Na Renatha Kipaka, Kagera
Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini (TASAF) mkoani Kagera wametakiwa kutumia fedha wanazopata kwa malengo yaliyokusudiwa ili ziweze kuwasaidia kuondokana na utegemezi.
Wito huo umetolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila, kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo, katika kikao cha kujadili na kutathimini mpango huo mkoani humo ambacho kilienda sambamba na kuwatembelea wanufaika wa Tasaf.
Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Ihangilo na Kamishango, Nguvila amesema fedha hizo zinatolewa kwa ajili ya kuinua vipato vyao ili waondokane na umaskini hivyo hawanabudi kuzitumia vizuri.
“Wapo baadhi ya wanufaika wakishapata hizi fedha wanazitumia kulipia mahari kwa ajili ya kuongeza mke mwingine, wengine wanashinda wanakunywa pombe. Lengo la Serikali ni kumiliki mali kama mbuzi, ng’ombe, kuku, kuweza kumudu kula milo mitatu na kukaa kwenye nyumba nzuri,” amesema Nguvila.
Amewataka watalam walio katika mpango wa kunusuru kaya maskini mkoani humo kuwatembelea mara kwa mara wanufaika hao kwa ajili ya kuangalia maendeleo yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Kagera, Constansia Buhiye amewataka wanufaika hao kuwa mabalozi wazuri katika matumizi sahihi ya fedha hizo na kuwasisitiza kuzitumia fedha vizuri kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi kama yalivyo malengo ya serikali ya chama hicho.
Nae Mkurugenzi wa Ukaguzi kutoka makao makuu ya TASAF, Shedrack Mziray ameeleza kuwa wameweka mikakati ya wanufaika kuwa wanalipwa kwa njia ya mtandao hasa wenye vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa lengo la kuondoa changamoto ya malalamiko ya kutolipwa fedha zao.
Baadhi ya wanufaika wa mpango huo katika vijiji vya Kamishango na Ihangilo, Valelia Alfred na Eradius Rwenyagila wameshukuru serikali kwa kuwapatia ruzuku ya fedha hizo ambazo zimewasaidia kuinua vipato vya familia zao.
Mkoa wa Kagera una jumla ya wanufaika wa TASAF 81,306 kwa kipindi cha pili cha awamu ya tatu.