Na Seif Takaza, Iramba
MKUU wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda, amewahimiza wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) wilayani hapa, kutumia fedha walizopata kununulia mbegu bora na pembejeo kwa ajili ya maandalizi ya kilimo msimu huu.
Akizungumza na wanufaika wa mpango huo katika vijiji vya Kitukutu na Kyengege, hivi karibuni, Mwenda amesema Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwa shughuli za maendeleo katika nyanja zote, hivyo kila mmoja awajibike katika kufanya kazi za uzalishaji mali ili kila mwananchi aondokane na umaskini .
‘’Ndugu zangu wanufaika na mradi huu wa kunusuru kaya maskini nawaombeni mtumie fedha hizi mlizopata kwa ajili ya kununulia mbegu bora na pembejeo za kilimo kwa ajili ya kilimo msimu huu, hivyo kila mmoja wenu anatakiwa kujipanga vizuri katika matumizi mazuri ya fedha hizo,” Amesisitiza Mwenda.
Amewataka wananchi wa wilaya hiyo walime mazao ya chakula na biashara ili kila kaya kuwa na chakula cha kutosha.
‘’Serikali yenu imetoa ruzuku kwa ajili ya zao la alizeti hivyo mnapaswa kujiandaa vizuri na kilimo msimu huu wa kilimo ili muweze kulima alizeti kitaalam na kwa kutumia mbegu bora tuweze kujitosheleza kwa mafuta ya kupikia,’’ amesema.
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF wa Halmashauri hiyo, Frida Lwanji amesema mpango wa kunusuru kaya maskini unaendelea kutekelezwa kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi .
‘’Mpango huu wa kunusuru kaya masikini umesaidia kuziwezesha kaya hizo kupata huduma za kijamii kama vile chakula na mavazi na kuanzisha miradi ambayo imewaongezea kipato.
“Katika miradi hiyo baadhi ya kaya zimepata maendeleo ambapo wengine wamefuga kuku, mbuzi,nguruwe na wengine wamejenga nyumba kwa kutumia fedha za ruzuku wanazopata.
‘’Wilaya ya Iramba ni miongoni mwa wilaya ambazo zinazotekeleza mradi wa kunusuru kaya maskini na tunatekeleza katika vijiji 51, na jumla ya kaya 5164 zinanufaika na mpango huo ambapo ni sawa na asilimimia 70 lakini pia tunatarajia kunufaisha walengwa wa wa mradi huu kwa vijiji 27 ni sawa na asilimia 30 malipo haya tunayofanya sasa ni kwa miezi Mei na Juni 2021,” amesema Lwanji
Naye Ofisa ufuatiliaji wa mpango wa TASAF,Andrew Nguni amesema jukumu lake ni kufuatilia miradi kwa wanufaika wa kaya masikini kuwa katika ubora unaotakiwa
‘’ Miradi ninayofuatilia ni pamoja na ajira ya muda mfupi, uhaulishaji wa fedha mradi wa timiza malengo kwa wasichana balehe waliopo mashuleni na nje ya mfumo wa shule na kuweka akiba na kuwekeza’’amefafanua Nguni .
Naye mnufaika wa kijiji cha Kitukutu, Rozi Donki ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia kwa kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile ujenzi wa zahanati , vituo vya afya ,ujenzi wa madarasa miradi ya maji, barabara na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Edson Selemani wa kijiji cha Kyengege alimhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa wanamuunga mkono Rais Samia katika shughuli za maendeleo na kushukuru kwa kuwapelekea mbegu bora ya alizeti na pembejeo nan kumuomba Mkuu wa Wilaya zipekwe mapema.