Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Wataalam 16 wa afya kutoka nchi sita za Afrika Mashariki wanapatiwa mafunzo katika kupima ubora na ufanisi wa dawa zinazotumika sasa na zile watakazozigundua.
Mafunzo hayo yameandaliwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Taasisi inayosimamia na kujenga uwezo katika kufanya tafiti za afya Afrika Mashariki (EACCR), Taasisi ya Utafiti ya Kilimanjaro (KCRI) na EDCTP.
Mratibu Mkuu wa Mafunzo kutoka EACCR, Profesa Reginald Kavishe, amesema miongoni mwa washiriki hao ni wafamasia, watafiti na wataalam wa maabara ambao wanajengewa uwezo katika suala zima la kupima dawa ili kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kufanya tafiti zinazohusiana na dawa.
“Sasa hivi kuna magonjwa mbalimbali na unakuta wakati mwingine hata dawa ambazo zimepitishwa wakati mwingine zinakuwa hazifanyi vizuri. Mfano tumeona kwenye malaria, HIV wakati mwingine tunaona hazifanyi kazi vizuri, kinachosababisha dawa zisifanye kazi vizuri hatuwezi kujua kama hatuna weledi wa kupima na kutathmini ni kitu gani kinasababisha.
“Inawezekana mgonjwa hatumii dozi kama inavyotakiwa na kusababisha dawa kwenye damu kutokufikia kile kiwango kinachotakiwa kutibu. Sasa kozi hii inakwenda kuwajengea uwezo wataalam wetu katika suala zima la kupima na kuweza kujua kwamba dawa ipo kwa kiwango kinachotakiwa kwenye damu,” amesema Profesa Kavishe.
Amesema pia kupitia mafunzo hayo washiriki wataweza kubaini kama vimelea vya ugonjwa vinajenga usugu na kumbadilishia mgonjwa dawa ama kushauri kitu gani kifanyike.
“Kama mgonjwa anatumia dawa lakini haponi mfano tukichukua sampuli kama ni damu, mkojo au hata mate tunaweza kupima na kujua kiwango cha dawa kilichoko mle ni kile kinachotarajiwa katika kuleta tiba, lakini wadudu au vimelea hawafi ni kwa sababu wamejenga usugu.
“Inaweza ikasaidia kumbadilishia mgonjwa dawa ama kushauri ni kitu gani kifanyike na endapo tutakuta dawa zipo chini ya kiwango ina maana pengine mgonjwa hatumii zile dawa kama alivyoelekezwa,” amesema Profesa Kavishe.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Elimu Endelevu na Maendeleo ya Weledi kutoka MUHAS, Profesa Deodatus Kakoko, amewataka washiriki kuzingatia mafunzo hayo na kuwa chachu kwa wengine.
“Sasa hivi tuna changamoto ya Covid, tuna changamoto ya HIV ambayo imedumu kwa muda mrefu zote hizi zinatuhitaji tuweke vichwa kwa pamoja ili tuweze kuzitatua,” amesema Profesa Kakoko.
Mmoja wa washiriki kutoka Chuo Kikuu cha Makerere Uganda, Kenda Tibira, amesema kupitia mafunzo hayo anatarajia kuongeza ujuzi na uwezo katika kufanya tafiti mbalimbali za afya.
EACCR inaratibu mafunzo katika nchi sita za Afrika Mashariki yaani Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia na Rwanda ambapo hutoa mafunzo ya ngazi tofauti kama vile Shahada ya Uzamivu, Shahada ya Uzamili na kozi fupi kwa ajili ya kujenga uwezo katika kufanya tafiti za afya.
Kwa kipindi cha 2017 – 2021 zaidi ya washiriki wa kozi fupi 200 wamepatiwa mafunzo, Shahada ya Uzamivu (watano) na Shahada ya Uzamili (26).