Na Kulwa Mzee – DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru wasanii 13 waliohusishwa na dawa za kulevya na kuwaamuru kuishi chini ya uangalizi wa kuwa na tabia njema kwa mwaka mmoja na wengine miaka mitatu.
Walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kufunguliwa maombi namba moja na mbili ya mwaka huu yaliyosomwa kwa mahakimu wawili tofauti.
Wasanii, wapenzi na wadau walijazana katika mahakama hiyo wakisubiri kujua hatima ya wajibu maombi waliokuwa wakishikiliwa na polisi takribani siku tano.
Wadau walikuwa wakikimbilia kila gari waliloliona likiingia katika eneo la mahakama wakidhani limewabeba wasanii hao bila mafanikio, lakini ilipotimu saa tano, waliingia wakiwa katika magari mawili.
Wasanii wanawake walipanda katika Noah yenye namba za usajili T 583 BPB na wanaume waliingia kwa gari la wazi lenye usajili namba T 643 ARQ Toyota Cruser.
HAKIMU SHAHIDI
Akisoma maombi namba moja mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, aliwataja wajibu maombi kuwa ni Hamidu Chambuso ‘Dogo Hamidu’, Rajabu Salum, Romeo Bangura ‘Romijons’, ambaye ni DJ wa msanii nyota, Nasib Abdul ‘Diamond’, Gedou Madigo, Khalid Mohammed ‘TID’, Johana Mathysen, Rechoel Josephat na Anna Kimario ‘Tunda’.
Katuga alidai Jamhuri imewasilisha maombi chini ya kifungu namba 73(E) na 74 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002 kwa kuambatanisha na hati ya kiapo iliyoapwa na Mratibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Dennis Majumba.
“Mheshimiwa hakimu, katika maombi yetu tunaomba vitu vitatu, Jamhuri tunaomba wajibu maombi wajidhamini wenyewe, wadhaminiwe na wawe katika uangalizi wa tabia njema kwa miaka mitatu.
“Pili tunaomba mahakama iwaamuru wajibu maombi wawe wanaripoti Kituo Kikuu cha Polisi angalau mara mbili kwa mwezi na tatu mahakama itatoa amri yoyote itakayoona inafaa,” alidai.
Katuga alidai Majumba katika kiapo chake anaeleza kwamba ana taarifa za kuaminika kupitia kesi za dawa za kulevya kuwa wajibu maombi wanajihusisha na dawa za kulevya na kutokana na tabia hizo kuwaacha katika jamii bila kudhibitiwa wanaweza kuleta uvunjifu wa amani.
Akijibu hoja hizo Wakili wa utetezi, Albert Msando, alidai kiapo kilichowasilishwa mahakamani hakitoi ufafanuzi taarifa zilizopatikana ni zipi na wajibu maombi kila mmoja anahusishwa na dawa zipi za kulevya maana kuna aina nyingi za dawa hizo.
Msando alihoji kifungu cha sheria kilichotumika kuomba wajibu maombi kuwa chini ya uangalizi, kifungu namba 73 (E) kwamba hakiendani na hoja zilizowasilishwa dhidi ya wajibu maombi.
Alidai kifungu hicho hakisemi lolote kuhusu dawa za kulevya na kwamba kinazungumzia wizi, kupokea mali za wizi na wale wenye makosa ya unyang’anyi.
“Mnasema wanaweza kusababisha uvunjifu wa amani, mtu anayetumia dawa za kulevya anasinzia, muda gani atavunja amani?” alidai Msando.
Katuga akijibu hoja za Msando alidai kiapo hakiwezi kueleza kila kitu, lakini pale ambapo mahakama itaona kuna haja ya kuwasilisha maelezo kwa upana, kifungu namba 79 cha CPA kinazungumzia ifanyike pale mahakama itakapokuwa imeshatoa uamuzi.
Akitoa uamuzi, Hakimu Shahidi alikubaliana na hoja za Wakili Msando kwamba kifungu namba 73(E) kimetumika kimakosa na badala yake mahakama ilifanya mabadiliko na kuweka kifungu namba 70 cha sheria hiyo ndiyo kitumike katika kuwasilisha maombi hayo kwani kinahusisha hoja ya uvunjifu wa amani.
“Pamoja na yote, mahakama inaamuru wajibu maombi wawe chini ya uangalizi wa tabia njema kwa kipindi cha mwaka mmoja ili iwe rahisi kujirekebisha na watasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 10 kila mmoja,” alisema Hakimu Shahidi.
HAKIMU MKEHA
Katika maombi namba mbili ya mwaka huu, yaliyosomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, wajibu maombi ambao ni Ahmed Hashimu ‘Petit Man’ ambaye ni shemeji wa Diamond na wenzake wanne, wameamuriwa na mahakama kuwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha miaka mitatu.
Hakimu Mkeha alitoa uamuzi huo baada ya upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, kuwasilisha maombi hayo kwa sababu imebainika wanajihusisha na dawa za kulevya.
Katuga aliwasilisha maombi hayo yaliyoambatana na hati ya kiapo iliyoapwa na ASP Majumba chini ya kifungu namba 73(E) na 74 cha CPA kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Aliwataja wajibu maombi kuwa ni TID, Said Linnah, Nassoro Nassoro, Bakari Khalee na Lulu Abbas ‘Lulu Diva’.
Wakili Katuga aliomba wajibu maombi hayo wawe katika uangalizi wa kipindi hicho, wajidhamini na wadhaminiwe, wawe na tabia nzuri, waripoti Polisi mara mbili kwa mwezi na amri nyingine yoyote itatolewe na mahakama kama itaona kuna haja ya kufanya hivyo.
Akijibu, Wakili Msando alidai anakubali maombi yaliyowasilishwa na Jamhuri, lakini anaomba wajibu maombi wajidhamini wenyewe na wasiwe wanaripoti Kituo cha Polisi.
Akitoa uamuzi, Hakimu Mkeha alisema sharti la wajibu maombi kuripoti Polisi haliepukiki na pengine linaweza kuepusha na mambo mengine.
“Mahakama inayakubali maombi ya Jamhuri, wajibu maombi kila mmoja atadhaminiwa na mdhamini mmoja wa kuaminika, watajidhamini wenyewe kwa dhamana ya maandishi ya Sh milioni 20.
“Watakuwa chini ya uangalizi kwa miaka mitatu kuanzia leo, wawe wenye tabia nzuri na wataripoti Kituo Kikuu cha Polisi mara mbili kwa mwezi,” alisema.
Wajibu maombi wote baada ya kukamilisha taratibu za mahakama walirudishwa Polisi kwa hatua nyingine za kuachiwa huru.