ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli amekosoa utendaji vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuacha dhahabu kutoroshwa Mwanza na kukamatiwa Kenya, huku Waziri wa Madini, Dotto Biteko, akisema wamekamata mtandao wa watu 12 wanaohujumu masoko ya madini hayo nchini.
Akizungumza Ikulu Dar es Salaam jana wakati akipokea fedha na dhahabu kilo 35.34 iliyotoroshwa Tanzania na kukamatiwa Kenya, Rais Magufuli alivipongeza vyombo vya ulinzi vya nchi hiyo kwa kukamata madini hayo yaliyotoroshwa Mwanza kwa ndege ambayo ilipitia Kilimanjaro (Kia), kabla ya kwenda Nairobi yalikokamatwa Februari 15 mwaka jana.
Dhahabu na fedha hizo ziliwasilishwa nchini na Mjumbe Maalumu wa Rais Uhuru Kenyatta, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Monica Juma.
Fedha za Tanzania Sh milioni 170, za Marekani dola 77,500 na za Kenya Sh 171,600 zilitoroshwa nchini mwaka 2004 baada ya kuibwa Benki ya NBC Moshi.
Kurudishwa kwa vitu hivyo, ni matunda ya ziara binafsi ya Rais Kenyatta, aliyemtembelea Rais Magufuli nyumbani kwake Chato hivi karibuni alipokuwa kwenye mapumziko.
ASHUKIA VYOMBO VYA ULINZI
Akizungumza jana, Rais Magufuli alisema; “dhahabu imetoroshwa kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza, ikapandishwa ikaenda mpaka Kia (Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro) akaenda mpaka Kenya.
“Hapa wa kupongezwa kwenye hii mali ni vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya.
“Najua wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama mko hapa, lazima niwatandike hapa hapa. Kwa sababu vimetoka uwanja wa Mwanza, vikaenda Kia, vilipofika Kenya, vile vyombo kabla ile mali haijasafirishwa kwenda Dubai vikashindwa.
“Sasa unaweza ukajiuza maswali mengi. Je, ilipokuwa ikibebwa kutoka Mwanza vyombo vya Tanzania vilikuwa vinafanya nini? Je, vilishirikiana na mhalifu au vilimwachia? Je, dhahabu ngapi zinapita bila watuhumiwa kushikwa? Hii nawaachia ninyi.
“Inawezekana kuna mahali mnafanya vizuri, lakini kuna sehemu mnalegalega. Hiki kilichotokea ya dhahabu kutoroshwa inadhihirisha aibu ya kwetu, kwamba tunaachia mali halafu inaenda kushikwa huko,” alisema Rais Magufuli.
Kutokana na hilo, Rais Magufuli alisema ataviandikia barua ya kupongeza vyombo vya ulinzi vya Kenya kwa kufanya kazi nzuri.
Alisema chanzo cha fedha hizo kurejeshwa ni baada ya kumwomba Rais Kenyatta kurejeshewa dhahabu hizo walipokutana Chato mkoani Geita.
“Kenyatta alipokuja Chato tulizungumza mambo mengi kuhusu mahusiano ya nchi hizi mbili. Hivi vitu vya dhahabu vinahitaji moyo wa jiwe. Kenyata ni mwaminifu ana upendo wa pekee pamoja na Serikali yake, vinginevyo zingepigwa kwa juu juu tu huko, lakini huu ni uaminifu wa hali ya juu sana.
“Na mimi mnipongeze basi kidogo, kwa sababu wangekuwa wengine tungepiga dili na Kenyatta, kwamba tupige juu kwa juu wala msingejua kama kuna dhahabu. Wakenya na Watanzania msingelijua hili, bali huu ni uaminifu na kumwogopa Mungu kwa mali za wananchi.
“Vyombo vya ulinzi vya Kenya oyeee. Hawa watu wamefanya kazi nzuri, zisingeshikwa leo tusingekuwa hapa wala Kenyatta asingemtuma waziri wake atoe ndege ya jeshi,” alisema Rais Magufuli.
Aliwataka wafanyabiashara na wachimbaji wa madini kuendesha shughuli zao kihalali, huku akiwakaribisha Wakenya kuja kununua madini kwenye masoko ya hapa nchini.
“Nawakaribisha ndugu zetu Wakenya kununua madini au kuwekeza mje hapa, sisi ni ndugu na hayupo atakayevunja undugu baina yetu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alitumia takribani nusu saa kuzungumza na Kenyatta kwa simu wakati akiendelea kuzungumza na viongozi walioshiriki hafla hiyo.
Yafuatayo ni namna mazungumzo hayo yalivyokuwa:
Rais Magufuli: Hallo.
Rais Kenyatta: Mheshimiwa Rais habari yako ndugu yangu.
Rais Magufuli: Nzuri bwana, mzigo umeshafika (akimaanisha dhahabu na fedha).
Rais Kenyatta: Nilikuwa nimeingia kwa kikao kidogo nikaacha simu kando.
Rais Magufuli: Ahaa, basi mimi nakushukuru sana.
Rais Kenyatta: Asante.
Rais Magufuli: Dada yangu Monica (Monica Juma, mjumbe maalumu wa Kenyatta ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje wa Kenya) ameshashusha mzigo wote, nimeuangalia hapa.
Rais Kenyatta: Asante, asante, asante sana, tumesema kwamba mali ya wananchi wetu lazima irudi kwa wananchi wetu.
Rais Magufuli: Sawa kabisa. Endelea wanakusikiliza hapa.
Rais Kenyatta: Tumesema kwamba sisi kazi yetu ni kuhakikisha tumelinda mali za wananchi wetu na mali hiyo iweze kuwajengea wananchi hospitali, barabara, shule. Walaghai hawa hawana nafasi kwa nchi zetu kabisa.
Rais Magufuli: Safi kabisa.
Rais Kenyatta: Mimi nasema tuendelee kushirikiana, Kenya na Tanzania hatuna mipaka, sisi ni kitu kimoja, tusaidiane. Kwa hayo machache, nasema tuendelee na uhusiano mwema na ujirani mwema, lazima tuendelee pamoja.
Rais Magufuli: Mimi nakushukuru sana, tutaendelea kupendana mpaka maendeleo ya Kenya na Tanzania yaweze kupatikana.
Rais Kenyatta: Ndio.
Rais Magufuli: Lakini la mwisho nataka kuwapongeza sana vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya kwa sababu hii mali ilitokea Tanzania haikushikwa na vyombo vya ulinzi vya Tanzania.
Rais Kenyatta: Ndio.
Rais Magufuli: Ilipofika Kenya ikashikwa, kwa hiyo vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya wanajituma kikamilifu, fikisha shukrani zangu na pongezi kwa waliohusika wote.
Rais Kenyatta: Hiyo pongezi na hongera zitafika.
Rais Magufuli: Asante sana.
BITEKO ALIVYOFICHUA MTANDAO WA WATU 12
Kwa upande wake, Biteko alisema wamewabaini watu 12 ambao ni mtandao na tayari wako ndani wakipatiwa elimu polepole.
“Mheshimiwa Rais, wako waliotaka kuhujumu masoko yako, kwa nia hiyo hiyo ovu wakaanzisha utaratibu wa kununua pembeni kwenye masoko, kama sokoni inauzwa gramu moja ya dhahabu Sh 92,000 wao wananunua kwa Sh 96,000 niliwasiliana nawe ukanipa maelekezo maalumu.
“Naomba nieleze ukweli, sekta hii bila vyombo vya ulinzi na usalama sisi wizara peke yetu hatuwezi, tayari tumewatambua watu 12 ambao sasa wako ndani wanapewa elimu polepole, maana wewe ulisema twende nao polepole.
“Tangu tumeanzisha opesheni hii, jana (juzi) nikiwa Geita, watu wanaopeleka dhahabu kwenye masoko wanapanga foleni utadhani ni yale maduka ya ushirika ya zamani, watu ni wengi sana,” alisema Biteko.
Vilevile Biteko alisema tangu yalipoanzishwa masoko ya madini mapato katika sekta hiyo yamepanda.
“Tangu umesema masoko yaanzishwe, tulichokuwa tunakipata kwa mwaka mzima, leo tunapata kwa siku moja. Mfano Chunya mwaka mzima ilikuwa inapatikana kilo 12, lakini leo ni kilo 270 zimefanyiwa biashara kwenye soko hilo.
“Geita nayo hivyo hivyo kilo 736 zimeuzwa, na Sh bilioni 136.7 zimefanyiwa biashara kwenye masoko yote nchini,” alisema.
Alisema anashangazwa na baadhi ya watu wanaposema Rais Magufuli anawakimbiza wawekezaji na kwamba tangu mwaka 2010 hawajawahi kutoa leseni za gharama kubwa za uwekezaji.
“Katika kipindi chako tunayo leseni mbili tutazitoa kwa ajili uchimbaji mkubwa. Ambazo tumezitoa kwa uchimbaji mdogo ni leseni 2,673, leseni za kati 32 na leseni za utafiti 105,” alisema.
IGP SIRRO
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro aliomba msamaha kwa niaba ya jeshi hilo kuhusu dhahabu hizo kutoroshwa huku akiahidi kosa hilo halitajirudia.
“Kwa niaba ya wenzangu, kwanza tuombe radhi kwa kukutia aibu kwa sababu mali hii imekamatwa Kenya na sisi mishahara yetu tunalipwa na Watanzania.
“Hivyo mheshimiwa Rais ulichotoa kwetu maelekezo ni amri, wanasema kufanya kosa mara moja sio kosa, lakini kurudia kosa ndio kosa zaidi. Nikuhakikishie tutajipanga vizuri.
“Nitoe salamu wale ndugu zetu ambao ni wahalifu wakidhani wanaweza kucheza kama nyuma, wakiendelea wasilaumu Serikali, madini ni mali yetu. Ulinzi wa mali yetu lazima tushirikiane sote,” alisema IGP Sirro.
DPP
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, alisema ushirikiano kati ya ofisi yake na ya DPP wa Kenya imefanikisha kurudishwa Tanzania dhahabu na fedha hizo.
“Februari 15, 2018 dhahabu ya kilo 35.34 ilikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta wakati msafiri mmoja aliyekuwa akisafiri kwa ndege ya Presission Air kutoka Mwanza alikamatwa,” alisema Mganga.
Alisema baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa, wakurugenzi wa upelelezi wa Kenya na Tanzania walianza upelelezi, na aliongoza timu ya watu 11 kuhakikisha dhahabu hiyo inarejeshwa.
Mbali na timu hiyo, Mganga alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi aliandika maombi kwenda Kenya kuhakikisha dhahabu hiyo inarejeshwa na kutumika kama kielelezo cha kesi.
Alisema kesi hiyo namba 8 ya 2018 ya uhujumu uchumi imefunguliwa jijini Mwanza.
“Tulipofika nchini Kenya tuliongea kwa undani na ndugu yangu Rubin Haji (DPP wa Kenya) na viongozi wengine kuhakikisha dhahabu hiyo inarudi,” alisema.