23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mdee: Watake wasitake Dar wataachia

Halima MdeeNa Kulwa Mzee, Dar es Salaam
MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), amesema sasa umefika wakati kwa polisi kuacha kutumika, huku akituma salamu kwa viongozi wa CCM, akisema watake wasitake wataachia Jiji la Dar es Salaam liongozwe na Ukawa. Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwake, muda mfupi baada ya kuachiwa kwa dhamana. Alidai kitendo cha kuwekwa ndani hakitawazuia kufanya kazi zao, na pia alilitaka Jeshi la Polisi kufuata taaluma za kazi zao kwa kuwa kufanya kazi kwa kufuata maagizo ni upuuzi. “Kosa hili ni la kipuuzi, polisi waache kutumika,” alidai na kuongeza kwamba Rais Dk. John Magufuli ajiandae kuongozwa na Ukawa atake asitake kwa sababu namba hazidanganyi. Jana Mdee pamoja na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shitaka la kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam (RAS), Theresia Mmbando. Halima (37), Waitara (40) na mfanyabiashara Rafii Juma (21) pamoja na Diwani wa Kata ya Kimara, Ephrein Kinyafu (33), walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi. Kabla ya kusomewa mashtaka, mawakili wa Serikali, Faraja Nchimbi, akishirikana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi na wakili mwingine wa Serikali, Mwanaamina Kombakono, waliiomba mahakama kutoa hati ya wito kwa mshtakiwa wa nne Diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema (56) ili aweze kusomewa shtaka Mwanaamina alidai washtakiwa hao walitenda kosa hilo, Februari 26, mwaka huu katika Ukumbi wa Karimjee wilayani Ilala, Dar es Salaam. Ilidaiwa washtakiwa hao walimjeruhi Theresia na kumsababishia majeraha. Washtakiwa hao walikana mashtaka, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa. Mdee na wenzake walikuwa wakiwakilishwa na jopo la mawakili likiongozwa na Wakili Peter Kibatala. Wengine ni John Mallya, Fredrick Kiwelo, Hekima na Omary Msemo. Kibatala aliiomba mahakama kuwapatia dhamana washtakiwa kwa masharti nafuu ikilinganishwa na kosa lenyewe. Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Shaidi alisema kila mshtakiwa atajidhamini mwenyewe na kutia saini ya dhamana ya Sh milioni mbili. Alisema hati ya wito wa kufika mahakamani kwa mshtakiwa Njema itolewe. Mdee na wenzake walitimiza masharti hayo ya dhamana na kuachiwa hadi Machi 16, mwaka huu kesi itakapotajwa. Jana, viongozi wa Chadema na baadhi ya wanachama walifurika mahakamani hapo kwa ajili ya kufuatilia kesi hiyo. Baada ya kuachiwa kwa dhamana, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, Mdee na Waitara walizungumza na watu waliokuwapo mahakamani hapo. Mwalimu alionya kwamba Serikali isithubutu wala kujidanganya kwamba itawaweka watu wao ndani ili waweze kuitisha mkutano wa Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam ambao umekwama kufanyika mara tatu kutokana na mvutano uliopo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles