WACHIMBAJI wadogo wa almasi wilayani Kishapu, maarufu kwa jina la Wabeshi, wamemuomba Rais John Magufuli kuwasaidia kutengewa eneo la kuchimba madini hayo, anaripoti Kadama Malunde.
Kwa mujibu wa wachimbaji hao, hatua hiyo itawasaidia kupunguza uvamizi wa Mgodi wa Almasi wa Williamson.
Wakizunguza na waandishi wa habari hivi karibuni kwa nyakati tofauti, Wabeshi hao walisema vijana wengi wakazi wa maeneo yanayozunguka mgodi huo wamekuwa wakitafuta namna ya kujiajiri.
Mabula Njile mkazi wa kijiji cha Nyenze Kata ya Mwadui Luhumbo, alisema endapo serikali itawapatia maeneo kwa ajili yao sehemu kubwa ya vijana hao hawataendeela na uvamizi mgodi wa Williamson.
Juma Ng’ombeyapi kutoka Kijiji cha Ng’wang’holo, alisema hajawahi kuona kiongozi yeyote wa juu wa serikali akifika katika maeneo yanayozunguka mgodi huo kusikiliza kero za wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba alionyeshwa kushangazwa na madai ya wachimbaji hao ambao alisema tayari walishapewa maeneo ya kuchimba lakini hawataki kuyaendeleza.