24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kupigwa marufuku mitumba kwazua taharuki

Pg 1Na Waandishi Wetu

WAKATI viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wanaokutana jijini Arusha wakipiga marufuku uingizwaji wa nguo za mitumba, kumekuwa na maoni tofauti miongoni mwa wananchi, huku wengine wakipongeza uamuzi huo na wengine wakipinga. Viongozi waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Rais Dk.

John Magufuli wa Tanzania, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Rais Paul Kagame wa Rwanda.

Marufuku hiyo ni moja ya hatua zilizopendekezwa katika kuinua viwanda vya nguo katika kanda ya Afrika Mashariki. Nguo za mitumba ni tegemo kubwa kwa wananchi wenye kipato kidogo, kutokana na bei yake nafuu huku zikitoa ajira kwa maelfu ya wachuuzi.

Serikali za Afrika Mashariki zimekuwa zikilaumu uagizaji wa nguo na viatu vilivyokwisha kutumika kama moja ya sababu zinazofanya viwanda vya ndani kusambaratika. Mbali na nguo za mitumba, viongozi hao watajadili pendekezo la kupunguza kiasi cha magari yaliyotumika yanayoingizwa katika kanda hiyo, lengo likiwa kusaidia viwanda vya utengenezaji magari vinavyoendesha biashara Afrika Mashariki.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, baadhi ya wataalamu wa uchumi wamekuwa na maoni tofauti kwa hatua hiyo.

Mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphrey Moshi alisema kilichoua viwanda ni sera mbovu na kuitaka Serikali kutoa muda wa kutosha kwa viwanda kuzalisha nguo mbadala wa mitumba.

“Kwanza watumiaji wengi wa nguo za mitumba wanasema nguo hizo ni bei nafuu na ni imara kuliko nguo au bidhaa za viwandani. Tujiulize, kwani mitumba ndiyo imeua viwanda? “Sera zetu ndiyo zimeua viwanda; kwa mfano awali sera ilisema viwanda ni mali ya umma, ikafika mahali Serikali ikashindwa kuviendesha, vikatolewa kwa sekta binafsi ambayo inataka faida nayo ikashindwa kutokana na mazingira yaliyopo,” alisema Profesa Moshi.

Alitaja sababu nyingine ya kufa kwa viwanda kuwa ni miundombinu mibovu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa umeme na maji huku akisema Serikali ijenge kwanza mazingira mazuri ya viwanda kabla ya kufuta mitumba.

“Watakaoumia ni wananchi kwa sababu inauzwa kwa bei nafuu. Serikali iweke muda wa angalau miaka miwili ya kujipanga na viwanda vizalishe kwa ushindani, kabla ya kufuta mitumba.

“Tutengeneze sera na tuone muda wa kutosha kuzitekeleza. Sekta binafsi haiwezi kuzalisha bila kuwa na sera nzuri,” alisema Profesa Moshi. Dk. Mashindano Naye mtafiti mwandamizi wa Taasisi ya Uchumi na Jamii (ESRF), Dk. Oswald Mashindano, alisema licha ya kuwaumiza wananachi wa kipato cha chini, lakini itakuja kuleta faida siku za usoni.

“Mwanzo utakuwa mgumu kwa wananchi wa kipato cha chini kwa sababu mitumba inauzwa bei nafuu.

Itabidi wanunue nguo mpya kwa bei ya juu. Lakini itakuja kuwa na manufaa makubwa kiuchumi kwa sababu katika mizania ya kibiashara Tanzania itakuwa inanunua bidhaa chache kutoka nje ya nchi na kuuza nje bidhaa nyingi,” alisema Dk. Mashindano. Alisema tatizo kubwa la Tanzania ni kukosa mifumo bora ya ukusanyaji kodi hivyo kudhibiti bidhaa kama mitumba kutazuia ukwepaji wa kodi na kulinda viwanda vya ndani.

“Uingizwaji holela wa bidhaa kutoka nje unawapa mwanya wafanyabiashara wengi kukwepa kodi. Wakishaingiza bidhaa wanauza kwa bei nafuu kwa sababu hawalipi kodi. Lakini wenye viwanda wanalazimika kuuza kwa bei ya juu kwa sababu wanalipa kodi, hivyo viwanda vitakufa,” alisema Dk. Mashindano. Kamote Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Utetezi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Hussein Kamote alisema uamuzi huo ni sahihi kwa sababu nguo za mitumba zinaathiri viwanda vya nguo vya ndani.

“Nguo za mitumba zina athari kubwa kwa viwanda vyetu. Pamoja na kwamba hatuna viwanda vingi vya nguo kama vile mashati, suruali na nyinginezo, bado wawekezaji wanahofia kujenga viwanda kwa sababu ya nguo za mitumba. “Unapotaka kuwekeza kwanza unaangalia soko.

Siyo nguo tu, tuna ngozi nyingi lakini hakuna viwanda vya viatu kwa sababu kuna mitumba ya viatu,” alisema Kamote. Kamote aliitaka Serikali pia kuweka mazingira wezeshi kibiashara ili kuwezesha wenye viwanda vya nguo na viatu kufanya biashara. “Serikali idhibiti magendo ya nguo yanayoweza kuathiri viwanda vya ndani na hata nguo zisizo na ubora. Uamuzi wa viongozi wa Afrika Mashariki ni sahihi na tunauunga mkono,” alisema Kamote.
Wafanyabiashara Baadhi ya wafanyabiashara waliohojiwa na gazeti hili walisema, ikiwa nguo za mitumba na samani za kichina zitapigwa marufuku, bidhaa zinazozalishwa nchini zitakua.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana,wafanyabiashara hao walisema kuwa, bidhaa hizo zinaingia kwa wingi nchini na kwamba zinauzwa kwa bei nafuu, jambo ambalo limechangia wananchi kuzikimbilia.

Mfanyabiashara mwingine, Issac Massawe alisema kuwa, kama Serikali itaamua kupiga marufuku uingizaji wa bidhaa hizo itasababisha samani kuadimika nchini. Hata hivyo, mfanyabiashara wa nguo za mitumba katika eneo la Manzese, Khamis Khatibu alisema ikiwa Serikali itazuia uingizaji wa nguo hizo utasababisha vijana wengi kukosa ajira.

Muuzaji wa duka la nguo za kike lililoko Sinza Madukani, Kuruthum Ally, alisema suala la kuzuia mitumba litakuwa gumu kwa wauzaji na watumiaji ambao ni wengi, lakini zaidi hatua hiyo itawaathiri wananchi wa hali ya chini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles