25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wanawake watakiwa kujitokeza kupima saratani ya mlango wa kizazi Kagera

Na Mwandishi Wetu, Kagera

ZAIDI ya Wanawake 600 mkoani Kagera wanatarajiwa kufikiwa na mradi wa uhamasishaji wanawake wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi kupima saratani ya mlango wa kizazi ifikapo Desemba mwaka huu.

Hayo yamebainishwa juzi mjini Bukoba na Mkurugenzi wa Habari na Uraghibishi kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Jumanne Isango wakati wa uzinduzi wa mradi huo.

Mkurugenzi wa Habari na Uraghibishi kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Jumanne Isango.

Amesema saratani ya mlango wa kizazi ni hatarishi sana kwa wanawake wanaoishi na VVU na ndio maana wametilia mkazo katika eneo hilo ili kujali afya za wananchi.

“TACAIDS kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia uwezeshaji wa Wanawake, (UN-WOMEN) wanatekeleza mradi wa uhamasishaji wanawake hasa wanaoishi na VVU kuchunguza saratani ya mlango wa kizazi mkoani Kagera wilaya ya Bukoba.

“Huu utakuwa ni mradi wa majaribio lakini pia tunatekeleza moja kwa moja kwani lengo ni kujali afya za wananchi wetu ikizingatiwa kua Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye maambukizi makubwa ya VVU,” amesema Isango na kuongeza kuwa:

“Katika mradi huu tunategemea kuona mwitikio mkubwa kwa wanawake waishio na VVU wakijitokeza kufanya uchunguzi. Tumeanza na Bukoba vijijini katika kata tano ambapo tunatarajia kufikia wanawake 600 kufikia Desemba mwaka huu watakaokuwa wamejitokeza kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi.

“Hivyo, tuna uhakika kabisa kuwa hii vita tutaishinda kwani nyenzo tunazo na uwezo hivyo jambo la msingi ni kuweka mikakati imara ambayo itatufikisha katika adhma ya kutokomeza ugonjwa huu,” amesema Isango.

Aidha, katika hatua nyingine Isango amebainisha kuwa kwa tayari kuna wanawake 25 kutoka Shirika la Wanawake wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi mkoani Kagera (AMWAVU) ambao wamepewa elimu juu ya dalili za saratani.

“Tayari kwa Kagera kuna wanawake 25 kutoka AMWAVU wameshapatiwa mafunzo juu ya saratani ya mlango wa kizazi juu ya dalili zake na namna inavyofanyika jambo ambalo tunaamini kuwa watapanua wigo wa elimu kwa wengine na kusaidia juhudi hizi kwani tayari wameanza kutoa elimu ndani ya kata za Bukoba zikiwamo Maluku, Kabagaile na Kemondo,” amesema Isango.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Moses Machali.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jen. Charles Mbuge, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Moses Machali amesema upande wao watahakikisha kuwa kampeni hiyo inafanikiwa kwani walikuwa wakiiongejea kwa muda mrefu.

“Kutokana na madhara ya saratani ya mlango wa kizazi unaowakabili wanawake wa mkoa wa Kagera nawahakikisha kwamba mradi huu sisi serikali mkoani hapa tutausimamia vizuri ili uweze kufanya vyema katika kuokoa maisha ya wanawake wengi wa mkoa wetu hasa wanaoishi na VVU.

“Nasi tuungane na taasisi nyingine za kiraia ikiwamo Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kupambana na saratani ya mlango wa kizazi pamoja na VVU ili siku moja tatizo hili lije kuwa asilimia 0.

“Kwani takwimu zinaonyesha kuwa nchini Tanzania kati ya wanawake 1,000 basi 50 wana ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi, hizi siyo taarifa nzuri hivyo ni wajibu wetu kuchukua hatua. Pia Tanzania ndio inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa saratani kwa Ukanda wa Afrika Mashariki huku Kanda ya Ziwa tatizo likiwa kubwa zaidi, na hali inaonyesha kuwa wenye VVU ndio walioko kwenye hatari ya kupata ugonjwa huu kirahisi,” amesema Machali na kuongeza kuwa asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi hufariki dunia ndani ya miaka mitano kutokana na kuchelewa kuanza matibabu.

Upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika lisolokuwa la Kiserikali la AMWAVU ambao ndio watekelezaji wa mradi huo, Gasper Lutainulwa, amesema kuwa wao pamoja na kutekeleza miradi mingine waliibua mradi wa saratani ya mlango wa kizazi na kwamba upo uhusiano mkubwa kati ya ugonjwa huo na VVU.

“Wanawake waishio na Virusi Vya Ukimwi wapo kwenye hatari zaidi ya kupata saratani sababu kinga zao za mwili zipo chini kidogo, hii ndio sababu iliyotusukuma kuja na mradi huu ili kuwasaidia wananchi wa Kagera.

“Mradi huu wa saratani ya mlango wa kizazi ni wa uhamasishaji kwa wanawake waishio na VVU wakiwa ndio walengwa wa moja kwa moja, hivyo wajitokeze kuchunguza dalili za awali za saratani hii. Tunategemea kuona mwitikio mkubwa kwa wanawake wa Kagera.

 “Hivyo, tupo tayari kuhakikisha ajenda yetu hii inatekelezeka kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo serikali,” amesema Lutainulwa.

Aidha, katika hatua nyingine Lutainulwa ametoa ombi kwa serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na wadau wengine kuona uzito wa kusaidiwa kuwakinga na saratani kwa wanawake wanaoishi na VVU kwa ajili ya kulinda kizazi cha sasa na kijacho.

“Tutoe ushirikiano mkubwa na pengine tuangalie kuwa akina mama hawa wanayo sababu ya kusaidiwa, pia tulitizame kwa jicho la tatu kwamba wanawake waishio na VVU tukiwasaidia katika eneo hili la kuwakinga na saratani tutakuwa tumesaidia kizazi hiki na kijacho,” amesema Lutainulwa.

Awali, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Safina Yuma amesema pamoja na kwamba Mwanamke yeyote kuwa na hatari ya kupata saratani ya mlango wa kizazi lakini wenye VVU wako kwenye hatari zaidi.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Safina Yuma. Picha| Mtanzania Digital.

“Niwaombe wadau mbalimbali kushirikiana na serikali katika kupamba na tatizo hili, kwa sasa kuna vituo takribani 700 nchini vinavyotoa huduma hii ya uchunguzi bure, hivyo tuhimize jamii ijitokeze kufanya uchunguzi kutokana na wenye VVU kuwa na hatari kubwa ya kupata saratani hii,” amesema Dk. Yuma.

Upande wake, Mratibu wa Programu za Ukimwi na Jinsia kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia uwezeshaji wa Wanawake, (UN-WOMEN), Jacob Kayombo, amesema kuwa kutokana na taarifa kutoka wizara ya afya na wadau wengine, wameona nibudi kutoa mchango katika eneo la saratani ya mlango wa kizazi kwa kina mama ikiwa kusaidia kufanikisha juhudi za serikali.

Mratibu wa Programu za Ukimwi na Jinsia kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia uwezeshaji wa Wanawake, (UN-WOMEN), Jacob Kayombo, akizungumza wakati wa uzinduzi huo. Picha| Mtanzania Digital

“Tumeona tutoe mchangamo mwingine katika mapambano haya ya serikali katika saratani ya mlango wa kizazi, mkoa wa Kagera umekuwa na suhirikiano sana kwani tangu tumeanza kuwasiliana umekuwa ukituongoza na taratibu za kufanikisha kampeni hii zimekuwa zikifanyika katika hali rahisi sana.

“Tunashukuru kwamba wadau mbalimbali wamekuwa na ushirikiano mkubwa katika zoezi hili, hivyo UN-WOMEN itaendelea kufanyakazi kwa karibu na serikali ikiwamo kutoa mchango pale litakapohitajika, hivyo tunaamini kuwa kwa hiki kinachofanyika hapa basi kitaenda kufanikiwa na kuwafikia watu wengi kwa ajili ya ustawi wa raia wetu wa Tanzania,” amesema Kayombo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles