23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

DC Sabaya atuhumiwa kwa rushwa, akana

Waandishi wetu-Hai

MKUU wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, anachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kutokana na malalamiko yaliyotolewa, kwamba analazimisha wafanyabiashara kumpa rushwa.


Mfanyabiashara wa utalii wa Kampuni ya Asante Tours, Cathberty Swai, alimtuhumu Sabaya kumpa vitisho na kudai fedha kwa nguvu ikiwa ni pamoja na kuwakamata wafanyakazi wake na kuwaweka mahabusu.


Swai alisema hayo katika kikao cha wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kilichofanyika jana Moshi mkoani Kilimanjaro.


Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu, alipotafutwa na MTANZANIA kuhusu suala hilo, alisema ofisi yake ipo katika mchakato wa kuzungumza na mfanyabiashara huyo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, alisema yeye alifungua kikao hicho cha TRA na kuondoka, kwa hiyo sasa anasubiri taarifa ya yaliyojiri ili aifanyie kazi.


Swai akizungumza katika mkutano na TRA, alidai mkuu huyo wa wilaya amekuwa ni kikwazo kwa wawekezaji na wafanyabiashara.


Alisema licha ya kulipa kodi serikalini, kiasi cha Sh milioni 148 kwa mwaka, lakini amekuwa akipokea vitisho na manyanyaso kutoka kwa mkuu huyo wa wilaya na kumlazimisha kumpa fedha.


Alidai mara kwa mara Sabaya amekuwa akivamia katika hoteli yake ya kitalii ya Weruweru River Lodge usiku kwa madai kuwa anakusanya kodi.
Swai alisema Sabaya akiwakuta wafanyakazi na wakashindwa kumpa majibu, huwachukua na kuwaweka mahabusu bila sababu za msingi.


“Amekuwa akija usiku hotelini na ile ni hoteli ya kitalii na alipomkuta meneja na akimuuliza maswali akashindwa kumjibu maana siyo kazi yake, alimchukua na kumweka ndani na kumtoa asubuhi, nilipomfuata kufahamu shida nini, alisema anataka Sh milioni tano, ametumwa na anafanya kazi ya Serikali,” alidai.


Swai alidai kuwa Sabaya alimweleza kwamba anaweza kuitafsiri kauli hiyo kama ni sawa na ya mkuu mmoja wa mkoa nchini ama rushwa.
“Alisema anahitaji hiyo fedha na anaripoti moja kwa moja juu.

Nilimpa milioni mbili, lakini bado alininyanyasa, na nilimfuata mfanyabiashara mwenzangu kuomba ushauri, alinishauri nimpe tu hizo fedha na kuniambia nikicheza na mjinga atanipasua jicho,” alidai.


Alidai baada ya kumpa fedha hizo, alikuja tena na kumpa milioni mbili kwa mara ya pili na mara ya tatu milioni mbili na akarudi tena kuvamia hoteli hiyo na kufanya fujo huku akiambatana na walinzi wake wawili.


“Nimesema haya nikiwa sijui hatima yangu itakuwaje, lakini mpaka sasa nimeshampa Sh milioni 10 na alikuja na kufanya fujo ambapo nilikuwa na mteja wangu mwenye wafuasi zaidi ya elfu 30,000, alimsumbua sana,” alidai.


Alidai mbali na hilo, alikuwa akiwachukua wasanii wa kucheza na nyoka kutoka Kanda ya Ziwa na kuwaleta hotelini hapo na kuwalipa, lakini Sabaya alikwenda na kuwafukuza huku wakiwa wameingia makubaliano ya kufungua bustani ya nyoka (snake park).


“Sijui hatima yangu itakuwa nini lakini nimeamua kuzungumza kwamba tunanyanyaswa tena sana, hatuna amani na kitakachonipata ni yeye, lakini sifikirii kama hata Rais anaweza kukubaliana na jambo kama hili, sisi tunalipa kodi ya Serikali na hatudaiwi kwanini tuteseke?” alisema.

SABAYA AJIBU
Jana Sabaya alikana tuhuma hizo huku na akatangaza kumnyang’anya mfanyabiashara huyo mashamba yake, na kuagiza polisi kumkamata.
“Tuhuma hizo zimetengenezwa na hazina ukweli wowote, wala sijawahi kumwomba rushwa,” alisema.


Pia jana Sabaya alitangaza kumnyang’anya Swai mashamba aliyodai aliyopora kwa wananchi wa Kijiji cha Kimashukuru akisema amepewa na Serikali ya kijiji hicho.


Sabaya alidai kuwa Ijumaa iliyopita ndiyo alipokea malalamiko hayo ya wananchi kuporwa mashamba na kuagiza uchunguzi ufanyike.
Katika mashamba hayo, kuna ngamia na nyani wanaofugwa na mfanyabiashara huyo.


Sabaya alidai wananchi walikuwa wakimiliki mashamba hayo tangu mwaka 1971.
Alidai kuwa Swai alivamia mashamba hayo yenye ukubwa wa zaidi ya hekari 15 na kufanya shughuli za utalii.


“Nilipokea taarifa za uporaji wa mashamba kutoka kwa wananchi wa kijiji hiki kuwa wameporwa, na niliunda kamati ya kuchunguza jambo hili na kugundua kuwa wakulima hao wamedhulumiwa.


“Kamati niliyounda ilifanya kazi chini ya Katibu Tawala (Das) Upendo Wella na ilitoa mapendekezo kuwa waliochukuliwa mashamba hayo warudishiwe na kulipwa fidia,” alisisitiza.


Pia aliagiza polisi kumkamata mwekezaji huyo na kumfungulia mashtaka ya kuendesha shughuli za kitalii katika mashamba hayo kinyume na taratibu.

HABARI HII IMEANDALIWA NA UPENDO MOSHA, SAFINA SARWATT NA OMAR MLEKWA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles