WKHAMIS SHARIF
-ZANZIBAR
MWENYEKITI wa Shehia ya Tumbatu Jongowe, Zanzibar, Miza Ali Sharif, amesema suala la wanawake kushindwa kutoa taarifa za utelekezwaji linalofanywa na waume zao ni tatizo kubwa ambalo huwaathiri kisaikolojia.
Amesema hatua hiyo inatokana na wanawake wengi kuhofia kunyooshewa vidole au kutengwa na jamii.
Akizungumza na MTANZANIA jana katika mahojiano maalumu, Miza alisema katika eneo lake vitendo vya utekelezwaji dhidi ya wanawake na watoto vimekuwa vikishamiri kila kukicha.
Mwenyekiti huyo alisema hali hiyo imekuwa ikichangia kuongezeka kwa idadi ya wanawake walioachika na kushindwa kutoa taarifa jambo linalofanya waendelee kuteseka bila kuwa na msaada.
Alisema tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo amepokea lalamiko moja la mwanamke ambaye aliachwa na mume na kutelekezwa na watoto bila matunzo.
“Si kama matendo haya hayapo, lakini wanawake wenyewe wanashindwa kutoa taarifa kwa kuhofia kuoneshewa vidole,” alisema Miza.
Akizungumzia kuhusu utelekezaji wa wanawake kwa wanaume wanaoenda kuvua ‘dago’, alisema hilo limepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na wanaume sasa kuweka muda maalumu wa kukaa dago.