Anna Ruhasha, Mwanza
TAKWIMU za kuanzia Septemba, 2019 hadi Oktoba mwaka 2020 za maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI (VVU) katika Halmashauri ya Buchosa iliyopo Wilayani Sengerema mkoani Mwanza ni asilimia 7.7 kiwango ambapo wanawake wameogoza.
Taarifa hizo zimetolewa na Mratibu wa UKIMWI katika Halmashauri hiyo, Frolian Mkangara, ambaye amesema wanaoishi na VVU katika Halmashauri ya Buchosa wanakadiriwa kuwa 17,795, wanaume kuanzia umri wa miaka 15 ni 6,390 na wanawake umri kuanzia miaka 15 ni 9,807 .
Aidha ameongeza kuwa watoto chini ya miaka 15 waliogundulika na VVU wakiume walikuwa 1,627 na wakike 1,385 na vituo 37 vimeweza kutoa huduma za upimaji na dawa za kufubaza makali ya VVU bure.
“Pamoja na takwimu hizo mgeni rasmi bado wanawake katika Halmashauri ya Buchosa wanaongoza hasa kuanzia umri wa miaka 24 -49 kulinganisha na wanaume wa umri huo,”amesema.
Kwa upande wake Mkurungenzi wa Halmashauri ya Buchosa, Paulo Malala ametumia Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kuitaka jamii kupima afya zao kila mara na kuchukua tahadhari kwa kutumia kinga.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti Ukimwi ambaye ni Diwani wa Kata ya Katwe, Maximilian Laurenti, amesema kuwa licha ya kundi la wanawake kuongoza takwimu za kuanzia maambukizi yameshuka kutoka asilimia 7.7 na kufikia asilimia 4.5 .
“Takwimu za kuanzia mwezi Oktoba 2020 hadi September 2021 jumla ya wananchi wapatao 42,395, wanawake 24, 299 na wanaume 18,096 kati yao waliogundulika na VVU wanawake ni 1,101 na wanaume 795 na kushusha kiwango cha maambukizi kufika asilimia 4.5” amesema Laurent