27.9 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wasira amshangaa Makamba

wasira*Asema huenda alibebwa tano bora ya urais CCM
Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam
MWANASIASA mkongwe aliyekuwa waziri katika Serikali ya awamu nne, Stephen Wasira, amemshangaa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba aliposema kuwa uwajibikaji katika utawala wa awamu ya nne ulikuwa ni wa kuleana.
Kauli ya Wasira imekuja siku moja baada ya gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA) kumnukuu Makamba akisema uwajibikaji katika Serikali ya awamu hiyo haukuwa wa kuridhisha kwasababu kulikuwa na utamaduni wa kuoneana haya, kujuana na kusitiriana.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu yaliyofanyika nyumbani kwake Mbezi jijini Dar es Salaam jana, Wasira alieleza kushangazwa na kauli hiyo ya Makamba akisema yawezekana aliyelelewa ni yeye.
“Labda alilelewa yeye…kama rafiki yangu Makamba anasema kulikuwa na kuleana, mimi kwa upande wangu sikulelewa nilifanya kazi na nikatimiza wajibu wangu kama nilivyopewa na Rais.
“Sasa kama aliona kulikuwa kuna kuleana mimi sijui yeye ndiye anajua maana mimi sikulelewa. Kama unafanya makosa halafu unaachwa huondolewi hapo ni kuleana.
“Na yeye inawezekana alilelewa maana kuna watu wanasema kuingia kwake tano bora ya urais alipendelewa labda huko ndio kulelewa ndio maana akasema hivyo,”alisema Wasira.
KASI YA MAGUFULI
Wasira ambaye aliongoza kamati iliyoandaa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, alisema kasi ya utumbuaji majipu aliyoanza nayo Rais Dk. John Magufuli ipo katika ilani ya chama hicho tawala na kwamba walipanga hivyo.
Mwanasiasa huyo ambaye alikuwa waziri katika kipindi chote cha miaka 10 ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, alisema si kweli kama ambavyo baadhi ya watu wanasema kwamba Serikali ya awamu ya nne haikufanya kitu, bali ilikuwa ikitumbua majipu kwa mtindo wa kimya kimya.
Alisema kila awamu inayoingia madarakani inakuwa na mtindo wake wa kufanya kazi na kwamba ni vigumu kulinganisha na awamu nyingine.
“Kila kiongozi ana ‘style’ yake, huwezi kulinganisha wakati wa Magufuli na Nyerere, Mwinyi, Mkapa au Kikwete hawa ni watu ‘individuals’ kila mtu ana mtazamo wake wa kuongoza na kila mtu ana ilani kwa wakati wake.
“ Wengine mara wanasema hatukuwa na Serikali awamu iliyopita wakidai kwamba haikufanya kitu, si kweli kabisa, Serikali ilikuwepo, lakini ili concentrate (kujielekeza) kwenye nini…lazima tufanye tathimini. Kila Serikali ina mazuri na mabaya.
“Ukitaka kufanya tathimini unawezaje kusema Jakaya Kikwete hakufanya kitu? Wakati alijenga shule nyingi za kata, barabara zilizojengwa wakati Magufuli akiwa waziri wa ujenzi hazikuwa zake bali ni mpango wa Serikali ya awamu ya Kikwete.
“Hakuna Serikali iliyo perfect (kamilika)na huku inaongozwa na wanadamu. Kila Serikali ina style yake na awamu ya nne ilikuwa ya kimya kimya kama nilivyoeleza. Ilifanya vizuri, mengine haijafanya sana na mengine haikufanya kabisa.
“Ukifanya uchunguzi Serikali zote utakuta kuna mazuri na mabaya. Mwalimu Nyerere alikuwa anaipenda Tanzania na Watanzania kutoka moyoni mwake na alikuwa tayari kufanya kazi bila kulipwa na wakati anastaafu akasema chukueni mambo mazuri tuliyofanya, mabaya acheni…hapo aliona kabisa Serikali haikuweza kutimiza yote,”alisema Wasira.
Kutokana na hilo, Wasira alisema popote duniani hakuna Serikali ambayo inaweza ikafanya kila kitu kwasababu hakuna binadamu aliye malaika.
“Hakuna Serikali itakayofanya kila kitu hata Magufuli ataacha mengine na mwingine atayakuta. Hakuna Serikali inayoongozwa na malaika bali inaongozwa na wanadamu. Kuendesha nchi si jambo dogo kwasababu ina mambo mengi.
“Matatizo ya bandari yalikuwepo na si kwamba yameisha. Mfano hivi sasa wamebadili jina la rushwa kuwa posho…kwa hiyo hivi sasa wamegeuza rushwa kuwa posho.
“Kwa kasi hii sasa wafanyakazi watarudi nyuma na kufanya kazi kwa nidhamu zaidi, lakini vichwa maji nao watatumia ‘style’ nyingine tu kama hiyo ya kugeuza rushwa kuwa posho,”alisema Wasira.
UTEUZI WA CCM
Wasira ambaye alikuwa miongoni mwa wanachama wa CCM waliojitokeza kutaka kuteuliwa na chama hicho kuwania urais, akizungumzia uteuzi huo alisema hakukuwa na namna kwasababu waliojitokeza walikuwa wengi.
“Walikuwepo watu 38 waliochukua fomu na kurudisha, wakateuliwa watano si kwamba walikata majina bali waliteua. Kanuni ya CCM ndiyo inasema hivyo sasa hivi hata nikisema haki haikutendeka itasaidia nini wakati uchaguzi ulishapita?
“Kanuni ya chama haisemi lazima waitwe ndio wahojiwe bali Kamati Kuu inajadili jina moja moja… kwa kuwa mimi sikuwepo ndani ya kikao hicho sijui kama nilijadiliwa… sielewi.
“Lakini nilisikitika kama binadamu na sikufanya chochote zaidi ya kusikitika maana ndio utaratibu wa chama inawataka watano,”alisema mwanasiasa huyo.
ZANZIBAR
Akizugumzia kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar, Wasira alikishauri Chama cha Wananchi (CUF) kikubali kushiriki uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 20, mwaka huu kwasababu wapiga kura ni wale wale.
Alisema amani ya Zanzibar ipo mikononi mwa Wazanzibari kwa kushiriki uchaguzi huo.
“Ili kuwe na amani Zazinzibar CUF waende kwenye uchaguzi kwasababu wapiga kura ni walewale, kama wanajua walishinda hofu yao nini?…hata wakirudia watashinda.
“Ushauri wangu kwa Wazanzibari wasaidie katika kuleta amani, wapige kura…wanaoipigia CUF au CCM na vyama vingine wafanye hivyo halafu kura zihesabiwe mshindi atangazwe kwa sababu hakuna namna kwa vile Mwenyekiti wa ZEC alisema uchaguzi uliopita ulikuwa na kasoro,”alisema.
JIMBO
Wasira ambaye alikuwa Mbunge wa Bunda kwa muda mrefu, akielezea kuhusu namna alivyoshindwa na upinzani katika uchaguzi wa mwaka jana katika jimbo hilo, alisema uchaguzi huo haukuwa wa huru na haki.
“Uchaguzi ule uligubikwa na corruption (rushwa), ulikuwa na kasoro nyingi sana…hakukuwa na uchaguzi pale, lakini kwa kuwa bado suala hili liko mahakamani tuliache kwanza,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles