kuanza Jumatatu ijayo na kuzihusisha wilaya zote za Kinondoni, Temeke na Ilala, walimu watapatiwa vitambulisho maalumu vyenye saini ya Makonda.
Katika mahojiano hayo, Wasira alisema hawezi kueleza zaidi kwa kuwa hajafanya utafiti kuhusu suala hilo.
Pia alisema kitendo cha kutengeneza vitambulisho hivyo na kuweka saini ya mkuu huyo wa Wilaya ya Kinondoni itakuwa ni gharama.
“Bado sijajua Makonda kafanya utafiti gani…lakini kwa akili ya kawaida sina hakika.
“Ingekuwa ni mpango wa nchi nzima ningeelewa kwa sababu lazima ungewashirikisha wadau wote wa elimu,”alisema.
Kada huyo mkongwe wa Chama Chama Mapinduzi (CCM), alisema walimu wamekuwa wakidai stahili zao nyingi kwa muda mrefu hivyo ni bora wangeboreshewa kwanza mahitaji yao muhimu.
“Hata serikali ya awamu ya nne ilijitahidi kuwalipa stahiki zao, wengine walipata mikopo lakini bado asilimia kubwa hawajapata.
“Hivyo ni bora wangeboreshewa stahiki na mishahara yao nadhani ingesaidia.
“Lakini Makonda ni kijana mdogo na damu yake inakimbia hivyo anaweza akafanya uamuzi na baadaye ukawa siyo sahihi…lakini ngoja tuone,”alisema Wasira aliyekuwa waziri katika kipindi chote cha miaka 10 ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.
Uamuzi huo wa Makonda pia umekwisha kupingwa na walimu na wadau mbalimbali wa elimu wakisema unawadhalilisha walimu.
Wanasema jambo lililo muhimu ni kuwaboreshea mishahara yao na mahitaji mengine.
Jana gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA) lilimnukuu Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia, akipinga mpango huo akisema utawashushia heshima walimu.
Aliitaka Manispaa ya Kinondoni kuweka utaratibu wa kuwaongozea walimu fedha za usafiri kwenye mishahara yao ili wajilipie wenyewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles